Ikiwa siku mbili baada ya Marekani kuitoa Tanzania kwenye nchi wanachama wa Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), hivyo kukosa zaidi ya Sh. trilioni moja, wahisani wengine 10 kati ya 14 waliokuwa wakichangia bajeti ya serikali kuu wamejitoa.
Kutokana na kujitoa huko, Tanzania iko nja panda katia kupata Sh. Trilioni 1.37 zilizotarajiwa kupatikana kupitia wahisani hao katika bajeti ya mwaka 2016/17, ambayo ni ya kwanza kwa serikali ya Rais Dk. John Magufuli.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. Servacius Likwelile, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wahisani wa maendeleo waliobaki kwa sasa ni Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya (EU), Denmark na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Wahisani wengine waliokuwa wakisaidia bajeti kuu ya serikali ni Uingereza, Canada, Denmark, Finland, Germany, Ireland, Japan, Norway na Sweden.
Wakati Dk. Likwalile akitaja wahisani hao wanne waliobaki, huenda wengi zaidi wakajitoa kutokana na tamko la mabalozi na wawakilishi wa nchi zao kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, ambao ndio ulifanya Tanzania ikose fedha za MCC.
Nchi hizo ni Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Uswisi, Uingereza na Marekani.
Sehemu ya tamko la mabalozi hao lilisema: “Tumesikitishwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wa kuendesha marudio ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, bila kuwepo makubaliano ya pamoja baina ya pande kinzani na ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa visiwani humo uliotokana na majadilino baina ya pande husika.
“Ili uwe wa kuaminika na kukubalika ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu.
Tunarejea wito wetu kwa serikali ya Tanzania kuonyesha na kuchukua uongozi katika suala la Zanzibar na kujielekeza katika kupatikana kwa ufumbuzi wa mgogoro huu kupitia mazungumzo baina ya pande husika kwa lengo la kudumisha amani na umoja katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Katika mkutano wa Bunge uliopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliwasilisha bungeni mwongozo wa kuandaa mpango na bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, ambao ulionyesha takribani Sh 1.37 trilioni za maendeleo zitatokana na wahisani.
Mpango huo ulionyesha sura ya bajeti ijayo itakuwa Sh. trilioni 22.99. kwa upande wa matumizi, Sh. trilioni 16.80 ni matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 6.65 kwa ajili ya mishahara.
“Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh. bilioni 6.182 na Sh. bilioni 4.81 ni fedha za ndani sawa na asilimia 77.8 ya fedha za maendeleo,” alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kusainiana mkataba wa makubaliano baina ya serikali ya Japani na Tanzani kwa ajili ya kupatiwa Sh. bilioni 116.4 za kuisaidia bajeti ya 2015/16, Dk. Likwalile alisema kujitoa kwa wahisani hao kumesababishwa na changamoto kwenye nchi zao.
Wakati akisema hayo, tangu mwaka juzi wahisani wengi walianza kusuasua kuchangia bajeti ya serikali kutokana na kashfa za rushwa, ikiwamo ile ya kuchotwa kwa Sh. bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Dk Likwalile alisema mchango wa wahisani katika bajeti ya 2014/2015 ilikuwa Sh. trilioni moja na katika bajeti iliyofuata ilishuka hadi Sh. bilioni 800 kwa bajeti ya 2015/2016 na hadi sasa wamechangia Sh. bilioni 400.
Alisema licha ya wahisani hao kujitoa kuchangia bajeti ya serikali, wamechangia moja kwa moja kupitia kwenye miradi mbalimbali.
Dk. Likwelile alisema bado wana mazungumzo na washirika wa maendeleo hivyo orodha inaweza kuongezeka kwa kuwa wamejipanga katika mfumo mzuri wa fedha.
Alisema wamechukua wataalamu elekezi kuangalia mfumo mzima wa ushirikiano na kwamba katika mwaka mwingine wa fedha kutakuwa na mabadiliko.
Pia alisema kuna uboreshwaji mkubwa uliofanywa na serikali iliyopo madarakani hasa katika matumizi ya fedha pamoja na ukusanyaji wa mapato ambapo tayari wahisani hao wameona kazi nzuri inayofanywa.
“Tunaendelea vizuri na mazungumzo kujitoa kwao katika kuchangia bajeti ya serikali siyo kwamba hawatusaidii bado wanaendelea kufadhili baadhi ya miradi moja kwa moja,” alisema Dk. Likwelile
Alipohojiwa ni madhara gani yanaweza kutokea kwa kukosekana fedha za MCC katika kuendeleza miradi ya umeme vijijini, Dk. Likwelile Wakala wa Umeme Vijijini (REA) haiwezi kuathirika kwa vile fedha hizo ambazo ni dola milioni 472 hawakuziweka kwenye bajeti.
Alisema fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya kuboresha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), miundombinu ya umeme na kuwawezesha wafanyabiasha kupata vifaa vya umeme.
Kuhusu makubaliano waliyoingia baina ya serikali ya Japani na Tanzania, alisema fedha hizo kwa ajili ya kuisaidia bajeti ya serikali pamoja na kuboresha biashara kwa lengo la kuongeza ajira.
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharu Yoshida, alisema mradi huo ni wa kwanza kati ya mitatu ya uendeshaji wa sera za maendeleo na kupitia mradi huu, wataunga mkono juhudi za Tanzania za kuongeza fursa za uzalishaji wa ajira, hasa kwenye sekta binafsi kwa kupunguza gharama za kufanya biashara.
Yoshinda alisema wanaelewa msingi wa kuimarisha utendaji kwenye sekta binafsi na kukuza uzalishaji wa ajira ni muhimu kwa maendeleo zaidi ya Tanzania.
Wakati huo huo, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mchungaji Peter Msigwa, ametoa tamko zito baada ya Tanzania kuenguliwa katika misaada ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC).
Katika tamko hilo, Msigwa ameutaka Umoja wa Ulaya (EU) nayo kuzuia misaada kwa serikali ya Tanzania kutokana na mwenendo wake katika uopngozi wa nchi hususan demokrasia.
Akizungumza jana mjini hapa, Msigwa alisema kambi ya upinzani imesikitishwa na maelezo ya Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dk. Augustino Mahiga, kutowaeleza wazi Watanzania sababu hasa ya serikali ya Marekani kusitisha utolewaji wa fedha hizo za msaada, badala yake kueleza mambo yasiyo na mashiko.
Alisema MCC ilieleza maeneo ambayo Tanzania imekiuka vigezo kuwa ni marudio ya uchaguzi wa Zanzibar na kupitisha Sheria ya Makosa ya Mawasiliano ya Mtandaoni, inayonyima uhuru wa wa kujieleza na uhuru wa kujumuika.
Mchungaji Msigwa alisema kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa Tanzania haikupaswa kushtushwa na uamuzi wa MCC kwa kuwa serikali ilivifahamu vizuri na mapema vigezo vya kustahili kupewa misaada na MCC.
Alsiema inashangaza na kusikitisha kuona Balozi Mahiga, msomi na mwanadiplomasia mzoefu kama akilitia taifa aibu ya mwaka kwa kulalamikia kuonewa.
“Kauli ya Waziri Mahiga za kukataa kukiri makosa yaliyo dhahiri yaliyofanywa na serikali ya CCM zinaweza kabisa kuuweka rehani uhusiano na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia ambao Tanzania imekuwa ikiupata kutoka kwa nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa kama MCC.
“Tukiweka mbele maslahi ya nchi hii yakiwamo ya kudumisha uhusiano wa kimaendeleo na nchi zingine, Kambi rasmi ya Upinzani tunaiomba MCC, Marekani na mataifa mengine kuzipuuza kauli zilizotolewa na Waziri Mahiga, kwani haziakisi ustaarabu wa Watanzania,” alisema Msigwa.
Pia alisema Tanzania si mbia mgeni kwa MCC kwakuwa ilishapokea awamu ya kwanza ya fedha za msaada za dola za milioni 698. Fedha hizo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo - Songea hadi Mbinga.
Aidha, alisema kuwa fedha hizo zilitumika pia kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na kusambaza umeme katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara pamoja na kutandaza njia ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami. CHANZO: NIPASHE
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment