BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI KUFUTA MISHAHARA YA VAT, NI KILIO CHA PROFESA IBRAHIM LIPUMBA.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
DAR ES SALAAM. 

Serikali itawasilisha bungeni rasimu ya maboresho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo itafuta misamaha ya kodi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema jana kwamba mpango huo unafanyiwa uchambuzi na Serikali na kwamba utawasilishwa katika Bunge la Bajeti wiki mbili zijazo.


Kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa CUF ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa akipigia kelele juu ya wingi wa misamaha ya kodi akisema imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha mapato ya Serikali.


Profesa Lipumba alisema hivi karibuni kuwa ili kuondoa kasi ya ukuaji wa nakisi, Serikali inatakiwa kufuta kabisa misamaha holela ya kodi inayofikia Sh1.8 trilioni ambayo ni sawa na asilimia tano ya pato la taifa.


Siku tano zilizopita, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, wakati akiwasilisha mpango wa Bajeti ya mwaka 2014/15 kwa wabunge, alisema Serikali imepanga kukamilisha utungwaji mpya wa Sheria ya VAT.


Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na kuongeza wigo wa kodi kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kuanzisha vyanzo vipya pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iingie kwenye mfumo rasmi wa kodi.


Katika bajeti ya mwaka 2013/14, Serikali iliondoa msamaha wa VAT kwa viwanda vya nguo vinavyotumia pamba ya ndani.


Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya taasisi ya CRC Sogema ambayo inaishauri Wizara ya Fedha, misamaha chini ya Kodi ya VAT ilifikia Sh802 bilioni kwa mwaka 2012, wakati jumla ya misamaha yote ilikuwa Sh1.8 trilioni.


Ripoti hiyo ya mwaka 2013 inasema: “Matokeo ya utafiti huu muhimu yanapendekeza kuwa kuna ufanisi zaidi kwa nchi zinazoendelea kujikita zaidi katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kuliko kutoa misamaha ya kodi kwa mashirika.”


Jana, Lukuvi alisema: “Serikali ina mpango huo na hivi sasa rasimu ya VAT bado inaandaliwa na jambo hilo lipo mikononi mwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”


Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema hakupatikana jana kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya rasimu hiyo.MWANANCHI

Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: