BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SABABU 14 ZINAZOTOA ISHARA YA UMALAYA

 
MATUMIZI mabaya ya mitandao ya kijamii, kupungua kwa hofu ya Mungu, ugumu wa maisha na matumizi holela ya dawa za kuongeza nguvu za kiume.

Na vyakula vinavyosaidia kuongeza hamu ya tendo la ndoa ni miongoni mwa sababu 14 zinazotajwa kuchangia kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wanaosaliti ndoa zao na kuanzisha mahusiano na wapenzi wa ziada maarufu kama ‘michepuko’.

Aidha, marafiki wasio waaaminifu wakiwamo wa wanawake ambao huutambulisha urafiki wao huo kwa jinala ‘shosti’ na pia visa vya baadhi ya watumishi wa ndani (hausigeli) kwa waume wa bosi wao ni sababu nyingine zinazotajwa kuchangia hali hiyo ya kushamiri kwa watu walio na michepuko, hasa kwenye maeneo ya mijini kama katika jiji la Dar es Salaam.

Awali, katika taarifa yake iliyowahi kunukuliwa na gazeti hili wiki mbili zilizopita, Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele, alisema idadi ya watu wanaofika kwao kuhitaji huduma ya vipimo vya nasaba (DNA) ili kujua uhalali wa watoto wao imeongezeka maradufu kulinganisha na miaka iliyopita.

Alisema kwa mwaka jana pekee, watu waliofika kuhitaji huduma ya DNA walikuwa takriban 200; lakini hadi kufikia Juni, idadi hiyo imefikia 203 na matarajio kuwa idadi hiyo itaongezeka mara mbili hadi kufikia watu zaidi ya 400 na hivyo kuzidi maradufu idadi ya wale waliofika kuhitaji huduma hiyo kwa kipindi chote cha mwaka jana.

Prof. Manyele alisema mwaka 2012, idadi ya watu waliohitaji huduma ya vipimo DNA kujua uhalali wa watoto walikuwa 154, mwaka 2013 wakaongezeka hadi kufikia 200, mwaka 2014 wakafikia 220 na mwaka 2015 walikuwa 203, idadi sawa na ile ambayo tayari imeshafikiwa mwaka huu ikiwa ni kipindi cha nusu tu ya mwaka.

Kufuatia takwimu hizo, Nipashe ilishawishika kufanya uchunguzi kujua chanzo cha kuwapo kwa michepuko hasa baada ya kuamini kuwa miongoni mwa sababu zilizoongeza idadi ya watu watakao huduma za vipimo vya DNA mwaka huu ni pamoja na wale wanaodhaniwa kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja na hivyo kutokuwapo kwa uhakika wa baba halisi wa watoto wanaozaliwa.

Katika uchunguzi wake huo uliohusisha mahojiano na watu mbalimbali wakiwamo wataalamu wa Sosholojia akiwamo Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Zainab Rashid, viongozi wa dini kama Sheikh Mkuu, Mufti Aboubakar Zubeir na baadhi ya wanandoa, ndipo Nipashe ilipobaini sababu 14 zinazochangia michepuko.

1. UKOSEFU WA HOFU YA MUNGU

Tabia hii inatajwa kuwa kinara wa sababu nyingine zote za kuwapo kwa michepuko. Watu wanapokosa hofu ya Mungu hufanya lolote kwa nia ya kuridhisha nafsi zao bila kujali juu ya athari zitakazofuatia baada ya kufanya hivyo, na mojawapo ni kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi ya nje ya ndoa zao.

Mufti wa Tanzania, Sheikh Zubeir, aliiambia Nipashe kuwa dini haikubaliani na mtu kuwa na mahusiano yasiyo rasmi na kwamba, kukiuka sharti hilo ni ishara ya kutomhofia Mungu na huko ni kujiweka katika hatari ya kupata adhabu kali iumizayo.

Alisema wanawake pamoja na wanaume waliopata mafundisho ya dini, kamwe hawawezi kujihusisha na mahusiano ya nje ya ndoa ambayo Mwenyezi Mungu huwa hayatambui.

“Maandiko yanasema mwanamke na mwanaume waliopendana waoane, wafunge ndoa ili iwe baraka kwao. Kujihusisha na mapenzi ya nje ya hapo, iwe ni kwa mwanamke au mwanaume, huo ni uchafu kwa tafsiri ya dini,” alisema Sheikh Zubeir.

Alisema katika miaka ya hivi karibuni, kunawatu wamekuwa hawataki kufuata maadili ya dini na jambo hilohuchangia kuondoa baraka katika jamii.

Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) lililopo Ituha jijini Mbeya, Imani Masika, alisema kupungua kwa hofu ya Mungu katika jamii huchangia vitendo visivyozingatia maadili ya dini na mojawapo ni kuongezeka kwa wanandoa wenye michepuko.

2. MITEGO MIKALI YA ‘MASHOSTI’

Hii ni mojawapo ya sababu kubwa zinazotajwa zaidi. Inaelezwa kuwa tatizo hili huwakuta zaidi kina mama ambao bila kujijua, hufanikisha mahusiano yanayozaa ‘michepuko’ baina ya waume zao na marafiki zao (mashosti).

Akizungumza na Nipashe, mwanamama aliyejitambulisha kwa jina moja la Aggy, mkazi wa maeneo ya Sinza, alisema yeye pia ni muathirika wa mitego ya ‘mashosti’ na ilibaki kidogo ampoteze mpenzi wake ambaye alikaribia kunasa jumla kwa kimwana mwingine aliyekuwa rafiki yake wa kufa na kuzikana.

“Shosti wangu tulipendana sana tangu tukiwa chuoni. Nikamtambulisha kwa shemeji yake, wakazoeana na ikafikia mahala wanawasiliana wenyewe bila mimi kunishirikisha. Kumbe mwenzangu alikuwa na yake.

Kuna kipindi nilimshitukia kutokana na namna alivyokuwa akivaa viguo vya ajabu wakati akitutembelea nyakati za wikiendi ambazo mzazi mwenzangu alikuwapo nyumbani. Nilipojaribu kumsema ikawa too late. Kumbe tayari walishakuwa wanatoka kitambo bila mimi kujua,” alisema Aggy na kuongeza:

“Ilibaki kidogo nimpoteze mzazi mwenzangu kwa sababu alishazama katika penzi hilo la mchepuko. Ushauri wangu kwa kina mama ni kutowaachia nafasi mashosti kwa kuamini kuwa hawana madhara kwa waume zao. Wengi huwa ni hatari kwa mitego na hivyo wanaume wachache hujikuta wakisalimika na majaribu yao. Na hii ni sababu mojawapo kubwa ya kuwapo kwa michepuko,” alisema Aggy.

3. VISA VYA ‘MAHAUSIGELI’

Wafanyakazi wa ndani, maarufu kama ‘hausgeli’, hawako nyuma katika orodha ya sababu za kuwapo kwa michepuko. Hawa, kwa mujibu wa watu waliozungumza na Nipashe, baadhi yao hugeuka kuwa michepuko ya siri ya baba wenye nyumba kwa namna mbili, ambazo ni ile ya wao (hausigeli) kukusudia kwa kuwatega waume wa mabosi zao ambao ni kina mama wenye kuwaajiri au hulazimika kuingia kwenye himaya za mababa wakware kutokana na vishawishi vya kibabe.

Akielezea jinsi hausigeli wanavyogeuka kuwa michepuko ya siri, kijana mmoja anayejishughulisha na biashara ya magari, mkazi wa Gongolamboto (hakutaka kujitaja jina), alisema kuna wakati alijikuta akitembea na hausigeli wao baada ya kunasa katika mtego wa ukarimu, unyenyekevu uliopitiliza na jicho zuri la binti asiyekuwa na hatia alilokuwa akimuonyesha mdada wa kazi.

“Mimi na mke wangu wote ni wahangaikaji. Sasa kuna binti wa kazi kutoka Iringa alikuja kwetu baada ya kumaliza kidato cha nne akiwa wa kawaida sana. Na alijawa na tabia njema. Mara jiji likampenda. Kula bure, kulala katika chumba kizuri cha peke yake na mabaki ya vipodozi vya mke wangu vikamfanya abadilike ghafla na kuonekana mrembo wa haja,” alisimulia kijana huyo.

“Kila mara niliporudi nyumbani mapema kabla ya mke wangu, binti huyu akawa akinifanyia ukarimu sana.

Bila kutambua nikajikuta namtongoza na mwishowe akawa nyumba ndogo yangu… tulidumu katika penzi la siri kwa muda mrefu kabla mke wangu hajastuka na kumtimua. Hali hii huwakuta wengi pia,” alisema.

Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Joan, mkazi wa Buguruni, alisema kuwa awali alipotua jijini Dar es Salam akitokea kwao Singida alikuwa akifanya kazi za ndani katika nyumba moja maeneo ya Tegeta. Na huko ndiko yalikomkuta makubwa baada ya baba mwenye nyumba kumtaka kinyumba huku akimtisha kuwa asipokubali atahakikisha anamuamuru mkewe kumtimua nyumbani kwao.

“Niliogopa sana kupoteza kazi. Ni kwa sababu kijijini kwetu nilikuwa nikitegemewa kutuma Sh. 20,000 kila mwezi za kusaidia huduma kwa bibi yangu. Mama alishafariki kitambo na baba yangu sijawahi kumtia machoni. Hata kidato cha nne nilimaliza kwa shida.

Hivyo nikalazimika kumkubali baba mwenye nyumba, baadaye penzi likanoga. Hata hivyo, mkewe alikuja kushitukia baadaye kwa sababu ni vigumu sana kuficha penzi,” alisema Joan.

“Nilikuja kutimuliwa kama mbwa. Siisahau siku hiyo… hata hivyo, sikuhangaika sana kwa sababu nilikuja kupata kazi maeneo ya Ilala kabla ya kuja kukutana na kijana mmoja tuliyependana kwa dhati na hadi sasa niko katika ndoa hiyo,” alisema Joan, aliyeongeza kuwa mumewe anajua kila kitu kuhusu mapito yake kimaisha na hivyo hahofii kusimulia mkasa wake huo.

4. DAWA KUONGEZA NGUVU

Baadhi ya watu waliozungumza na Nipashe walisema kuwa sababu nyingine ya kuwapo kwa watu wengi wenye michepuko jijini Dar es Salaam ni pamoja na tabia ya baadhi yao kutumia kiholela dawa za kuongeza nguvu au vyakula vinavyotajwa kusaidia kuongeza hamu ya tendo la ndoa, hasa supu ya pweza.

“Kuna wanaume hufanya mambo kwa kuiga. Wanatumia dawa za kuongeza nguvu kutokana na simulizi wanazopata kwa rafiki zao na wengine hula vyakula vyenye kuongeza hamu ya tendo la ndoa karibu kila siku… kwao supu ya pweza ni kama maji ya kunywa.


 Matokeo yake, badhi hujikuta hawatosheki kwa wake zao na hivyo kuangukia mikononi mwa michepuko ili kukidhi haja zao,” alisema mwanaume mmoja anayejishughulisha na biashara ndogo ndogo katika soko la Mwanyamala.

5. ULEVI

Mwingine aliyezungumza na Nipashe ni mwanafunzi mmoja wa kike katika Chuo Kikuu cha Mzumbe (kampasi ya Dar es Salaam), aliyesisitiza sharti la kutoandikwa jina lake gazetini. Alisema ulevi wa kupindukia wa badhi ya wanandoa ndiyo chanzo cha kujikuta wakiwa na michepuko.

Akieleza zaidi, mwanfunzi huyo alisema siyo ajabu kumkuta mwanaume akiwa ni mnywaji wa pombe kupita kiasi huku mkewe akiwa ni mchamungu.

Matokeo yake, wanaume wa aina hii huenda katika maeneo wanayouza vilevi wakiwa peke yao kwa sababu wake zao si wanywaji na huko ndiko hujikuta wakisaliti ndoa zao kwa kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na wanawake walio walevi wenzao.

“Njia pekee ya kuzuia michepuko itokanayo na tabia hii ni kwa wanwake kuhakikisha kuwa wanaongozana na waume zao katika maeneo yote wanayokwenda kulewa… hii ni ngumu kidogo lakini hakuna namna rahisi.

Na njia ya kudumu ni kuhakikisha kuwa kila mmoja haangukii mikononi mwa mtu wasiyeendana tabia. Akibadilika kwa kuwa mlevi wakati wewe siyo mlevi unamshitaki kwa wazazi na viongozi wa dini na ikishindikana unaachan naye ili kujihakikishia usalama kwa sababu michepuko kwenye maeneo ya ulevi huambatana na uwezekano wa kupata maambukiuzi ya magonjwa mengi ya hatari,” alisema mwanafunzi huyo.

6. KUTORIDHISHANA

Sababu nyingine inayotajwa kuwa chanzo cha kuwapo kwa michepuko ni hali ya kutoridhishana katika tendo la ndoa baina ya wapendanao. Akizungumza na Nipashe, mwanandoa mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Mudy alisema kuwa katika eneo hilo, mara nyingi wanaokosea ni kina baba.

Akifafanua, Mudy alisema kuwa kwa kawaida, kina mama huhitaji maandalizi ya kutosha kabla ya tendo la ndoa lakini kwa bahati mbaya, wapo wanaume wasiotambua hilo au kupuuzia na badala yake kujioendelea kwa kujipa raha wao wenyewe pasi na kumaliza kiu ya wenzi wao.

“Utakuta jitu linahema na kuvamia mambo haraka utafikiri kuna ugomvi au ni kama kibaka anayeiba mahala. Matokeo yake, hujipa raha wenyewe na kuwaacha wenzao wakiwa bado hawajfika mwisho wa safari.

Vitendo vya aina hii huchangia kuwapo kwa michepuko kwa sababu mwisho wa siku wanawake wa aina hii hujikuta wakilazimika kutafuta burudani nje ya ndoa zao… hapo ndiyo utasikia mke wa tajiri fulani anaangukia kwenye mikono ya hausiboi wake, mtunza bustani au hata dereva wa mumewe.

Na huko mitaani utasikia mama fulani, mke wa bosi Fulani anatembea na muuza mkaa wa nyumba jirani. Hata wanaume wasiporidhishwa na wake zao hujikuta pia wakinasa kwenye mtego huu.


Hii ni sababu mojawapo kubwa ya kuwapo kwa michepuko ndani ya ndoa zetu,” alisema Mudy.

Mhadhiri Zainab wa Chuo cha Ustawi aliiambia Nipashe kuwa baadhi ya wanandoa aliowahi kuwahoji kuhusiana na tabia hiyo, walijibu kuwa hawarishishwi na huduma wanazopata kwa wenzi wao.

Alisema wanaochepuka zaidi kutokana na kisingizio hicho ni wanaume, hasa kutokana na athari za mfumo dume uliopo katika jamii na ambao huwafanya wanaume kuamini kuwa wao ndiyo wa ‘kudekezwa’ na kupata kila wanachostahili katika mapenzi, lakini bila kufikiria pia wajibu wao kwa wake zao.

“Kwa hiyo katika utamaduni wetu, inaonekana mwanaume anachepuka zaidi. Lakini suala la kuchepuka lipo pande zote,” alisema.

7. MITANDAO YA KIJAMII

Kuongezeka kwa matumizi ya simu za mikononi zenye uwezo wa kutuma picha (smart phone) na pia mitandao ya kijamii kama whatsapp, facebook, twitter na instagram kumetajwa vilevile kuwa ni miongoni mwa sababu kubwa zinazochangia kushamiri kwa michepuko katika jamii.

Mwalimu mlezi wa shule moja ya sekondari ya bweni ya wasichana inayoendeshwa kwa misingi ya kidini aliiambia Nipashe kuwa hivi sasa, kupitia simu na mitandao ya kijamii, kazi ya kuwachunga wanafunzi wa kike dhidi ya wanaume wakware imekuwa ngumu kwao.

“Maendeleo haya katika mawasiliano yana faida na hasara zake. Mojawapo ya changamoto zilizopo ni hiyo ya simu na mitandao ya kijamii kutumiwa kwa kazi ya ukuwadi.

Mabinti zetu hujikuta wakigeuzwa kuwa michepuko ya wanaume waliokosa maadili kupitia simu hizi na ndiyo maana tunajitahidi kuzia zisiwepo lakini baadhi ya wanafunzi wamekuwa wajanja zaidi, hawashikiki hata kidogo,” alisema mwalimu huyo.

Aidha, imeelezwa kuwa uwezo wa kutumiana picha za mnato na video zenye kuwaonyesha wahusika wakiwa katika mikao yenye ushawishi dhidi ya wanaume na wanawake kupitia mitandao ya kijamii huchangia pia kuongezeka kwa michepuko katika jamii, hasa kwenye miji kama Dar es Salaam ambako watumiaji wengi wa simu hunufaika na huduma za mitandao mbalimbali ya kijamii kama kama whatsapp, twitter, instagram na facebook.

Mchungaji Masika alisema hivi sasa kuna watu hurusha vitu vingi vya ajabu kwenye mitandao ya kijamii na kwa bahati mbaya, masuala mengi huwabadili wandamu kifikra na baadhi kuangukia katika tabia zinazozaa michepuko.

“Hivi sasa, mitandao ya kijamii ni sawa na mwalimu anayejitegemea… ina ushawishi mkubwa ulimwenguni kote.

Hivi sasa mafundisho ya kidini yamekuwa yakikwazwa na utandawazi,” alisema Mchungaji Masika huku akisisitiza kuwa watumiaji wanapaswa kuwa makini kwa kuitumia mitanbdao kwa mambo yenye kuwajenga kiroho na siyo kuwaharibu.

8. TAMAA/MAISHA YA KUIGIZA
Kuna baadhi ya vijana, wa kike na wa kiume, hujawa na tamaa ya kuwa na vitu vikubwa na vyenye thamani ya juu kuliko uwezo wao kwa sababu tu ya kuiga maisha ya vijana wenzao waliofanikiwa. 


Hali hiyo huchangia pia kuwapo kwa michepuko kwa sababu wale wa kiume hujikuta wakiangukia mikononi mwa kina mama walio kwenye ndoa huku kina dada wakiangukia pia kwa wanaume wenye kuendekeza tabia ya kutoka nje ya ndoa.

9. HALI NGUMU YA MAISHA

Hii ni sababu nyingine inayotajwa kuwa kiini cha kuwapo kwa michepuko. Baadhi ya wanandoa, hasa kina mama hujikuta wakilazimika kutafuta wanaume wengine nje ya ndoa zao ili kupata fedha za kujikimu baada ya waume zao kushindwa kuwapa huduma muhimu.

“Kuna familia hukabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kiasi kwamba mama hujikuta anakosa namna isipokuwa kuwa na michepuko yenye kumpatia fedha za kujihudumia yeye na watoto. 


Mara nyingi familia za hivi ni zile ambazo baba hushindwa kutimiza wajibu wake au hupata matatizo kama ya ugonjwa au hata kufungwa gerezani,” ilielezwa na mmoja wa watu waliozungumza na mwandishi wa Nipashe

10. VISASI

Sababu nyingine inayotajwa kuchangia kuwapo kwa michepuko katika jamii, hasa mijini, ni visasi wanavyokuwa navyo baadhi ya wanandoa dhidi ya wapendwa wao baada ya kubaini kuwa wanasalitiwa.

Baba aliyejitambulisha kwa jina la Joseph, mkazi wa Mbagala Charambe, aliiambia Nipashe kuwa yupo mwanamke mmoja wa jirani yake amebadilika tabia ghafla na kuwa na mahusiano na vijana kadhaa mitaani kutokana na kile kilichobainika kuwa ni kulipa kisasi dhidi ya mumewe ambaye alishamfumania mara kadhaa na kuwatumia viongozi wa kidini na wanaukoo kumkanya mara kadhaa kuwa aache tabia ya kutoka nje ya ndoa bila ya mafanikio.

“Hivi sasa huyo mama hakamatiki mtaani. Ksasi ni sababu mojawapo inayochangia kuwapo kwa michepuko mingi jijini Dar es Salaam,” alisema Joseph.

11. KUONGEZEKA KWA GESTI

Mmoja wa watu waliozungumza na Nipashe alisema hivi sasa, nyumba za kulala wageni maarufu kama ‘gesti’ zimetapakaa karibu katika maeneo yote jijini Dar es Salaam. 


Na hadi sasa, zipo nyingi nzuri za ghorofa zinazoendelea kuchipuka kama uyoga huku zikitambulishwa kwa majina yasiyohusisha neno ‘guest house’ na badala yake kutumia majina ya ‘inn’, ‘lodge’,‘executive’, ‘annex’, ‘park’ na hata ‘hoteli’.

“Tuambiane ukweli, hivi tangu lini hoteli ya kweli ikajengwa kwenye mitaa yetu ya uswahilini kama Tandale, Gongolamboto, Buguruni na Vingunguti? 


Hizi ni gesti tu, na nyingi husaidia kushamiri kwa michepuko kwa sababu ndizo ambazo wake za watu na waume za watu humaliza haja zao na wapenzi wao wan je ya ndoa,” alisema mtu huyo.

12. FILAMU CHAFU

Kukithiri kwa uuzwaji wa filamu mbaya zinazoonyesha mambo ya chumbani kwenye mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kunatajwa kuwa ni sababu nyingine ya kushamiri kwa michepuko kwa sababu baadhi ya watu hutaka watu wa kujaribu nao yale wanayoyaona kwenye filamu hizo.

“Yapo mambo ya ajabu kwenye filamu hizi za Kizungu ambayo baadhi ya wanandoa huyashuhudia lakini huogopa kuyajaribu kwa wenzi wao… matokeo yake, hutafuta wapenzi wengine na kujaribu nao. Hapo hujikuta wakinasa na michepuko kuendelea kuongezeka,” alisema Douglas, mkazi wa mitaa ya Kariakoo jijini Dar es Salaam.

13. MISIFA YA KIJINGA

Mhadhiri Zainab aliiambia Nipashe kuwa sababu nyingine ya kushamiri kwa michepuko katika jamii ni mila potofu katika baadhi ya makabila, hasa zile za wanaume kujiona ndiyo ‘vidume wa shoka’ pindi wanapokuwa na msururu wa wanawake nje ya ndoa.

“Tamaduni nyingine zinadhani kuwa mwanaume kuchepuka ni ujasiri, wakiamini mwanaume hawezi kuwa na mwanamke mmoja,” alisema Zainab.

14. SABABU YA KISAIKOLOJIA
Mhadhiri Msaidizi, Zainab, alisema kuwa hivi sasa, matukio ya watu kutoka nje ya ndoa au kuwa na wapenzi wasio rasmi zaidi ya mmoja yamekuwa mengi na hali hiyo inahatarisha
afya ya wahusika, hususan wanandoa.

Alisema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kuanzia jana, yeye ameshakutana na mashitaka manne yanayohusiana na malalamiko ya wanaume dhidi ya wake zao, wakidai kuwa wana wapenzi wengine nje ya ndoa zao. Alisema wahusika wana umri wa kati ya miaka 35 hadi 45.

Alisema mbali ya kuwapo kwa sababu nyingi zinazosababisha watu kutoka nje ya ndoa, lakini mojwapo kubwa ni ya Kisaikolojia na hii hutokana na baadhi ya watu kuwa na matarajio kuwa ni lazima wapate huduma fulani katika ndoa na hilo linaposhindikana, hakuna njia nyingine kwao isipokuwa ni kutafuta wapenzi wengine nje ya ndoa zao.

Zainab alisema ili kuepukana na vitendo vya kushamiri kwa mahusiano yasiyo rasmi nje ya ndoa, jamii nzima wakiwamo wazazi wanatakiwa kuongeza umakini katika malezi na kusisitiza maadili mema kwa kuwa kinyume chake, jamii itazidi kuharibika. 


“Malezi bora yenye kuzingatia misingi ya dini ni muhimu kwa familia. Fikiria katika familia ambayo mtoto kila siku anashuhudia mama na baba wakigombana kwa sababu ya hiyo inayoitwa michepuko. 

Ni wazi kwamba mtoto wa hivi atakuwa na tabia hiyo pia ukubwani mwake… wazazi wanandoa wazingatie maadili,” alisema Zainab.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: