BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAZIRI MKUU WA RAIS DK JOHN MAGUFULI AANGUA KILIO.


Waziri Mkuu mteule, Majaliwa Kassim Majaliwa akiwashukuru wabunge kwa kumuidhinisha kushika wadhifa huo, bungeni mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 


Dodoma. Mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa amekuwa Waziri Mkuu wa Kumi na Moja baada ya Bunge kuidhinisha pendekezo la Rais John Magufuli jana, lakini akasema alipata taarifa za uteuzi wake kupitia runinga wakati akihamisha vifaa kutoka nyumba za Serikali.

Pamoja na ubashiri kumtaja kuwa mmoja wa watu waliokuwa wanapewa nafasi ya kuteuliwa kuwa mtendaji mkuu wa Serikali, Majaliwa, ambaye alikuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), alisema hakuwa na taarifa kuwa ameteuliwa.

“Kama binadamu nilipata mshtuko na kujikuta nikitoa machozi,” alisema Majaliwa nje ya ukumbi wa Bunge. “Sijui Rais aliona nini kwangu, alitumia vigezo gani kuona mimi nafaa. Lakini namshukuru kwa kuona nafaa na kuniamini kunipa nafasi hii kubwa.

“Sikuwa na taarifa yoyote. Juzi niliapishwa na kama ilivyo kawaida familia yangu, ndugu, jamaa na wapigakura wangu walikuja kushuhudia tukio hili muhimu. Baada ya kuapishwa wengine walishaanza kuondoka tangu juzi na wengine walikuwa waondoke leo (jana) na taratibu zote za tiketi nilishakamilisha.

“Kama ningekuwa na taarifa nisingeingia gharama zote hizo kwa kuwa wengine wameshaondoka.”

Uteuzi wa Waziri Mkuu ulitawaliwa na usiri mkubwa na hilo lilijionyesha jana wakati bahasha iliyokuwa na barua ya jina lake iliwasilishwa bungeni na mpambe wa Rais. Barua hiyo ilikuwa ndani ya bahasha tatu na iliandikwa kwa mkono wa Dk Magufuli, kwa mujibu wa Spika Job Ndugai.

Wakati Ndugai akifungua bahasha hizo, wabunge walionekana kuwa na tashwishi na kuangua kicheko baada ya katibu wa Bunge kufungua bahasha ya kwanza na kukuta nyingine ndani hadi ilipomalizika ya tatu.

“Na barua yenyewe imeandikwa kwa mkono wa Rais,” alisema Ndugai akimaanisha kuwa jukumu la kuandika barua hiyo hakupewa msaidizi wake huku wabunge wakishangilia.

Akisoma barua hiyo, Ndugai alisita mara mbili kutaja jina na kusababisha ukumbi wa Bunge kulipuka kwa kelele kabla ya kutaja Majaliwa na wabunge kupokea kwa makofi na vifijo.

Wakati hayo yakitokea, Majaliwa hakuwapo ndani ya ukumbi wa Bunge.

“Nilikuwa katika harakati za kuhamisha vyombo vyangu kutoka katika nyumba ya Serikali kwa kuwa nilipata nyingine ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) baada ya kipindi cha uwaziri kwisha,” alisema nje ya ukumbi wa Bunge.

Alisema wakati wanatoa vyombo katika nyumba hiyo, mmoja wa vijana waliokuwapo aliwasha runinga kwa ajili ya kuangalia Bunge na yeye akasogea karibu, ndipo akamuona Spika akitaja jina lake kuwa Waziri Mkuu.

Majaliwa, ambaye kitaaluma ni mwalimu, alithibitishwa na Bunge kwa kupata kura 258 ambazo ni sawa na asilimia 73.5 ya kura zote 351 zilizopigwa, huku kura 91 zikimkataa.

“Namshukuru Rais kuniamini na kulileta jina langu bungeni. Nawahakikishia kwamba nitawapa ushirikiano bila kujali vyama vyetu na nitafanya kazi pamoja kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema kwa jukumu ambalo amepewa atashirikiana na wabungewote ili waweze kuwasaidia wananchi waliowatuma bungeni kuwaletea maendeleo.

Alisema anaendelea kuwa Majaliwa yuleyule na ataendelea kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari kwa kuwa amekuwa akishirikiana nao wakati akiwa naibu waziri.

Lakini akatahadharisha kuwa anavyoonekana kuwa ni mtu mpole na mnyenyekevu ni tofauti na alivyo kiutendaji.

“Unaweza kuwa mpole, lakini makini katika utendaji wa kazi. Upole ni tabia ambayo inaweza kumfanya mtu kuelewa jambo na kutekeleza kwa ufasaha,” alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam Tv baadaye jana.

“Lazima kama kiongozi upokee jambo, ulisikilize uchuje upate majibu na lazima usimamie ukweli wa jambo lenyewe. Kwa hiyo suala la upole ni jambo moja na suala la usimamizi wa kazi ni jambo jingine.”

Wabunge wachache waliopata nafasi ya kuchangia hoja ya kuliomba Bunge liidhinishe pendekezo la Rais la kumteua Majaliwa kuwa Waziri Mkuu ambalo liliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu, George Masaju baada ya Bunge kusitisha shughuli zake kwa dakika 45, walimuelezea mbunge huyo wa Ruangwa kuwa ni mtu msikivu, mchapakazi, mpole na mwenye uwezo wa kujibu hoja za wizara yake.

Mbunge wa Isimani (CCM), William Lukuvi, ambaye pia alikuwa akitajwa kuwa angeweza kupewa nafasi hiyo, alikuwa wa kwanza kuchangia hoja akieleza kuwa Rais amependekeza mtu mwenye sifa.

“Kwa wanaomfahamu, sisi tunamfahamu tumefanya naye kazi. Mimi nimefanya naye kazi nikiwa kwenye mwamvuli wa Waziri Mkuu. Lakini pia wabunge wengi wa zamani tunamjua. Hawezi mtu hata mmoja kusema amegombana na Mheshimiwa Majaliwa,” alisema Lukuvi, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Uratibu na Bunge kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi.

“Lakini na Watanzania kwa nafasi mbalimbali za kusikiliza mijadala au hoja mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na Mheshimiwa Majaliwa hapa bungeni au waliopata fursa ya kumuona akitembelea miradi yake huko mikoani wanamjua Mheshimiwa Majaliwa kwamba ni mtu muadilifu, kwanza muadilifu sana.

“Lakini pili amejaliwa kuwa na sikio, ni msikivu. Kassim Majaliwa ni mchapakazi. Tumemshuhudia hapa akidhihirisha uwezo wake kwa kuyasema na kuyafuatilia kwa vitendo katika eneo lake la elimu akiwa naibu waziri wa Tamisemi anayeshughhulikia elimu.”

Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Sera, Utaratibu na Bunge akimbadili Lukuvi, aliunga mkono hoja akimuelezea Majaliwa kuwa mtu asiye na kashfa katika Serikali, mchapakazi na msikivu.

Sifa kama hizo zilitolewa na mbunge wa Nzega Vijijini (CCM), Dk Hamis Kigwangallah aliyesema kuwa Majaliwa ni mwadilifu anayesikia na anayefaa katika nafasi hiyo.

Mbunge wa mwisho kuchangia hoja hiyo kabla ya kupiga kura alikuwa Kangi Ligola wa Mwibara ambaye alimsifu Majaliwa kuwa ni jembe la pili baada ya Magufuli.

Lakini Ligola nusura avuruge halki ya hewa bungeni wakati alipodai kuwa mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea na wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia walishangilia kwa kupiga makofi wakati Spika alipotangaza jina la Majaliwa.

Kubenea alikuwa wa kwanza kutoa taarifa kuwa Ligola alitumia jina lake vibaya na kumtaka afute kauli yake, lakini Ndugai alisema apuuze hayo na kumpa nafasi ya kuchangia hoja, akionekana kutaka kuendelea kusisitiza aombwe radhi, Spika alizima kipaza sauti chake na kumruhusu mbunge mwingiune Andrew Chenge achangie, .

Baada ya mbunge huyo wa CCM kuchangia, Mbatia alisimama akinukuu kanuni aliyoitumia na kutoa taarifa kuwa Ndugai alitumia jina lake vibaya na hivyo kumtaka afute kauli yake kuepusha shughuli za Bunge kuharibika.

Ndipo Ndugai alipomtaka Ligola afute kauli hiyo kuepusha mtafaruku ambao ungeweza kusababishwa na hali hiyo. Majaliwa anakuwa Waziri Mkuu wa 10 wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Waziri Mkuu wa 11 tangu kumalizika kwa utawala wa kikoloni mwaka 1960.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: