Juma Mtanda, Morogoro.
Chama cha mchezo wa karate mkoa wa Morogoro (TASHOKA) kimepata mafunzo ya mifumo ya utendaji kazi katika hatua ya awali ya ufundishaji klabu za mchezo huo pamoja na mifumo mbalimbali ya mapigano kutoka ngazi ya chini hadi ngazi ya juu kwa siku mbili mkoani hapa.
Mafunzo hayo yalikuwa na lengo la kuwapatia elimu ya kutosha walimu wa mchezo huo ili kufahamu mifumo ya uendeshaji klabu na kudhibiti vilabu holela na kusimamia maadili pamoja na ufundishaji kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo mjini hapa Mwakilishi wa shirikisho la karate la kimataifa la Japan tawi la Tanzania, Jeromeh Mhagama alisema kuwa chama cha karate Morogoro wamegundua kuwa inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kiufundi na utendaji upande wa utawala ndio maana ya kutoa mafunzo hayo.
Mhagama alisema mchezo wa karate unaonekana ni mchezo wa kihuni kutokana na kuwa na walimu wasio na sifa na ujuzi wa kufundisha wanafunzi.
“Mchezo wa karate una maadili yake na mwalimu lazima ayafahamu hayo maadili na kama hawezi kujua atafundisha wanafunzi na kutumia vibaya mafunzo ya karate kwa kuanzisha ugomvi usio na tija mhusika akijivunia uwezo alionao wa kusukumba makeke na ngumi kwa mpinzani.”alisema Mhagama.
Kwa upande wa mwalimu wa klabu ya karate Msamvu, Badi Hamis alieleza kuwa mafunzo hayo yamewaongezea ujuzi na kuahidi kuyatumia vyema katika ufundishaji wa wanafunzi wapya na wale wa zamani.
Mafunzo hayo pia yalihusisha na mazoezi ya kushirikisha matumizi ya mwili katika mazoezi, upigaji wa ngumi kutumia nguvu za miguu ikijumuisha walimu wa karate kutoka vilabu ya Kihonda Karate, Msamvu Karate na DDC karate pamoja na wanafunzi 30 wa madaraja mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment