BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MBUNGE WA CCM VITI MAALUMU AMCHONGEA MWENZAKE KWA NAIBU SPIKA BUNGENI MJINI DODOMA

Mbunge wa CHADEMA viti maalum kutoka mkoa wa Geita, Upendo Peneza katika picha ya maktaba.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Juliana Shonza (CCM) nusura achafue hali ya hewa bungeni baada ya kuomba mwongozo wa Spika kuhusu vazi alilovaa Mbunge mwenzake wa Viti Maalumu, Upendo Peneza (Chadema).

Peneza alikuwa amevaa suruali ya rangi ya kaki ambayo ina mpira kiunoni na blauzi ya rangi ya maziwa.

Shonza akitumia kanuni ya Kudumu ya Bunge namba 149 kifungu cha 1 hadi cha 3 alisema Peneza hajavaa vazi rasmi la bungeni.

Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema kwa sababu mbunge huyo ameketi, atakaposimama atamwona alivyovaa na kutoa majibu ya mwongozo huo.

“Sijamuona amevaa nini,” alisema Dk Tulia na kuamsha kelele za chini kwa chini kutoka kwa baadhi ya wabunge waliotaka asimame ili Naibu Spika aweze kumwona.

Hata hivyo, kauli hiyo ya kutaka asimame ilipokewa na mmoja wa wabunge wa upinzani ambaye alisema; “huo ni wivu wa kike.”

Dk Tulia aliwasihi wabunge hao watulie na kwamba angetoa uamuzi baada ya mbunge huyo kusimama.

Alisema uamuzi huo ni kwa mujibu wa kanuni ya 149 (8) Spika atakaporidhika kuwa mbunge aliyetolewa taarifa kwa mujibu wa fasili ya (7) ya kanuni hajavaa mavazi rasmi ataamuru mbunge huyo atoke nje ya ukumbi. Hadi jioni, Naibu Spika alikuwa hajatoa mwongozo.

Michango Ofisi ya Rais
Mbali na mwongozo huo, wabunge waliponda utaratibu unaofanywa na Serikali wa kuwahamisha watumishi wanaobainika kufanya ufisadi, wizi na uhujumu uchumi wakisema kitendo hicho ni kinyume na utawala bora.

Wakichangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utawala Bora na Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2016/2017, walisema utaratibu wa kuwahamisha watumishi hao umekuwa ukifanya waendelee kutafuna fedha za Serikali wanapohamishiwa.

Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alisema wananchi wa jimbo lake wanaambiwa wachangie maabara na madawati lakini Sh2.2 bilioni zilizotolewa na mgodi wa Resolute katika Wilaya ya Nzega zimeliwa.

“(Dk Khamis )Kigwangalah (Naibu Waziri wa Afya), aliandamana, alipigwa mabomu aliwekwa jela

akapata kasungura ka Sh2.2 bilioni kakaenda halmashauri,” alisema Bashe na kuongeza: “Aliyepiga dili mmoja mmempandisha cheo, huyu mtu aliharibu Ilala na baadaye mkamhamishia Nzega yaani Nzega ni jalala!”

Alisema mtumishi huyo alipohamishiwa Nzega akachukua Sh2.2 bilioni ambazo zilielekezwa kwenye ujenzi wa majengo ya maabara yaliyokuwa yamefikia kwenye linta na amehamishiwa tena mkoani Kagera ambapo ni mhandisi.

Bashe alisema pia kuna mweka hazina mmoja aliyehamishiwa Nzega, akitokea Sumbawanga na baadaye Magu ambako kote ana tuhuma za uhujumu uchumi.

“Leo (jana) amekamatwa na wenzake wakiiba hela za maegesho, wenzake wamewekwa ndani yeye bado anazunguka zunguka tu,” alisema.

Mbunge wa Kasulu Mjini (CCM), Daniel Nsazugwanko aliunga mkono kauli ya Bashe akisema mtumishi anayelalamikiwa kwa ufisadi na kupelekwa wilayani Nzega aliwahi kuiba pia Kasulu na baadaye kuhamishwa.

Alitaka wezi wote wa fedha za Serikali watafutwe, wakamatwe hata kama wakistaafu na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mbunge wa Kondoa Mjini (CCM), Edwin Sanda alitaka utaratibu wa kutumbua majipu usiwe kuwahamisha watumishi waliofanya makosa katika halmashauri kwenda katika maeneo mengine.

Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Severina Mwijage alisema mmoja wa makandarasi wilayani Muleba analindwa na mmoja wa wanaCCM jambo ambalo linamfanya kuendelea kubaki wilayani humo na kupewa zabuni.

Alisema jambo hilo halikubaliki na kuitaka Serikali kuchukua hatua kwa watu wanaobainika kutofanya vyema katika miradi.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace Kiwelu alihoji sababu za watumishi waliokula Sh90 milioni zilizotolewa na wahisani kupitia Mfuko wa pamoja (Busket fund), hawachukuliwi hatua za kisheria na Takukuru. 


Alisema watumishi hao katika Manispaa ya Moshi waliamuriwa na Takukuru kurejesha fedha hizo na ni Sh70 milioni tu zilizorejeshwa.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: