BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UKAWA WAANZA MIVUTANO ZANZIBAR, BAADHI YA KUNDI LATAKA KUREJEA KATIKA BUNGE MAALUM LA KATIBA.


WAKATI viongozi wa kile kinachoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wanaonesha kushikamana hadharani, habari za ndani ya Umoja huo zinasema kuwa mivutano imeanza kuzuka huku baadhi ya viongozi wake wakitaka kurejea Bunge Maalum la Katiba.
Habari kutoka ndani ya Umoja huo zinasema kuwa angalau viongozi wawili wa vyama vinavyounda UKAWA wanataka kurejea bungeni na kushiriki mchakato wa kutunga Katiba mpya wakati Bunge hilo litakapoanza tena Agosti mwaka huu.

Habari zinasema kuwa viongozi hao wawili, wanataka kurejea tena bungeni kwa sababu wameanza kubaini kuwa kuna ujanja mwingi ndani ya UKAWA na kuwa baadhi ya vyama vinavidanganya na kuvitumia vingine, bila kuonekana kwa faida yoyote dhahiri.

“Tulisusa Bunge kwa pamoja, lakini sasa inaanza kuonekana kuwa wapo wenzetu ambao wana maslahi binafsi na kuonekana kututumia sisi kwa manufaa yao ya kisiasa na hata kifedha,” anasema mmoja wa viongozi wa UKAWA, ambaye anahisi baadhi ya wenzao wanapata maslahi zaidi kuliko wengine.

Kuna madai kuwa UKAWA wamepatiwa fedha, tena nyingi na mfadhili ama wafadhili wa nje ya Tanzania, lakini fedha hizo zinaishia mifukoni mwa kiongozi mmoja ama wawili wa umoja huo, usiosajiliwa na unaoendesha shughuli zake za kisiasa, bila hati zozote za kuuhalalisha kuendesha shughuli za kisiasa.

Viongozi wa vyama CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na vyama vingine vidogo vidogo walisusa Bunge Maalumu la Katiba mwezi uliopita, wakiazimia kuendesha kampeni ya kutafuta Katiba mpya nje ya Bunge, kupitia mikutano ya hadhara ya wananchi. UKAWA walifanya mkutano wao wa kwanza mjini Zanzibar juzi.

Pamoja na kwamba ni dhahiri kuwa Umoja huo na shughuli zake haziungwi mkono na wananchi wa Tanzania walio wengi, lakini viongozi wake wameendelea kushikilia kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa, wanasema kuwa UKAWA wamechagua kuanzia mikutano yao Zanzibar, kwa sababu huko ndiko wana uhakika wa kupata watu wa kuhudhuria mikutano yao, kwa sababu ya wanachama wa CUF.

“Wamekimbia Zanzibar kwa sababu huko Bara watampata nani wa kwenda kupoteza muda wake kusikiliza hoja zisizokuwa na mashiko,” amesema mchunguzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: