BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KATIBA MPYA YAOMBEWA KATIKA SIKUKUU YA EID HAJI TANZANIA.

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhnEJDDnhoCg80EuyRlIYJyUxA8o9IBNEHzQP17c6b_UBMhS3fFVxyvzpEW4-e33J93D_IAYyzV0HtSRNA9UGYKgjFmf9Ra-yuHqSudNs8RILRnR2cWxGHdVNC-ISZbECObM7AD1hGq7YN9/s1600/unnamed+(3).jpg
WATANZANIA wametakiwa kuomba kwa ajili ya amani ya nchi na kuiombea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, inayotarajiwa kukabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete kesho kutwa ili iweze kufikishwa kwa wananchi na kujadiliwa kwa amani na utulivu na Watanzania wote.

Aidha, wametakiwa kuilinda kwa nguvu zote amani ya nchi iliyopo, badala ya kugeuza siasa na dini kuwa vyanzo vya kuvurugika kwa amani ya Tanzania inayopigiwa mfano na nchi nyingi duniani. Hayo yalisemwa jana kwa nyakati tofauti wakati wa sherehe za Sikukuu ya Idd el Haji iliyofanyika sehemu mbalimbali nchini.

Mjini Dodoma, Shehe wa Mikoa ya Dodoma na Singida wa Jumuiya ya Waislamu ya Ahmadiyya, Bashart ur Rehman Butt alipokuwa akitoa mawaidha ya sikukuu hiyo kwenye Msikiti wa Makole Sabasaba mjini hapa, alisema ni lazima Watanzania wote waendelee kuomba kwa ajili ya Katiba Iliyopendekezwa ili kulinda amani na utulivu nchini.

“Wananchi wanatakiwa kuisoma ili wafahamu mambo yote mazuri yaliyoainishwa ndani ya katiba hiyo, hilo litakuwa jambo la msingi,” alisema.

Pamoja na hayo, aliwakumbusha Waislamu kuikumbuka siku hiyo ya Idd el Haji (Adhiya) kwa kusherehekea pamoja na jamii yenye watu wasiojiweza.

“Msingi wa sikukuu hii inatukumbusha kujitolea na kufurahi na jamii ya wasiojiweza wakiwemo watoto yatima, wazee walemavu na wale wanaoishi katika mazingira magumu… ni vizuri kama wote hao watakumbukwa,” alisema.

Alisema kama yalivyo maagizo ya Mtume Muhammad (S.A.W), ni vizuri kama wenye nacho watawasaidia wale ambao hawana ili watu wote wafurahie sikukuu.

Alisema; “Ni muhimu kujitolea siku kubwa kama hii na kuacha tabia ya kufungia vitu ndani bila kuwashirikisha wengine.”

Shehe huyo alisema si vema Waislamu wakachinja na kisha dhabihu yote ikawekwa kwenye majokofu wakati wengine wanatakiwa kusaidiwa.

“Mtu akifanya hivyo atakuwa amekwenda kinyume na agizo la Mtume,” alisema na kuwataka waumini kuonesha mfano wa kusherehekea na waumini mbalimbali sawa na maagizo ya Kiislamu yaliyoagizwa na Mtume ambayo yanataka viongozi wa dini kuonesha mfano kwa waumini wanaowaongoza.

Katiba yapongezwa Kwa upande wake, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu aliipongeza Serikali kwa kukamilisha mchakato wa Katiba Inayopendekezwa, licha ya awali kazi hiyo kuonekana kuwa ngumu kutokana na changamoto kadhaa zilizokuwa zimejitokeza tangu kuanza kwa mjadala katika Bunge Maalumu la Katiba mwanzoni mwa mwaka huu.

Shehe Rajabu aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akitoa hotuba kwa Waislamu wa Mkoa wa Dodoma kwenye swala ya Idd el Haji, iliyofanyika kwenye Msikiti wa Gaddafi.

Alisema licha ya kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa bado waumimi wa dini ya Kiislamu wana hamu ya kutaka kuona Mahakama ya Kadhi inatambulika kikatiba katika siku za usoni.

Shein akataa vurugu Naye Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wasiwe chanzo cha kuvurugika kwa amani kwa visingizio vya harakati za kidini na kisiasa.

Aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa katika Baraza la Idd el Haji kwenye Ukumbi wa Chuo cha Kiislamu Kiuyu, kilichopo Mkoa wa Kaskazini Pemba, na kuongeza kwamba amani ndio uhai wa nchi na serikali itatumia nguvu zake zote kuilinda.

Dk Shein alisema Tanzania imefikia kuwa nchi ya amani kutokana na misingi ya uongozi bora iliyowekwa na viongozi wa awamu zote zilizopita na kusisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kufurahia baraka zilizopo nchini na kufanya jitihada ili kuilinda neema na heri hiyo iliyopo.

Katika hotuba yake hiyo, Dk Shein alitoa mwito kwa wananchi na kuwataka kutoingiza ubinafsi na kupewa nafasi katika masuala yanayohusu jamii hasa mambo ya siasa na dini na kuwataka kuepuka kushabikia mambo yanayokwenda kinyume na maadili mema.

"Wale wote wanaofanya hivyo, watambue kuwa wanafanya makosa kwa kufikiri kwamba wana uwezo zaidi kuliko wengine wa kuondosha matatizo katika jamii kwa kutumia nguvu zao...ni vyema tukaelimishana juu ya mema na mabaya kwa busara, badala ya kiburi na dharau," alisema Dk Shein.

Kutokana na umuhimu wa amani hapa nchini, Dk Shein alisisitiza kuwa Serikali zote mbili zitasimamia amani na utulivu kwa uwezo wake wote kwa kutambua kwamba hakuna mbadala katika suala la amani.

Pamoja na hayo, aliwataka wananchi kutambua kwamba wana jukumu la kupambana na maovu mbalimbali yakiwemo ujambazi, ubakaji, udhalilishaji wa wanawake na watoto, ajali za barabarani, ulevi, rushwa, dhuluma, uhasama na chuki zisizokuwa na msingi.

Kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini, Dk Shein alieleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada zake kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo mbalimbali katika kuimarisha miundombinu ikiwemo barabara, usambazaji wa maji safi na salama, huduma za umeme na huduma nyinginezo.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: