BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NI HATARI TUPU: MTANDAO WA VIBAKA NA UHALIFU NAMNA WALIVYOJIIMARISHA KATIKA MAENEO MENGI YA JIJI LA DAR ES SALAAM.


Eneo la Tandale la jijini Dar es Salaam.


Dar es Salaam.
Pamoja na kuendelea kuvutia misururu ya watu wanaoingia katika Jiji la Dar es Salaam kila kukicha, maeneo yake mengi yamebainika kuwa si salama.


Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa Mwananchi katika maeneo mbalimbali yanayotajwa kwa uporaji, umethibitisha kuwapo kwa matukio ya wizi na uporaji kwa kutumia mbinu mpya zinazobuniwa na vibaka kila kukicha.


Maeneo hatarishi ambayo yamebainika katika uchunguzi huo ni pamoja na Buguruni, Kinondoni, Tandale, Msasani, Mwananyamala, Ubungo, Temeke na hata maeneo ya ‘uzunguni’.


Katika maeneo yaliyofanyiwa uchunguzi, zimebainika aina na mbinu tofauti za wizi, ukiwamo wa simu na maeneo zinapouzwa.


Mbinu hizo ni vibaka kujifanya wanafanya mazoezi ya kukimbia na kuwakwapua mikoba na kompyuta wapitanjia. Pia wapo wanaofanya hivyo kwa kutumia pikipiki na magari. Wapo pia wanaojifanya wanaongoza magari na wengine kujifanya wanajitolea kukarabati barabara.


Eneo la Mkwajuni limekuwa na matukio mbalimbali ya kihalifu ikiwamo ukabaji na uporaji wa vitu na mali za watembea kwa miguu.


Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kawawa, Elizabeth Massawe anasema: “Mwaka jana hali ilikuwa mbaya zaidi na watu walikuwa wanakabwa sana. Lakini kuanzia Januari mpaka Machi kuna watu watatu tu ndiyo waliokutwa wamekufa katika Bonde la Mkwajuni, kuna vijana wawili wa kiume na mwanamke mmoja aliyeuawa na kutupwa chini ya Daraja la Mto Ng’ombe hapo bondeni.”


Massawe anataja sababu ya kukithiri kwa matukio hayo kuwa ni pamoja na eneo hilo lenye vichaka na uwazi mkubwa, kuwa mbali na makazi ya watu… “Kwa hivyo inakuwa rahisi vibaka kufanya uhalifu, lakini tayari nimeshaunda kikosi cha ulinzi shirikishi ambacho kinaendelea na kazi ya kuimarisha ulinzi.”


Mjumbe wa Mtaa wa Mkunguni B, Rajabu Omary anasema mpaka sasa hakuna usalama wa watu kutembea kwa miguu katika eneo la bonde hilo kutoka Magomeni au Kinondoni Studio.


“Kuanzia saa 12.00 jioni hutakiwi kutembea kwa miguu kama unahitaji kuwa salama, vinginevyo utakuwa unatengeneza ushawishi wa kufanyiwa uhalifu. Ulinzi wa polisi hauwezi kufika mpaka huku, lakini sisi na jamii kwa pamoja tunatakiwa kuwa walinzi kwa kila mmoja wetu.”


Maeneo hayo ambayo siyo salama, yanajumuisha eneo la Kinondoni Studio na kwa Manyanya.


Licha ya kukithiri kwa wizi, maeneo hayo yanatumika pia kama kichaka cha wahalifu hao. Vibaka wengi baada ya kuiba hukimbilia barabara za Morogoro na Kawawa kwenye mabonde ya Jangwani na Mkwajuni kujificha.


Katika Bonde la Mkwajuni kuelekea Jangwani, huko kunatajwa kuwa ni hatarishi zaidi kwani asilimia kubwa ya vibaka wa maeneo mbalimbali ya jijini wameweka makazi yao eneo hilo na huishi katika vibanda vilivyojengwa kwa miti na mifuko ya sandarusi.


Mkazi wa Mkwajuni, Mwanaisha Simbakalia anasema hali si salama kwani hata wale wanaopora kwa kutumia pikipiki nao hukimbilia huko na baadhi ya pikipiki zinazotumika kufanyia uhalifu hufichwa katika maeneo hayo.


“Ukitaka kuthibitisha hilo, pita maeneo ya hapo bondeni Mkwajuni kuanzia saa moja jioni, utaona pikipiki nyingi zinatokea huko bondeni zinakuja kupaki maeneo ya pale Morocco Magomeni,” anasema Mwanaisha.


Mkazi mwingine, Anatory Mkude anasema vitu vingi vinavyoporwa kwenye maeneo ya Magomeni, Kariakoo, Mkwajuni, vinafichwa katika maeneo hayo na baadhi ya wafanyabiashara wanakwenda kununua na kwenda kuviuza mikoa ya jirani na hususan pikipiki.


“Vitu vyote vinavyoibwa kwenye barabara hii ya Morogoro na Kawawa vinauzwa huku, waporaji wote wanapatikana huku haya maeneo si salama hata kidogo,” anasema.


Dawa za kulevya
Wakazi wa Kinondoni pia walieleza kuwa dawa za kulevya zinauzwa bila kificho maeneo hayo: “Hebu angalia juu ya nyaya hizo za umeme, si unaona vile viatu vinavyoning’inia, hiyo ni alama yao inayotambulisha kuwa eneo hilo ukihitaji dawa za kulevya unazipata.


“Ukiona kuna viatu vingi kwenye waya mmoja viking’inia ujue hapo kuna dawa za kulevya za aina zote, kuanzia unga, mirungi na bangi,” anasema Mkude na kuongeza kuwa biashara hizo ni miongoni mwa sababu kubwa zinazowafanya baadhi ya wakazi katika maeneo hayo kugoma kuhama licha ya Serikali kuwataka wafanye hivyo ili kuepuka maafa.


Mkazi wa eneo la Jangwani, Sunguti Mrindoke anasema alihamia hapo mwaka 2009, akitokea Kigoma na kusema kuwa maeneo hayo yamejaa vitendo vya uhalifu.


Mbinu mpya Msasani, Masaki
Wakazi wa Msasani, Masaki na Oysterbay ambako awali hakukuwa na wizi wa kutishia, katika siku za hivi karibuni wamelalamika kuibuka kwa aina ya uhalifu.


Makundi ya vijana wanaofanya mazoezi ya kukimbia hukwapua mali za watembea kwa miguu katika barabara kubwa na ndogo.


Mara nyingi wezi hao huiba asubuhi wakiwategea wale wanaoamka mapema kuwahi kazini au katika shughuli zao za kawaida.


“Utawaona vijana wako katika makundi wanakimbia, ghafla wanakukaribia wanakuibia na kuendelea kukimbia, hata ukipiga kelele si rahisi watu kujua kinachoendelea,” anasema mkazi wa Masaki, Ubalozini, Salome Semdoe.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura anasema, amewahi kupata malalamiko hayo ya vijana wanaojifanya kwamba wanafanya mazoezi asubuhi kufanya uhalifu.


“Unajua wimbi la wizi kama huu lipo na nimeshapata malalamiko kutoka kwa wakazi wa hayo maeneo, tunalifanyia kazi. Mambo kama haya yapo hata katika nchi zilizoendelea, hadi leo hii Marekani nao wanalalamika vibaka wa aina hii na kuna ukabaji kama ilivyo hapa,” anasema.


Wambura anasema wizi wa aina hiyo na kuibuka kwa wimbi la makundi ya uhalifu kama Panya Road, unaendelea kukua baada ya kukua kwa sayansi na teknolojia ambako vijana wanajifunza uhalifu kupitia mitandao ya kijamii.


Mkazi wa Msasani, CCBRT, Prisca Mlaponi alitoa ushuhuda akisema amewahi kuibiwa mkoba wake wenye fedha na hereni na vijana waliokuwa wamevaa nguo za mazoezi huku wakikimbia.


Kadhalika, wakazi wa maeneo ya Kariakoo, Jangwani wamelalamikia wizi wa aina yake ambao makundi ya vijana ambao hujifanya wanatengeneza barabara huwasubiri waendesha bodaboda na wenye magari na kuwaibia.


Akielezea tukio lililomkuta, dereva wa Bodaboda, Seif Mashishanga anasema aliporwa na vijana hao alipokuwa akitaka kuvuka Uwanja wa Kajima akielekea Kariakoo.


“Tuliwakuta vijana sita wakiwa wanajenga barabara, walipotuona wakatusimamisha na kutudai fedha za ujenzi wa barabara, tuliposimama tu wakatuvamia na kutusachi mifukoni, walichukua simu na kila kitu, pamoja na bodaboda.”


Mwananyamala


Katika eneo la Mwananyamala, vibaka wanatumia mbinu ya kupanda daladala kama abiria wa kawaida na wakiwa humo huwasoma abiria wenye vitu vya thamani.


Wakati wakushuka vibaka hao hukwapua pochi au simu na kushuka huku wakikimbia.


Maeneo yanayosifika kwa wizi huo ni Mwanayamala A au njia panda ya kwenda Hospitali ya Mwananyamala na Ujiji.


Mkazi wa Mwananyama Ujiji, Sharifa Abdallah anasema wezi hao ni wenyeji na wanajulikana maeneo hayo hivyo hata inapotokea amekwapua na aliyeibiwa kupiga yowe hawezi kupata msaada.


“Kibaka anaweza kupanda daladala katika kituo cha A, akifika Ujiji au kwa Manjunju anaomba kushuka lakini tayari ameshamsoma mtu atakayemkwapua, japo konda anakuwa mlangoni anakopitia huyo mwizi lakini hamfanyi chochote kwa kuogopa ‘kufanyiziwa’ au na yeye ana mgawo wake katika wizi huo,” anasema.


Wageni Ubungo
Eneo la Ubungo darajani jirani kabisa na kituo cha mabasi yaendayo mikoani, vibaka wanaongezeka kila kukicha na wanabuni mbinu mbalimbali za wizi.


Abiria wanaokwenda mikoani wamekuwa wakiporwa vitu vyao na matapeli hao ambao wamekuwa wakiwarubuni kwa kuwauzia sabuni au mbao badala ya simu.


Mwandishi wetu ameshuhudia simu hizo zikiuzwa kwa abiria hao kuanzia Sh15,000 mpaka 30,000 na baada ya kuuza wauzaji hao hutokomea.


Eneo la Ubungo Darajani nako kuna wale wanaochezesha kamari kwa kutumia karata tatu. Hili ni kundi la vijana ambao wanakuwa wengi wengine wakisubiri wapita njia na kuwapora simu na mikoba yao kisha vibaka ho wanakimbilia chini ya daraja.


Buguruni
Ukifika eneo hili kama uko kwenye foleni ukiwa ndani ya daladala, gari binafsi au unatembea kwa miguu lazima uwe makini hasa kwa vitu kama simu za mkononi, pochi na begi la mgongoni.


Kwa mfanokama ‘unachati’ na simu halafu madirisha ya gari yako wazi, si ajabu simu yako ikakwapuliwa. Inaelezwa kuwa vibaka wa Buguruni si rahisi kuwakamata kwa sababu wanavifahamu vichochoro vyote vya maeneo hayo.


Kadhalika, vibaka wengine hufanya uhalifu huo kwa makundi. Wanajifanya wanapigana au wamemkamata mwizi sasa ukithubutu kuingilia wanakugeuza wewe mwizi halafu wanakuibia kila ulichonacho na kuondoka.


Lakini wizi wa hatari zaidi Buguruni ulioibuka hivi karibuni ni ule wa kujifanya wanakuja karibu na gari lako wakati unaegesha.


Wezi hao hujisogeza karibu na kuanza kukuelekeza sehemu ya kuegesha au jinsi ya kugeuza. Wakati unafungua mlango ili utoke, mwizi hushikilia sehemu ya mlango bila wewe kujua. Ukigeuza mgongo tu chochote atakachokikuta ndani ya gari, ni halali yake.


Chang’ombe, Keko,
Katika eneo hili, vibaka wamekuwa tishio katika maeneo ya Barabara ya Changombe na Darajani eneo la Keko licha ya kuwapo kwa doria ya mara kwa mara ya polisi wakishirikiana na ulinzi shirikishi.


Baadhi ya vibaka hao wanadaiwa kutumia mbinu ya kujichanganya na wafanyabishara ndogondogo ambao huuza bidhaa zao kandokando ya barabara.


“Mara kadhaa tumeshuhudia watu wakiporwa hasa wakiwa ndani ya magari, wengine wanajifanya waosha magari lakini kumbe ndiyo wanachunguza kitu wanachoweza kuiba haraka, kisha utashtukia gari likigongwa kwa nguvu lazima utashtuka na kushusha kioo ili kuangalia kinachoendelea hapo ndipo unalizwa,” anasema Athumani Mussa.


Anasema wezi hao wamekuwa wakipora zaidi simu na mikoba midogo ya kina mama. Akizungumzia hali hiyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Keko Mwanga A, Rama Diga anasema vitendo vya uporaji katika eneo hilo vimeendelea kushamiri ingawa polisi jamii wamekuwa wakifanya jitihada za kuthibiti.


“Kweli wanasumbua hasa kuanzia saa 12 jioni lakini nakumbuka mwaka jana nikiwa bado mwenyekiti, tuliwahi kufanikiwa kuwakamata vibaka kadhaa lakini wale walioporwa baada ya kurejeshewa simu zao, hawakuwa tayari kwenda kuwashtaki, hali hiyo inawakatisha tamaa vijana wanaojitahidi kulinda usalama,” anasema Diga.


Anasema anaamini kuwa kama watu wanaoporwa wangekuwa wanakubali kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha kesi zao zinafikishwa polisi kisha mahakamani, ingesaidia kwa sababu sheria ingechukua mkondo wake kwa vibaka hao kufungwa jela.


“Hata hivyo, vibaka hao wapo kimtandao, wengine wanatoka Tandika wengine maeneo ya hapa jirani wakishapora wana watu wao maalumu ambao huwapelekea mali hizo za wizi, hasa katika Mtaa wa Agrey, Kariakoo hawakurupuki kuuza ovyo,” anasema Diga.


Mahakama ya simu, Tandale kwa Mtogole
Eneo maarufu jijini Dar es Salaam ambalo linasifika kwa matukio ya uhalifu ya kudumu ni Tandale kwa Mtogole maarufu kama ‘mahakama ya simu’ kutokana na kukithiri kwa wizi wa simu za mkononi.


Jambo la ajabu ni kuwa ukiibiwa simu yako unaweza kuipata ileile lakini kwa bei watakayokupangia.


Watu mbalimbali waliozungumzia suala hilo wakiwamo wapigadebe na waendesha bodaboda wanasema wezi wengi wa simu ni ‘mateja’ ambao wanaweza kuiba simu yenye thamani ya Sh500,000, kuiuza kwa kati ya Sh50,000 hadi 100,000.


Mchuuzi wa vocha katika eneo hilo, Raymond Richard anasema hazipiti saa mbili kabla ya watu kuibiwa hapo.


“Siyo simu tu, hawa kina mama huibiwa sana pochi zao wakiwa katika magari. Wanaiba mchana kweupe kabisa, wapo wanaokamatwa na kupigwa na wengine hufanikiwa kukimbia,” anasema Richard na kuongeza: “Mfano wiki mbili zilizopita kuna jamaa alipigwa hadi kufa baada ya kuiba huko Kwa Tumbo na kukimbilia hapa (Kwa Mtogole).”


Inaelezwa kuwa wezi hao huthubutu kuwaibia wanawake wigi wakiwa kwenye magari… “Utashangaa weaving linachomolewa na kibaka anakimbia nalo,” anasema mkazi wa eneo hilo, Chilo Yusufu.


Mama lishe katika eneo hilo, Zainab Omary anasema wezi hao wamebuni njia mpya, hupanda katika mabasi na kuwaelekeza wenzao walioko kituoni, abiria wenye simu nzuri na pochi.


“Siku hizi ndiyo mtindo wao, mmoja anaweza kupanda basi mbali tu na kuwafuatilia abiria, baadaye huwajulisha wenzake na basi likifika tu kwa Mtogole mtu huibiwa,” anasema huku akisisiza kuwa wanawajua wezi wote wa eneo hilo kwa majina na wanapoishi.


Katika muda ambao mwandishi wetu alikuwa katika eneo hilo, alishuhudia vibaka hao wakirandaranda pembeni ya kila daladala lililokuwa likisimama kituoni, huku abiria wanaoelewa sifa za mahali hapo wakifunga vioo kukwepa kukwapuliwa simu na vitu mbalimbali.


Barabara ya Kilwa, Temeke, Mtoni Mtongani
Eneo la Mtoni Mtongani karibu na Mto Mzinga nako kuna kundi la vijana wanaofanya uporaji wa simu na vitu vingine vya thamani kutoka kwenye magari yanayokuwa kwenye foleni.


Eneo hilo lililopo katika Barabara ya Kilwa, wilayani Temeke, ni miongoni mwa maeneo yanayokuwa na foleni kubwa jijini Dar es Salaam na vibaka ambao wengi wao wanatajwa kuwa wanatokea Temeke, Tandika na Mbagala, hupita kwenye magari na kukwapua simu.


Wakazi wa eneo hilo, wanasema kundi la vijana hao limeongezeka katika siku za hivi karibuni kiasi kwamba sasa wameanza kuiba vitu hata mchana tofauti na zamani.


Mwenyekiti wa Mtaa wa Mtongani, Khamisi Mtongo anasema eneo hilo limekuwa hatari kwa muda mrefu, lakini hakuna jitihada za kutosha zilizofanyika ‘kulisafisha’.


“Zamani ilikuwa ikifika saa 12 jioni, hakuna mtu aliyekuwa anapita kwa miguu. Pale ilikuwa lazima uporwe. Hali hiyo bado inaendelea japokuwa imepungua kidogo,” anasema Mtongo.


Akizungumzia namna vijana hao wanavyotekeleza uhalifu, Mtongo anasema baadhi yao mchana huosha magari kando ya Mto Mzinga, lakini inapofika jioni husogea barabarani na kuanza kupora vitu.


Mkazi wa Mtoni Kijichi, Meshack Lauwo anasema mbali na vibaka kupora simu, wamekuwa waking’oa vitu kwenye magari yaliyoharibika.


“Ole wako gari likuharibikie pale usiku. Watakuja kujifanya wanataka kukusaidia, ukizubaa wanaanza kufungua taa uko hapo hapo,” anasema Lauwo ambaye ni fundi cherehani.


Kaimu Kamanda Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Zakaria Sebastian anasema ataongeza nguvu katika eneo hilo, ingawa kila siku polisi hutakiwa kufika hapo kuanzia saa moja hadi saa tatu foleni inapokuwa imepungua.


Kamanda huyo anasema, baadhi ya vibaka wanatumia pikipiki kufanya uporaji hasa wa mikoba ya wanawake.


“Nitawasiliana na wahusika waongeze nguvu katika eneo hilo,” anasema Sebastian.


Pia uchunguzi umebaini kuwa katika maeneo ya Temeke Mwisho na Tandika, kuna vijana wanaochomoa fedha na simu mifukoni.


Katika eneo la Tandika, kundi la vijana ambao hupenda kugawanyika katika makundi ya watu watatu, huwavizia wapita njia na abiria katika kituo cha daladala ili kuwaibia.


Mfanyabiashara ya urembo, Celina Mtavangu anasema kuwa mmoja wa vijana hao akishachomoa simu au fedha kutoka kwa mteja, humpatia mwenzake haraka na kuondoka eneo la tukio.


Uzunguni nako hatari
Mbali na maeneo ya ‘uswazi’ ambayo husifika kwa uporaji, eneo la katikati ya jiji hasa la Barabara ya Barack Obama, Ocean Road si salama. Vibaka wengi huweka kambi kuanzia eneo la makutano ya barabara ya hiyo na ile ya Chimala.


“Kila siku watu wanalia wameporwa simu upande huu kuanzia Hospitali ya Ocean Road hadi Aga Khan. Madereva wa pikipiki huvizia watu waliomo ndani ya magari wanaotumia simu zao, huwagongea na wakishusha tu kioo huwapora simu na kutokomea.


“Vibaka hao wengi huonekana kuanzia saa 11 jioni na Wazungu wanaibiwa sana mitaa hiyo,” anasema mchuuzi wa bidhaa katika eneo hilo, Said Seleman.


Wakati Seleman akibainisha hayo, Fatma Ramadhan anasema alishaibiwa vitu vya thamani vya takriban Sh1 milioni baada ya vibaka kumtishia kwa panga rafiki yake aliyekuwa amemwacha kwenye gari pembezoni mwa barabara hiyo.


Anasema baada ya kuibiwa vifaa hivyo vikiwamo vidani na nguo, aliwatafuta baadhi ya vibaka anaofahamiana nao ambao waliingia katika ‘Msitu wa Gymkana’ kuwatafuta waliohisiwa kuiba pasi na mafanikio,


“Nashukuru kwamba waliziacha simu zilizokuwa kwenye eneo la gia. Ningekuwapo mimi najua wasingenifanyia vile ila yule dada aliogopa panga ndiyo maana aliwaachia. Tuliripoti kituoni tukio hilo lakini hadi sasa vitu havijapatikana,” anasema Fatma.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: