BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BIBI HARUSI MWENYE SHAHADA YA PILI YA UALIMU, ATOROKA SAA CHACHE KWA KUTUMIA PIKIPIKI AKIWA SALUNI ANAPAMBWA KABLA YA KUFUNGWA KWA NDOA MKONI MOSHI TANZANIA.

Moshi. Bibi harusi amezua gumzo mjini hapa baada ya kutoweka saa tatu kabla ya kufunga ndoa ambayo sherehe yake iligharimu Sh7 milioni.

Bibi harusi huyo, Doroth Msuya alitoroka Jumamosi saa 6:30 mchana wakati akitokea saluni eneo la Lole, Mwika wilayani Moshi Vijijini. Habari zinasema Doroth alitoka saluni hapo akiwa anakimbia akimuacha mpambe wake akiendelea kupambwa.

Doroth, ambaye ana shahada ya pili ya ualimu, alikuwa akitarajiwa kufunga ndoa na Joseph Machange, ambaye ana shahada ya kwanza na anasubiri kuendelea na shahada ya pili ya ualimu.

Ndoa hiyo ilikuwa ifungwe saa 9:00 alasiri kwenye Usharika wa Lole wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini na baadaye sherehe katika Ukumbi wa Mamba Complex.

“Ni tukio ambalo kwa kweli halina majibu, ila sisi kama kanisa tulitangaza kama kawaida Jumapili tatu mfululizo na ukumbuke na send off (sherehe ya kumuaga bibi harusi) ilishafanyika,” alisema Rodrick Mlay, mchungaji kiongozi aliyekuwa afungishe ndoa hiyo.

Mchungaji Mlay alisema upande wa kanisa ulikamilisha mchakato wa ndoa hiyo kwa kufuata taratibu zote za kanisa.

Mchungaji huyo alikataa kuzungumzia kwa undani kuhusu sakata hilo akitaka watafutwe wana familia wenyewe.

Mchungaji aeleza kilichotokea
Mchungaji wa usharika huo, Elikesen Shao alisema walikuwa kanisani wakisubiri wanaharusi, lakini ghafla ilikuja taarifa kuwa bibi harusi ametoweka jambo lililofanya wazazi wa pande mbili kukutana na kujadiliana kwa faragha.

“Walifanya mazungumzo na wazazi wa pande mbili, mchungaji kiongozi akanipa jukumu mimi la kufanya maombi na kuwapa neno la faraja wanafamilia,”alisema mchungaji huyo.

Alisema baada ya mambo kuharibika, Mchungaji Mlay aliwatangazia ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa nje ya kanisa kuwa kumetokea hitilafu na bibi harusi hakutokea kanisani.

MC aeleza kilichojiri
Mtu aliyepangwa kusherehesha harusi hiyo, MC William Ngalo alisema alikwenda kufunga vifaa vya muziki ukumbini, lakini hadi saa 3:00 usiku maharusi hawakutokea.

“Mimi kama MC (mshereheshaji) nilivyopewa kazi nilileta vifaa asubuhi nikavifunga ukumbini. Nikiwa ukumbini, nikapigiwa simu kuwa kuna taarifa mbaya, bibi harusi katoroka saluni,” alisema.

“Nilivyofuatilia nikaambiwa bibi harusi alienda saluni asubuhi na akiwa huko alienda kujisaidia ndipo alipochomokea hukohuko akachukua bodaboda na akaishia moja kwa moja.”

Alisema watu walianza kumtafuta bibi harusi huyo Mwika nzima lakini yeye aliendelea na utaratibu wake ukumbini hadi saa 3:00 usiku huku akiwaomba radhi waalikwa kwa shughuli kuchelewa kuanza.

Mashuhuda wasilimulia
Kwa mujibu wa mmoja wa waumini wa usharika huo, ilipofika saa ya kuingia kanisani mchungaji ilibidi atangaze kuahirisha ibada, huku familia ikiomba wananchi waliokuwapo kushiriki kula chakula. 


“Hicho chakula kilikuwa kimeandaliwa hapo Lole nyumbani kwa bwana harusi. Ilibidi waombwe majirani na wanafamilia wakile maana tayari mambo yalikuwa yameharibika,” alisema.

Baba atinga polisi
Wakati hayo yakiendelea, juzi asubuhi ndugu wa bwana harusi wakiwa pamoja na baba mzazi, Eliringia Machange, walikwenda kituo cha polisi cha Himo kufungua shauri la tukio hilo lakini inadaiwa kulitokea utata wa aina gani ya kesi ifunguliwe.

Machange alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini akataka mwandishi wetu akachukue taarifa hizo polisi au aulizwe bwana harusi mwenyewe.


“Kimsingi mpaka sasa hivi hajapatikana, lakini nisingependa kulizungumzia mimi hilo tukio. Ni vyema ukampata bwana harusi mwenyewe kwa kuwa ndiye anaweza kulielezea vizuri zaidi,” alisema Machange. 

Tukio hilo limekuwa gumzo katika maeneo mbalimbali ya Marangu, Mwika, Himo na Moshi Mjini, huku kila mmoja akijiuliza nini hasa kilimpata bibi harusi huyo msomi.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: