BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HAYA NDIYO YALIYOSABABISHA RAIS MSTAAFU KARUME NA MAALIMSEIF KUKUTANA FAGHALA VISIWANI ZANZIBAR.

Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ, Maalim Seif Sharif Hamad wakifurahia jambo wakati wa mazungumzo yao nyumbani kwa Karume, Mbweni mjini Zanzibar.

ZANZIBAR. 

Rais Mstaafu wa Zanzibar awamu ya sita, Dk Amani Abeid Karume amekutana na viongozi wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar na kujadiliana hali ya kisiasa iliyojitokeza katika mjadala wa Katiba Mpya, pamoja na kujitoa kwa wabunge wa Ukawa kwenye vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa viongozi hao wamekutana faragha Aprili 30, nyumbani kwa Rais huyo mstaafu eneo la Mbweni mjini Unguja.


Viongozi wengine walioshiriki mazungumzo hayo ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Mkurugenzi wa Uenezi, Habari na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Abdallah Bimani, Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo na Katibu Mtendaji wa Kamati hiyo, Mansoor Yussuf Himid.


Wajumbe wengine katika msafara huo walikuwa ni Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu na Eddy Riyami huku mjumbe mmoja wa kamati hiyo, Aboubakary Khamis Bakary ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria wa (SMZ) akikosekana.


Imeelezwa kuwa kamati hiyo ilitoa muhtasari wa mwelekeo wa mjadala wa Katiba Mpya na sababu za wajumbe wa Ukawa kutoshiriki vikao vya Bunge la Katiba.


Kamati hiyo ilitaja ni Bunge hilo kutawaliwa na ushabiki, vijembe, matusi na kebehi, huku ikielezwa pia kuwapo na dhamira ya kupuuzwa maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba.


Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Mzee Moyo aliithibitishia jana kamati yake kukutana na Rais mstaafu Karume, ingawa alikataa kuelezea lolote lililojadiliwa wala kutaja azimio lililofikiwa baada ya kikao hicho kumalizika.


“Ni kweli kamati yangu ilikutana Rais Mstaafu Karume nyumbani kwake, wala si kificho, tumekubaliana Jussa atakuwa ndiye mzungumzaji wa yale tuliyoyazungumza na kuafikiwa, yeye na Mansoor ndiyo makatibu watendaji wa kamati yetu,”alisema Mzee Moyo.


Gazeti hili lilipompigia simu Rais Mstaafu Karume ili aeleze ajenda na madhumuni ya kikao hicho, hakuwa tayari kueleza lolote.


Hata hivyo, baada ya kumalizika mkutano huo, baadhi ya viongozi hao akiwamo Maalim Seif , Jussa na Mzee Moyo walikwenda moja kwa moja kushiriki mkutano wa hadhara wa Ukawa uliohutubiwa na viongozi wa juu wa CUF, NRA, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi na NLD.


Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF, ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ismail Jussa akizungumza na Mwananchi Jumapili amesema kwamba walikutana na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Karume kama waanzilishi wa maridhiano ya kupatikana kwa mwafaka wa kisiasa Zanzibar na hatimaye kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.


Alisema katika mkutano wao na Rais Mstaafu Karume, walizungumza kuhusu jinsi ya kulinda maridhiano na Serikali ya Umoja wa Kitaifa hasa kutokana na kuwapo baadhi ya watu wenye mwelekeo wa kutaka kuvuruga maridhiano hayo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: