BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WATU WATANO WAUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA ASKARI

VILIO na simanzi vimewakumba wakazi wa Oldonyosambu, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha baada ya askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) kudaiwa kuwaua kinyama kwa kuwapiga risasi watu watano na kujeruhi wengine saba kwa kile kilichodaiwa kuingiza mifugo ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Mlima Meru.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani humu, linawashikilia askari sita wa Suma JKT kwa mahojiano.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati akizungumza na Nipashe jana na kukiri jeshi hilo kuwashikilia askari hao wakati uchunguzi ukiendelea.

Watu walioshuhudia walisema tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la Madukani, Mtaa wa Maua uliopo Kata ya Oldonyosambu.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti, mashuhuda wa tukio hilo, Samson Abel na Thobias Kivuyo, walidai wafugaji kadhaa waliingiza mifugo eneo la msitu wa hifadhi hiyo wakisaka malisho ya mifugo yao.

Waliendelea kusimulia kuwa askari wa Suma JKT wanaolinda msitu huo waliikamata mifugo hiyo kwa lengo la kuipeleka kituo kidogo cha polisi cha Oldonyosambu.

Hata hivyo, mashuhuda hao walidai kuwa wakiwa njiani kuipeleka mifugo hiyo kituoni, ghafla, kwa sababu wanazozijua wenyewe, askari waliwashambulia wachungaji wawili kwa risasi na kuwaua papo hapo.

Nipashe haikuweza kuthibitisha madai ya mashuhuda hao moja kwa moja, hata hivyo.

Mashuhuda hao waliendelea kueleza kuwa wakati askari hao wakiipeleka mifugo hiyo kituo cha polisi, waliingia mtaani na kuwatishia wananchi kwa kupiga risasi juu hewani kwenye maeneo ya makazi ya wananchi.

Walidai kuwa kitendo hicho kilisababisha watu wawili zaidi waliokuwa wakipalilia karoti kwenye mashamba yao kuuawa.

Aidha, walidai, risasi zilizorushwa hewani zilijeruhi raia wengine saba waliokuwa wakikimbia kuokoa maisha yao.

Diwani wa Kata ya Odonyosambu, Raymond Lairumbe, akizungumzia tukio hilo, alisema askari hao wanaolinda msitu huo, wakiwa kwenye lindo walikuta mifugo ya wananchi ndani ya msitu.

Alisema waliwakamata na kuwashambulia kwa risasi vijana wawili waliokuwa wanachunga mifugo hiyo ambao walifariki dunia papo hapo kutokana na kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na majeraha makubwa waliyokuwa wameyapata mwilini.

Diwani huyo alidai kuwa mmoja wa majeruhi alifariki dunia baadaye na hivyo kufanya idadi ya watu waliokufa kufikia watano.
Alisema wamesikitishwa na tukio hilo la wananchi kuuawa kama wanyama bila kujali haki za binadamu.

Aliitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria askari waliofanya kitendo hicho.

Habari zilizopatikana jana katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, zilieleza kuwa ilipokea maiti za watu wanne wanaodaiwa kufa kutokana na tukio hilo.

SILAHA ZA JADI
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Mkumbo, akizungumzia kwa kina tukio hilo katika mahojiano na Nipashe mjini humu jana, alisema lilitokea juzi majira ya saa 11 jioni baada ya baadhi ya wananchi wa Oldonyosambu kuvamia eneo la msitu kwa kuingiza ng’ombe ndani ya hifadhi ili kuwapatia malisho.

Alisema tukio hilo la kuuawa kwa watu watano na wengine saba kujeruhiwa lilitokea baada ya askari kukamata ng’ombe 45 waliokuwa wameingizwa ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ya malisho.

Alisema baadhi ya wananchi walichukua silaha za jadi kukabiliana na askari hao ndipo wakaamua kufyatua risasi kwa lengo la kujihami, lakini risasi zikawapata wananchi hao.

Kamanda alisema baadhi ya majeruhi wanapata matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Arusha ya Oltrumet.

Kamanda Mkumbo aliwataja watu waliofariki dunia kutokana na tukio hilo kuwa ni Mbayani Melau (27) ambaye ni mfugaji na mkazi wa kijiji cha Kandaskirieti, Julius Kilusu (45) mkulima na mkazi wa Kandaskirieti, Lalashe Meibuko (25) mkulima na mkazi wa Kandaskirieti na Seuri Melita (32) mkazi Olkokola.

Alisema miili yote imehifadhiwa katika Hospitali ya Mount Meru kwa uchunguzi zaidi.

Aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni wakulima William Ngirangwa (29), Mathayo Masharubu (34), Julius Lazaro (32), Evalyn Melio (28) na mtoto mwenye umri wa miaka 13 (jina tunalihifadhi), wote wakazi wa kijiji cha Kandaskirieti ambao wamelazwa Mount Meru na hali zao siyo nzuri.

WAKITOKWA MACHOZI
Huku wakitokwa na machozi, majeruhi wasimulia jinsi baa hilo la kupigwa risasi na askari lilivyowakumba.

Majeruhi hao walidai askari hao walikuwa wamevaa mavazi kama ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na SUMA JKT, wakiwa katika maeneo tofauti ya mjini Oldonyosambu.

Akiwa kwenye wodi jana, Julius Lazaro (32), alisema anashindwa kuelezea tukio hilo kwa kuwa haelewi kwanini alipigwa risasi wakati yeye alikuwa nyumbani kwao eneo la Madukani.

"Mimi nikiwa nyumbani, tulisikia milio ya risasi msituni na ghafla likatokea kundi la watu likirusha mawe na kushtuka tukaona askari wanatufuata kutuuliza nani aliyewarushia mawe, tukawaambia hatuwajui, wakaamuru tupotee, tukiwa tunaondoka eneo hilo, nikapigwa risasi mguuni,” alisema.

Alisema askari hao walikuwa wamevaa mavazi kama ya kijeshi na wengine nguo kama za askari wa hifadhi na baadhi yao walikuwa na suruali za kiraia na fulana.

Majeruhi mwingine Ngirangwa (29) akisimulia kwa uchungu tukio hilo, akiwa wodini humo, alisema siku ya tukio alikuwa akitoka kazini kuchimba moramu, lakini akiwa njiani kurejea nyumbani, alisikia ngurumo za silaha za moto.

"Wakati naendelea kutembea kufika eneo la Madukani, nilishtuka kuona na mimi napigwa risasi ya mguuni, tumboni na mkononi, na hapo nilianguka nikapoteza fahamu. Sikuelewa kinachoendelea hadi nimejikuta nipo wodini," alisema.

Majeruhi huyo alisema yupo wodini na ndugu zake hawafahamu chochote kuhusu kilichomkuta.

Alisema kuwa anajisikia maumivu makali kwa kuwa alikuwa bado hajapatiwa matibabu ya kutolewa risasi mwilini.

Majeruhi mwingine, Mathayo Masharubu (34) alisema siku ya tukio alipigiwa simu kuwa kuna watu wameuawa katika shamba la msitu wa serikali ambao walitokea Olkokola, lakini akashangaa kusikia risasi zikirindima madukani alikokuwa na kuanza kukimbia kuondoka eneo hilo akitumia pikipiki.

Alisema kuwa wakati akijaribu kuokoa maisha yake, risasi ilimpata kwenye moja ya makalio yake.

Alidai kuwa kisa cha askari hao kupiga risasi ovyo ni hasira za wakazi wa Olokokola kuwarushia mawe, lakini upande wa oldonyosambu hakukuwa na mtu aliyerusha mawe.

"Nilipopigwa risasi, nilishtuka sana na kupoteza fahamu hadi kujikuta niko wodini, naomba msaada wa viongozi serikali ili nitolewe risasi mwilini mwangu kwani hadi sasa hatujapata huduma yoyote sababu hatuna fedha na tukio limetukuta ghafla," alisema.

Nipashe pia ilishuhudia wodini humo mtoto mwenye umri wa miaka 13 anayesoma katika Shule ya Msingi Leminyoli, akiwa anashindwa kuzungumza kutokana na maumivu aliyonayo ya kupigwa risasi tumboni na kutokea mgongoni.

MIILI HAITAZIKWA
Diwani Lairumbe alisema miili hiyo haitazikwa hadi viongozi watakapofika kuzungumza na wananchi na kwamba huo ni uamuzi wa wananchi.

Alisema askari hao walidhamiria kuua sababu waliofariki wote wamepigwa risasi kichwani.

Diwani huyo alisema kiwa baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa wananchi wake, alikwenda polisi kuomba kibali cha kuingia msituni ili kuchukua miili hiyo ya watu wanne waliokuwa wameuawa. 


"Tulichukua miili hiyo hadi Hospitali ya Mkoa Mount Meru kuhifadhi na baadhi ya majeruhi wamelazwa Hospitali za Selian, Mount Meru na Olturument," alisema.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: