TFF YAITOA NISHAI SIMBA SC, YAIPIGA FAINI YA DOLA 150.
Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF) limetoa adhabu kwa vilabu, kocha na mchezaji kwa utovu wa nidhamu katika ligi kuu Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa afisa habari wa TFF, Baraka Kiziguto, kocha Jackson Mayanja wa Kagera Sugar amepigwa faini ya sh. 500,000(wastani wa dola 270) na kufungiwa mechi tatu kwa kutoa lugha ya kashfa kwa maneno na vitendo kwa waamuzi wa mechi yao na Mtibwa Sugar kuwa walipewa rushwa.
Adhabu dhidi ya Kocha Mayanja kwenye mechi hiyo namba 136 iliyochezwa Aprili 1, 2015 kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 40(1) ya Ligi Kuu.
Klabu ya Mtibwa Sugar imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya timu yake kukataa kuingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi namba 142 dhidi ya Stand United iliyochezwa Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Nayo Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (wastani wa dola 150) kwa mujibu wa kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu baada ya timu yao kugoma kuingia kwenye vyumba vya kuvalia nguo (changing room) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar. Hatua hiyo ilisababisha wachezaji wakaguliwe kwenye gari lao.
Pia Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kuzingatia kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu baada ya vilevile kugoma kuingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo hiyo namba 146 iliyochezwa Aprili 6, 2015.
Kipa Tony Kavishe wa Polisi Morogoro amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kosa la kumpiga ngumi mwamuzi msaidizi namba mbili, Hassan Zani kwa kuzingatia kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Alifanya kosa hilo kwenye mechi namba 147 dhidi ya Mgambo Shooting iliyochezwa Aprili 5, 2015 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
0 comments:
Post a Comment