MTOTO WA CELINA KOMBANI AWANIA UBUNGE, AAHIDI KUENDELEZA MAZURI ENDAPO ATASHINDA UBUNGE JIMBO LA ULANGA MASHARIKI MORO.
Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani
Na Juma Mtanda, Morogoro.
Mgombea ubunge kwa tiketi ya chama cha Mapinduzi (CCM), Goodluck Mlinga ameahidi kuendeleza mazuri yote yaliyokuwa yakifanywa na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani endapo ataibuka mshindi katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Ulanga Mashariki utaofanyika Novemba 22 mwaka huu mkoani Morogoro.
Moja ya kuendeleza mazuri ya Celina Kombani ni kuhakikisha kinajengwa chuo kipya kitakachokuwa na uwezo wa kutoa cheti na stashahada ili wanafunzi wote waliohitimu elimu ya kidato cha nne wanapata elimu ya juu katika chuo hicho.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu mkoani hapa, Mlinga ambaye ni mtoto wa kwanza wa marehemu, Celina Kombani alisema kuwa hana mashaka na kuwatumikia wananchi wa jimbo la Ulanga Mashariki kutokana na kujifunza mambo mengi ya upendo yaliyokuwa yakifanywa na mzazi wake katika jimbo hilo hasa ya kimaendeleo.
Mlinga alisema kuwa moja ya mambo anayokusudia kuyaendeleza katika jimbo hilo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwa kujenga mabaraja mapya, kuhamasisha wananchi katika sekta ya elimu na wanajitoa nguvukazi katika ujenzi wa nyumba mpya za walimu, usimamiaji wa ujenzi wa madarasa mapya na sambamba na upatikanaji wa madawati.
“Nimeanza kampeni kwa kufanya mikutano katika kata mbili nne na leo nitafanya kampeni katika kata mbili na kampeni zetu tuzindua rasmi Novemba 7.”alisema Mlinga.
Kwa upande wa mgombea ubunge jimbo hilo kupitia ATC-Wazalendo, Issaya Maputa alieleza kuwa ACT endapo itashinda kiti hicho wananchi wa jimbo la Ulanga Mashariki watanufaika katika nyanja za huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, miundombinu ya barabara na uchumi.
Maputa alisema kuwa lengo la ACT kuingia katika kinyang’anyoro hicho kuona wanahakikisha inasimamia uanzishwaji wa benki ya wananchi wa jimbo la Ulanga Mashariki ili kuweza kukopesha mitaji yenye liba nafuu kwa wananchama na kujikwamua kiuchumi.
“Moja ya mambo yaliyonisukuma kuingia katika uchaguzi huu ni kusimamia upatikanaji wa huduma muhimu kwa kuanzia na huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, upatikanaji wa majisafi na salama, miundombinu ya barabara na uanzishwaji wa benki ya wananchi Ulanga.”alisema Maputa.
Maputa alisema kuwa kwa upande wa uchumi atakikisha kilimo, ujasiliamali vinapatiwa kipaumbele endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwaongoza kama mbunge wao.
Msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Ulanga, Isabela Chilumba alieleza kuwa wilaya hiyo ina majimbo ya uchaguzi mawili likiwemo la Malinyi na Ulanga Mashariki.
Chilumba alisema kuwa jimbo la Malinyi lilifanya uchaguzi wake na Dk Haji Mponda wa CCM kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 lakini kwa jimbo la Ulanga Mashariki uchaguzi wake ulishindwa kufanyika kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Komba kufariki dunia.
“Kuna vyama vya siasa vitatu ambavyo vimesimamisha wagombea katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Ulanga Mashariki.”alisema Chilumba.
Chilumba alivitaja vyama hivyo na wagombea wake kuwa ni Goodluck Mlinga kutoka chama cha Mapinduzi (CCM), Panklas Ligongoli wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Issaya Maputa wa ACT-Wazalendo.
Kipenga cha uzinduzi wa kampeni kwa jimbo la Ulanga Mashariki lilifunguliwa Oktoba 13 huku Oktoba 25 na 26 kampeni zake kwa vyama vyote vilisitishwa kupisha upigaji kura katika uchaguzi mkuu na kutangazwa kwa matokeo yake.alisema Chilumba.CHANZO/MTANDA BLOG
0 comments:
Post a Comment