BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NASEMA ACHENI WANANCHI WAJADILI KATIBA MPYA KWA UHURU WOTE ILI KUSIWE NA USHAWISHI WA VYMA VYA SIASA AMA MAKUNDI YA KIDINI..

 
JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata) limesema Watanzania waachwe huru kwa ajili ya kuijadili Katiba Inayopendekezwa ili muda wa kura ya maoni utakapofika waweze kufanya uamuzi sahihi bila ya kushawishiwa na vyama vya siasa au makundi ya kidini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Jukata Deus Kibamba, alisema vyama vya siasa visiingilie jambo hilo, kwani kuendelea kupiga kampeni kutawafanya Watanzania kupiga kura ya maoni kwa shinikizo la vyama vya siasa na madhehebu ya dini.

"Sisi msimamo wetu tunataka wananchi wenyewe waisome katiba hiyo, waielewe halafu waamue kupitia sanduku la kura," alisema Kibamba.

Kibamba alisema dalili zilivyo sasa ni wazi kuwa wakati wa upigaji wa kura ya maoni utajaa mvutano kutokana na wanasiasa na vyama siasa kugawanyika na kuanza kupiga kampeni ya ndio na hapana dhidi ya Katiba hiyo Inayopendekezwa.

"Nakwambia kutachimbika wakati wa kupiga kura ya maoni, kama wanasiasa wataendelea na lugha zao za kuipigia debe na wengine kuibeza," alisema Kibamba na kuongeza kuwa ndio maana wanampongeza Rais Jakaya Kikwete na vyama vingine vya siasa jambo hilo lipigiwe kura baada ya Uchaguzi Mkuu.

Alisema jambo hilo likifanyika kabla ya uchaguzi au wakati wa uchaguzi mkuu, wanasiasa watachanganya wananchi na akasisitiza kuwa ni vyema Watanzania waachwe waisome Katiba hiyo inayopendekezwa.

Jukata pia kupitia kwa jarida lao la robo mwaka, imedai kuwa kauli zilizotolewa na baadhi ya viongozi mara baada ya Katiba inayopendekezwa kupitishwa zinaweza kuwa na athari kubwa katiba mchakato wa kupata katiba mpya.

Taarifa hiyo ilisema ni wakati sasa wa kuachwa kwanza huru kwa Watanzania wenyewe waijadili Katiba Inayopendekezwa ili waweze kutoa uamuzi sahihi.

“Katiba ni yetu sote hakuna mwenye haki ya kuandika Katiba kuliko wengine hivyo dhana ya maridhiano na muafaka ipewe kipaumbele,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Tangu kupitishwa kwa katiba hiyo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wamenukuliwa wakitoa matamko mbalimbali wengine wakitaka wananchi waikatae katiba hiyo na wengine wakieleza kuwa inawajali wananchi hivyo waikubali.

Jarida hilo la Jukata lilitoa Kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ya kutamani kura ya maoni ifanyike kabla ya uchaguzi mkuu au pamoja na uchaguzi mkuu kuwa inakwenda kinyume na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais Jakaya Kikwete na Kituo cha Demokrasia Tanzania ya kusitisha mchakato huo hadi uchaguzi mkuu upite.

Aidha, ilisema kauli ya kuomba makundi maalumu kama vile wafugaji, wakulima na wanawake kuwakumbuka kwa kuwa masuala yao yamewekwa kwenye Katiba pendekezi ni kauli ambazo tafsiri yake ni kupiga kampeni kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na Serikali Kuu.

Jukata pia imetaja tukio la kutaka kupigwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman na baadhi ya wajumbe wa BMK kutoka Zanzibar baada ya kupiga kura ya hapana kuwa ni jambo la aibu.

Wakati huohuo, Viongozi Wakuu wa Nchi, Viongozi wakuu wastaafu, Mabalozi, viongozi wa madhehebu ya dini na viongozi kutoka nje ya nchi wametajwa kuhudhuria sherehe kubwa ya kihistoria ya kukabidhiwa Rais katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba.

Tukio hilo la kukabidhi rasimu ya Katiba litafanywa na Rais Kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk Rehema Nchimbi alisema tukio hilo litafanyika kesho katika uwanja wa Jamhuri na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kuona mchakato wa katiba umefanyika kwa amani na utulivu mkubwa bila vurugu wala kumwaga damu kama ilivyo kwa nchi nyingine.

“Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kubaki salama kwa kipindi chote cha mchakato wa katiba tofauti na yanayojitokeza nchi nyingine wakati wa mchakato kama huo,” alisema.

Alisema viongozi wakuu wa kitaifa, viongozi wa dini, viongozi wakuu wastaafu wa Tanzania bara na Zanzibar, mabalozi na viongozi wakuu wote watahudhuria katika tukio hilo kubwa la kihistoria.

Dk Nchimbi alisema sherehe hizo zitafanyika kuanzia saa sita mchana, lakini milango ya Uwanja wa Jamhuri itakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi.

“Wananchi wote wanaalikwa kuhudhuria shughuli hiyo na kushuhudia tukio hilo kubwa na la kihistoria ambalo halijawahi kutokea, wananchi wa mkoa wa Dodoma tuna haki na wajibu wa kuonesha furaha yetu kwa bunge hili la kihistoria limefanyika mkoani Dodoma pekee na si mahali pengine,” alisema.

Alisema Bunge lilifanyika kwa amani na utulivu na wananchi kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Jamhuri ni njia mojawapo ya kuonesha furaha na shukrani kwa Mungu.

Pia alisema kutakuwepo na makundi mbalimbali kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar na makundi hayo ni pamoja na wafugaji, wakulima, wavuvi, wanawake, vijana wazee, wachimbaji madini wadogo, walemavu na wasanii, wananchi na wote ambao katiba iliyopendekezwa imewagusa.

“Serikali ya mkoa wa Dodoma inatoa mwito kwa wananchi wote na mikoa ya jirani kuhudhuria kwa wingi ili kushuhudia tukio hilo kubwa,” alisema.

Alisema tukio hilo kubwa na la kihistoria litatanguliwa na tukio muhimu na maalumu la kuomba dua na shukrani kwa kukamilika salama kwa shughuli za Bunge Maalum la Katiba Mkoani hapa. Alisema dua na shukrani itakafanyika leo katika viwanja vya Mwalimu Nyerere kuanzia saa 10 jioni.

Alisema viongozi wa Serikali na taasisi zisizo za kiserikali, viongozi na waumini wa dini mbalimbali watahudhuria.

Aidha, alisema kutakuwa na ulinzi wa kutosha na miundombinu ya usalama ya kitaifa itakuwa Dodoma kuhakikisha sherehe hizo zinafanyika kwa usalama na utulivu mkubwa.

Pia alisema tukio kama hilo linategemewa kufanyika huko Zanzibar.

Alipohojiwa na waandishi wa habari kwa nini makabidhiano hayo yanafanyika Uwanja wa Jamhuri na si Ikulu ya Rais iliyopo Chamwino, Dk Nchimbi alisema hilo limetokana na unyeti wa tukio hilo ambalo limeonesha watu wengi wanahitaji kuhudhuria na kushuhudia rasimu hiyo ikikabidhiwa.

Pia alipohojiwa ni viongozi gani kutoka nje ya nchi watakaohudhuria makabidhiano hayo alisema bado hana taarifa kamili.

“Kama watakuwepo mtawaona siku ya tukio bado sina taarifa kamili juu ya viongozi wan chi za nje au wawakilishi wao,” alisema.

Waislamu waaswa wasiandamane Wakati huo huo,Waislamu nchini wametakiwa kutowasikiliza baadhi ya watu wanaowashawishi kuandamana juu ya suala la Mahakama ya Kadhi kwani jambo hilo linafanyiwa kazi ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewaahidi kuhakikisha mambo yao yanaingizwa kwenye katiba.

Akizungumza wakati sikukuu ya Idd-ul-Adha mkoa wa Pwani iliyofanyika mjini Kibaha, Mbunge wa Jimbo la Mafia Abdulkarim Shah ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Baraza la Idd alisema Waislamu wasikubali kuingia kwenye mtego huo wa maandamano kupinga katiba.

Shah alisema kuwa serikali ni sikivu na kupitia kiongozi wake mkubwa haiwezi kwenda kinyume na makubaliano waliyokubaliana ambapo Waziri Mkuu alisema suala lao linashughulikiwa hivyo ni vema Waislamu wakawa na subira.

“Msikubali kutumika kwani kuna baadhi ya watu wanataka kutumia suala la Kadhi kufanya maandamano jambo ambalo linaweza kuleta uvunjifu wa amani ya nchi na wanapaswa kuheshimu kauli zinazotolewa na viongozi wao za kudumisha amani,” alisema Shah.

Alisema kuwa kupitia viongozi wao wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) waumini wa dini hiyo wanapaswa kupeleka hoja zao na si kwenda kinyume, ikiwa ni pamoja na kuandamana kwani kila jambo lina wakati wake.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: