GAZETI LA MWANANCHI LAZOA SIFA KILA KONA MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI DUNIANI TANZANIA.
Mwakilishi wa kampuni ya Mwananchi Communicatins LTD mkoa wa Morogoro, Amina Juma akizungumza jambo wakati akiwasirisha mada katika mdaharo wa maadhimisho ya kuadhimisha kilele cha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani iliyoandaliwa na chama cha waandishi wa habari Morogoro (Moropc) juzi.PICHA/JUMA MTANDA.
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella amelisifia gazeti la Mwananchi kwa kuandika habari nyingi za mikoani ukiwamo wa Mwanza tofauti na magazeti mengine ambayo yamejikita kuandika habari za Dar es Salaam.
Mongella ambaye aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya Mwananchi inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, alisema: “Habari nyingi ziko maeneo ya vijijini ambako pia ndiko wanakoishi wananchi wengi; ni sawa kuzipa uzito habari za Dar es Salaam, lakini siyo busara kupuuza zile za vijijini,” alisema.
Alitoa kauli hiyo wakati akifunga Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari lililofanyika mkoani Mwanza na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa habari yakiwamo mashirika ya Umoja wa Mataifa.
“Baadhi ya magazeti yanafanya vizuri sana, mfano gazeti la Mwananchi limepiga hatua kubwa. Linakuwa na ukurasa wa kila siku wa kuandika habari za Kanda ya Ziwa tofauti na magazeti mengine,’’ alisema Mongella na kuongeza.
“Kuna haja ya kujenga uwezo kwa wanahabari katika maeneo ya wilayani na mikoani ili kuongeza nguvu ya kupata habari kuisaidia Serikali kutimiza wajibu kwa umma.”
Kauli hiyo ilikuja saa chache baada ya Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile kusema vyombo vya habari nchini vinapaswa kutumia mfumo wa uongozi wa MCL ili kukidhi mahitaji ya tasnia bila kuleta mgongano.
Balile ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Jamhuri alisema mfumo huo umesaidia kampuni hiyo kufanya kazi zake kwa uhuru zaidi bila viongozi wake kuingiliana kwenye majukumu yao ya kila siku.
“Wahariri wa Mwananchi wako huru kwa sababu wanafanya kazi bila kuingiliwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wao ambaye ana jukumu la kushughulikia utawala wa ujumla na masuala ya biashara. Lakini chumba cha habari kinabaki kwa wahariri na waandishi wao ili wafanye kazi zao kitaaluma zaidi,” alisema Balile.
Katika hotuba yake, Mongella alisema kuna fursa kubwa kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ukiwemo Mwanza ambazo kama zingetangazwa zingesaidia kuleta mabadiliko makubwa kwa maendeleo ya Taifa hasa ikizingatiwa mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano inayokusudia kuleta mabadiliko ya kiuchumi nchini.
“Natamani sana niendelee kuwa mkuu wa mkoa nisitumbuliwe kabla ya mwakani siku kama ya leo ili shughuli kama hii (kongamano) ifanyike tena Mwanza nikiwa bado hapa ili tushirikiane kwa pamoja kumsaidia Rais Magufuli,” alisema.
Awali mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (Misa-Tan), Simon Barege alisema maadhimisho hayo, yamegongana na matukio matatu ya kihistoria, maadhimisho ya miaka 250 tangu kuanzishwa kwa sheria ya kwanza ya uhuru wa kupata taarifa duniani ambayo asili yake ni Sweden na Finland.
Pia, maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na maazimisho ya miaka 25 ya kuridhiwa kwa Azimio la Windhoek la kanuni za uhuru wa vyombo vya habari na maadhimisho haya yanafanyika ikiwa ni mwaka wa kwanza wa mzunguko wa miaka 15 ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Milenia (SDG)MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment