MPOKI BUKUKU KUAGWA LEO DAR, KUZIKWA KESHO DODOMA
MPIGAPICHA Mwandamizi wa The Guardian Limited, Mpoki Bukuku (44) aliyefariki dunia juzikati baada ya kupata ajali ya gari, mwili wake unatarajiwa kuagwa leo na kuzikwa kesho mkoani Dodoma.
Msemaji wa familia, ambaye ni kaka wa marehemu, Gwamaka Bukuku, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mwili wa marehemu utaagwa nyumbani kwake, Tabata Kimanga.
“Mwili wa marehemu utachukuliwa Jumatatu (leo) kutoka hospitali yaTaifa ya Muhimbili na baada ya hapo utaletwa hapa nyumbani kwake kwa ajili ya kuagwa,” alisema.
Bukuku alisema baada ya taratibu hizo kumalizika, mwili huo utasafirishwa na kupelekwa nyumbani kwa wazazi wake, Dodoma kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika kesho.
CHADEMA YAMLILIA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeelezea kupokea kwa masikitiko taarifa za msiba wa Mpoki Bukuku.
“Kwa hakika tasnia ya habari imempoteza mmoja wa wapambanaji hodari ambaye hakusita kuitetea na kuilinda kamera yake hata mbele ya vitisho vya aina yoyote ile vilivyolenga kuminya uhuru wa habari,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema Mpoki Bukuku ameondoka katika kipindi ambacho vyombo vya habari na uhuru wa habari kwa ujumla, ambao aliutetea kwa vitendo, ukipitia katika changamoto kubwa na kuongeza kuwa ujasiri na uthubutu wake ungehitajika sana katika nyakati hizi.
“Chadema inaungana na tasnia nzima ya habari katika kumlilia Bukuku kwa majonzi makubwa. Tunatoa pole na salamu za rambirambi kwa familia yake, ndugu, jamaa, marafiki, wafanyakazi wenzake wa The Guardian Ltd, wanahabari wenzake na wadau wa habari kwa ujumla nchini kwa kuondokewa na mpendwa wao,” taarifa hiyo ilieleza.
Alhamisi ya wiki hii, Mpoki aligongwa na gari katika eneo la Mwenge wakati akitoka kazini na kuvunjika miguu yote miwili na mkono mmoja.
Baada ya kufikishwa hospitalini akiwa anapatiwa matibabu, juzi alifariki dunia katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI).
0 comments:
Post a Comment