BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WANANCHI WA JIMBO LA KIBANDA WABOMOLEWA NYUMBA 150 DAR ES SALAAM, KATAPILA LANASA KWENYE MATOPE


Wakazi wa Kibamba Iloganzila, Dar es Salaam, wakiwa wamembeba mwenzao kumpandisha garini kwa ajili ya kumpeleka hospitali, baada ya kupatwa na mshituko alivyoona nyumba yake inabomolewa. Picha na Jackline Masinde

Dar es Salaam.
Vilio na majonzi vilitawala jana eneo la Iloganzila jimbo la Kimbamba jijini Dar es Salaam wakati wa ubomoaji wa nyumba zaidi ya 400 lilipoanza, ambapo hadi saa nne asubuhi nyumba zilizokuwa zimebomolewa ni 150.

Hata hivyo, kazi ya ubomoaji ilishindwa kuendelea baada ya makatapila mawili kati ya matatu yaliyopelekwa kufanya kazi hiyo kuzama kwenye tope, na katapila la tatu lilipojaribu kuyanasua yale mawili nalo lilipata pancha na kushindwa kuendelea na kazi.

Kazi hiyo ya ubomoaji iliahirishwa jana na itaendelea leo, iwapo makatapila hayo yatakuwa yamenasuliwa kutoka kwenye tope na lile lingine kama litakuwa limezibwa pancha.

Ubomoaji huo unafanyika kwa amri ya Mahakama Kuu kutokana na wananchi hao waliojenga kudaiwa kuuziwa viwanja kwenye eneo la Henry Kashangaki na kundi la watu 11 linalotuhumiwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wa Iloganzila.

Shughuli hiyo iliyokuwa ikifanywa na wakala wa Mahakama; Msolopa Investment, iliendeshwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi, huku mmiliki wa eneo hilo, Kashangaki akilindwa na mabaunsa kwa kushirikiana na polisi.

Mwananchi ilifika eneo hilo saa 3:00 asubuhi na kukuta ubomoaji wa nyumba ukiendelea huku wananchi wakiangua vilio, wengine walikuwa wakihamisha vyombo na wengine wakibomoa nyumba zao wenyewe na wengine walikuwa wamekaa tu bila kufanya chochote.

“Kama unavyoona shughuli ya ubomoaji imeanza tangu saa 2:00 asubuhi mpaka sasa zaidi ya nyumba 150 zimebomolewa, na lengo lao nikubomoa nyumba zote zilizopo eneo hili,”alisema diwani wa eneo hilo, Dweza Kolimba.

Mabomu yarindima
Wakati ubomoaji ukifanyika kuliibuka vurugu zilizosababishwa na diwani wa eneo hilo, alipomuuliza mmiliki wa eneo kuhusu kesi iliyoko mahakamani ambayo itasikilizwa Mei 20 mwaka huu.

“Mzee tunaomba utupe maelezo ya kina, unafahamu kwamba una kesi mahakamani ambayo itasomwa Mei 20, mwaka huu juu ya mgogoro wa eneo hili ?” Alihoji diwani huku akiwa amezingirwa na wananchi ambao baadhi yao walisikika wakisema, “akamatwe huyo ..akamatwe huyo haiwezekani aje kuvunja nyumba zetu wakati ana kesi mahakamani,” alisikika mmoja wa wananchi hao.

Kitendo hicho kilifanya wananchi waanze kumzingira mmiliki huyo na kumrushia mawe, jambo ambalo lilisababisha Jeshi la Polisi kuingilia kati na kurusha mabomu kuwatawanya wananchi.

Watano wazimia
Hata hivyo baada ya vurugu hizo ambazo zilidumu kwa dakika 15, shughuli ya ubomoaji iliendelea na wakati huo watu watano walizimia na wawili kati yao waliwahishwa hospitali ya Kibamba na wengine walipewa huduma ya kwanza na kurudia hali zao.

Msaidizi wa Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Liberata Samson akizungumza kwa niaba ya mbunge wa jimbo hilo, John Mnyika ,alisema kaya zaidi ya 200 hazina makazi na hawajui watafanya nini .

“Tunasubiri zoezi hili limalizike tukae na tuangalie tutawasaidiaje wananchi hawa, maana jana(juzi) tumekesha tukihangaika kuzuia ubomoaji huo, lakini juhudi zetu hazikufanikiwa kwa sababu tulikuwa tumechelewa,” alisema.

Wawili wakamatwa
Wakati kazi hiyo ikiendelea kuliibuka kundi la vijana walioanzisha vurugu na kurusha mawe.

“Tumewakamata vijana wawili ambao baadaye walijitetea na kuomba msamaha tukawaachia, lakini baadaye aliibuka kijana huyo huyo ambaye alikamatwa na kuachiwa alikuja na panga pamoja na bisibisi kwa lengo la kufanya vurugu tumemkamata na bado tunamshikilia,” alisema msimamizi wa ubomoaji huo upande wa Jeshi la Polisi, Chuwa Ludovick kutoka Mkoa wa Kipolisi Kinondoni.

Ofisa Mtendaji wa mtaa, Leila Kamganda na watu wawili, Shaha Matibwa na Dominic Kamchope walikimbia na kutokomea kusikojulikana baada ya kuona tingatinga za kubomoa zimefika eneo la tukio wakihofia kupigwa na wananchi.

“Ofisa mtendaji katoweka hajulikani alipo, wanaotuhumiwa kuuza maeneo na wenyewe wamekimbia wamewaacha wananchi wanateseka kama unavyowaona,”alisema diwani.

Wananchi walonga
“Hatuna pa kwenda tutaenda wapi…hapa nilipo hii nyumba ndiyo ilikuwa msaada wangu, imebomolewa nitakuwa mgeni wa nani mimi,” alilalamika Ester Mathias.

Soudi Omary mmoja wa watu waliozimia na kuzinduka baada ya nusu saa alisema nyumba aliyokuwa amejenga aliuziwa na mmoja wa watu waliokimbia kwa kusaidiana na viongozi wa mitaa.

“Nimechanganyikiwa, mke wangu kazimia kakimbizwa hospitali hapa nilipo akili imehama nasuburi wamalize nijenge kibanda cha kujihifadhi leo, nina watoto watatu bado wadogo sijui nitaishije kazi yangu ni dereva wa daladala,” alisema Omary.

Baadhi ya wananchi walikuwa wakimkimbilia mzee Kashangaki na kumpigia magoti huku wakiomba awaone huruma kwani waliuziwa maeneo hayo bila kujua . 


Tunakuomba mzee hili eneo wazazi wangu waliuziwa na mtu na sasa wazee wangu ni marehemu nimeachiwa kama urithi,”alisema.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: