WAANGALIZI WA UCHAGUZI MKUU OKTOBA 25 WASHIKWA NA BUTWAA NA KUWASHANGAA WATANZANIA.
Kiongozi wa timu ya waangalizi wa Jumuiya ya EAC katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Moody Awori akizungumza na wajumbe wa Jumuiya hiyo mjini Dar es Salaam.
WAANGALIZI kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wameelezea kushangazwa na amani na utulivu uliokuwepo wakati wa kupiga kura.
Kiongozi wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi Mkuu kutoka EAC, Moody Awori, ambaye pia ni Makamu wa Rais mstaafu wa Kenya amemueleza hayo Rais Jakaya Kikwete alipofika Ikulu jana mchana.
“Sisi kutoka Kenya tulishangaa, unakwenda kwenye kituo watu wako kimya, tunakupongeza pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM),” alisema Awori. Aliongeza kuwa, “Tunatarajia kuwa uongozi mpya unaoingia madarakani, utafuata nyayo zako.”
Awori alimueleza Rais kuwa katika shughuli zao za uangalizi, walitembelea vituo zaidi ya 12 kwa siku jijini Dar es Salaam na kote hali ilikuwa shwari. Alieleza kuwa wamejifunza kitu kikubwa katika uchaguzi huo.
Watanzania kwa jadi yao ni watu wa amani na utulivu, lakini pia kabla ya uchaguzi, Rais Kikwete aliweka wazi kuwa Serikali yake ina wajibu wa kulinda watu na mali zao na kuhakikisha watu wote wanashiriki katika kupata haki yao ya kupiga kura kwa amani, uhuru na utulivu bila kubughudhiwa na hilo ndiyo jambo kubwa na la msingi kwa Serikali yake.
Awali jana asubuhi, Rais Kikwete alihudhuria hafla ya kukabidhiwa vyeti kwa washindi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Rais mteule Dk John Magufuli na Makamu wa Rais mteule, Mama Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali na viongozi wa waangalizi wa uchaguzi hapa nchini, viongozi wa dini na watu mbalimbali.
Baadaye Rais Kikwete aliongoza mapokezi ya Rais mteule katika Ofisi ndogo za CCM Lumumba, ambako wanachama, mashabiki na wapenzi wa CCM walifika kumpokea na kumsalimia mgombea wao, ambaye ameibuka mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment