BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MKURUGENZI WA HABARI IKULU AFUNGASHA VIRANGA.


Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu anayemaliza muda wake, Salvatory Rweyemamu akizungumza wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwandishi wa habari Msaidizi wa Ikulu, Premy Kibanga. Picha na Ikulu


Dar es Salaam.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu amemaliza mkataba wake na kuondoka huku akiwashukuru watendaji kwa muda wote aliokuwa nao wakimsaidia Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete.

Kuondoka kwake kunampa fursa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli kuunda safu mpya ya Kurugenzi ya Mawasiliano. Salva aliteuliwa, kwa mara ya kwanza, na Rais Kikwete kushika wadhifa huo Septemba 17, 2007 na alimaliza mkataba wake Septemba 11, 2015 lakini aliongezewa hadi Novemba 10.

Baada ya Dk Magufuli kuapishwa Novemba 5, Rais Kikwete aliondoka siku iliyofuata kurudi nyumbani kwao Msoga, Chalinze, na kwa kuwa Salva amemaliza pia muda wa nyongeza ameondoka na kurudia majukumu yake ya awali.

Kabla ya kuteuliwa kusimamia Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu Salva alikuwa mmoja wa wamiliki na Mhariri Mtendaji wa kampuni ya Habari Corporation (sasa New Habari Corporation). Mwaka huo, aliteuliwa kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Peter Kallaghe aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita Salva aliweka wazi kuwa ataondoka katika ofisi hiyo Jumatatu ya wiki hii (jana) na kumkaimisha msaidizi wake, Mwandishi wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga kuendelea na majukumu yatakayojitokeza.

“Nimetumika Ikulu kwa zaidi ya miaka minane na kwa kipindi hicho chote nimesaini mikataba kadhaa ya kuendelea na kazi. Wakati umefika wa mimi kuondoka. 


Nawashukuru viongozi wa Ikulu pamoja na Rais Kikwete aliyeniamini kuwa msaidizi wake. Nampongeza Dk Magufuli pia kwa kuchaguliwa kwake kuendelea kuwatumikia Watanzania,” alisema Salva ambaye pia aliwahi kuwa mkurugenzi wa kampuni ya mawasiliano ya umma ya S & G.

“Mkataba wangu wa mwisho wa kazi uliisha Septemba 11, 2015 kabla sijaongezewa mwingine unaokamilika Novemba 10 na siku hiyo nitaikabidhi ofisi kwa Premi Kibanga. Nimemaliza kuweka mambo yote sawa tangu Jumapili. 


Ninaondoka nikiwa mwenye furaha, nilishirikiana vyema na Makatibu Wakuu; Philemon Luhanjo na Balozi Ombeni Sefue,” alisema. Aidha, amewashukuru waandishi wa habari kwa ushirikiano waliompa kwa kipindi chote alichohudumu kwenye kurugenzi hiyo mpaka wakati huu anapoondoka.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: