BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ASKOFU KANISA LA UFUFUO NA UZIMA AMTISHA MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM PAUL MAKONDA

ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye aliisaidia Polisi kwa siku tatu kuhusu biashara ya dawa za kulevya, ametishia kuamuru mapepo anayotoa kanisani yaingie kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Makonda ndiye aliyetangaza kumtaka Gwajima pamoja na jumla ya wanasiasa na wafanyabiashara 64 kufika Kituo Kikuu cha Kati cha Kanda Maalum ya Dar es Salaam Ijumaa kwa ajili ya mahojiano kuhusu biashara ya madawa ya kulevya.

Askofu Gwajima alisema licha ya jina lake kutajwa katika tuhuma hizo nzito, hana mpango wa kumshtaki Makonda kwa kuwa atakuwa anaishtaki serikali.

Alisema Makonda ni mteule wa Rais John Magufuli, hivyo kumshtaki Mkuu huyo wa Mkoa ni sawa na kumshtaki aliyemteua pia na hayuko tayari kufanya hivyo kwa kuwa anavutiwa na Rais na utendaji kazi wa serikali yake.

“Mimi najua cha kufanya," alisema Gwajima wakati akizungumzia kanisani kwake jana, hatua ambazo atachukua nje ya kumshtaki Makonda mahakamani.

"Yesu alipopita mahali, akakuta kuna mtu ana mapepo 2,000, alivyoanza kuyatoa yakamwambia turuhusu twende kwa wale nguruwe," alisema.

"Sasa sisi mapepo yatakapouliza tutayaambia nguruwe ni nyama yasiende huko, tutayaambia pa kwenda."

Aidha, Gwajima jana aliwaeleza waumini wake yaliyomkuta huku akiwaonyesha nyaraka za ukaguzi baina yake na Jeshi la Polisi.

Alhamisi, Askofu Gwajima alifika kwenye Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam baada ya jina lake kuwa miongoni mwa majina 65 yaliyokuwamo katika orodha ya pili ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam huyo ya watuhumiwa wa dawa za kulevya aliowataka waripoti polisi Ijumaa.

Lakini Akofu huyo aliamua kuripoti siku moja kabla na kushikiliwa na jeshi hilo hadi juzi.

Askofu Gwajima alifika kanisani hapo majira ya 5:18 asubuhi na kulifanya kanisa kuzizima kwa shangwe kwa takribani dakika 10 wakati anaingia huku ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa kanisani hapo na walinzi wa kanisa hilo waliokuwa kwenye sare ya suti nyeusi na tai nyekundu na miwani ya rangi nyeusi.

Nipashe ilishuhudia kanisa hilo likiwa limefurika maelfu ya waumini huku wengine wakionekana kukosa mahali pa kuketi na kulazimika kusimama na wengine kuketi kwenye viunga vya nje ya kanisa hilo.

Baada ya Askofu Gwajima kuingia kanisani na kuketi, wasaidizi wake walitangaza kuwa baada ya kutoa sadaka, Askofu huyo atazungumza nao, tangazo ambalo 'lililipua' zaidi kanisa hilo kwa shangwe huku baadhi ya waumini wakishangilia kwa kunyanyua viti.

Utoaji sadaka ulipomalizika, Askofu Gwajima huyo alisimama na kueleza kuwa kabla ya kuhubiri neno la Mungu, aeleze kwanza kuhusu kilichompata polisi.

Alisema taarifa za kutakiwa kuripoti polisi alizipata Jumatano wakati akiwa kwenye chopa lake wakiwa safarini na wenzake kuelekea Dodoma kutoa huduma ya kiroho.

Askofu Gwajima alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, alimtaka rubani wake ageuze chopa kurejea jijini Dar es Salaam ili siku iliyofuata (yaani Alhamisi) aripoti alikotakiwa.

"Nisingeweza kuendelea na safari ya kwenda kutoa huduma kwa sababu nilikuwa tayari nimeshatajwa kwenye hizo tuhuma na nisingeeleweka kwa wale niliokuwa naenda kuwapa huduma," alisema.

Askofu Gwajima alisema kuwa baada ya kufika kituoni, alihojiwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam. Kamishna Simon Sirro na kumweleza kuwa tuhuma dhidi yake zimetokana na chuki.

Alisema alimwomba Kamishna Sirro amruhusu aeleze kwa uhuru kwa kuwa anayemtuhumu kwa kashfa hiyo, aliwahi pia kumtuhumu Kamanda huyo kwa kufumbia macho biashara ya uvutaji shisha jijini.

"Lakini Sirro aliniambia kwamba lazima wanihoji na nikamwambia niko tayari kwa sababu tangu nizaliwe sijawahi kunywa pombe aina yoyote, kuvuta sigara wala kwenda 'disco'," alisema Askofu Gwajima.

Alisema yuko tayari wampime na hata wakibani ana pombe mwilini mwake, waseme anatumia dawa za kulevya.

Askofu Gwajima alisema kuwa baada ya kuhojiwa, alipelekwa kupimwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kwamba upimaji uliofanyika huko ulikuwa wa wazi na anaamini Ofisi ya Rais ilikuwa na wawakilishi katika kupimwa kwake huko.

Alidai hakubainika kuwa na tatizo katika vipimo hivyo lakini polisi wakawa wanamhoji kuhusu uhalali wa mali zake ikiwamo ndege na chopa na kuwajibu kuwa umetokana na huduma ya neno la Mungu.

Aliongeza kuwa, baada ya vipimo hivyo, alikwenda na polisi hadi nyumbani kwake ambako alifanyiwa ukaguzi.

DAWA ZA KULEVYA
Askofu huyo alidai kuwa polisi hawakukuta dawa za kulevya nyumbani kwake huku akiwaonyesha waumini wake baadhi ya nyaraka za ukaguzi alizodai kupewa na polisi. Nipashe haikuthibitisha nyaraka hizo, hata hivyo.

"Nyumba yangu ina gorofa tatu, sasa polisi walivyosema wakakague nyumbani kwangu, niliwaambia twende na tulivyofika watu wote waliokuwa nyumbani walitoka nje. Kwa hiyo polisi walikagua karatasi kwa karatasi, dro kwa droo na mpaka kumaliza ilikuwa ni saa nane usiku," alisema.

"Baada ya kukagua na kuona hakukuwa na kitu, niliwaaomba waandike kwamba hawajakuta kitu, waliandika na nikaomba wanipatie na mimi ‘copy’ (nakala), wakanipatia, hii hapa (alionyesha kanisani).

"Nimepelekwa hadi kwa Mkemia kupimwa na niliwaambia hata wakikuta sigara au pombe waseme ni dawa lakini kazi ilifanyika kwa uwazi, na baada ya kupimwa sikukutwa na kitu, walikagua hadi akaunti zangu za benki hawakukuta kitu.

"Naomba tusiwalaumu polisi, wanafanya kazi ngumu sana na wanateswa kama sisi, wanaambiwa waende wakakague kwa mtu hata kama hakuna kitu."

Askofu Gwajima alisema Kamanda Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu, Mkuu wa Kikosi cha Upelelezi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hawapaswi kulaumiwa katika kukamatwa kwake.

Alisema vita dhidi ya dawa za kulevya inapaswa kuungwa mkono lakini hakubaliani na utaratibu unaotumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (Makonda).

"Kwa mfano mimi na Makonda huwa tunawasiliana na hata ukiangalia simu yangu, utaona meseji zake, alishawahi kufika hapa kanisani kwetu tukampa na kipaza sauti akazungumza, kwanini alishindwa kusema kama tunauza, naamini anafanya hivi kwa lengo la kuchafua majina ya watu kwa sababu anazozijua mwenyewe," alisema.

Akizungumzia maisha ya 'selo', Askofu Gwajima alisema hafurahii kuachiwa kwake kwa sababu amewaacha watu ambao hawana mtu wa kuwasemea na hawajapimwa wala kukaguliwa kama ilivyofanyika kwake.

Alisema kuwa akiwa selo, alikutana na askari polisi ambao walituhumiwa katika sakata hilo na anawaonea huruma kwa sababu hawajui hatma yao na hawana mtu wa kuwatetea.

"Niwaambie kitu, msilaumu polisi wala ofisi ya Rais narudia tena kwa sababu hawahusiki na hili, isipokuwa ni kiumbe mmoja tu labda na watu wake wawili watatu ndio wameibuka katikati, polisi nao wanateseka kama sisi, tangu wametuhumiwa wako ndani mpaka sasa na hakuna wa kuwasaidia, hawawezi kuzungumza kwa sababu wataonekana ni waasi," alisema.

"Na kwa sababu hiyo, mimi nimejivika rasmi kombati kusema kwa ajili yao. Namuomba Rais aingilie suala hili maana wanateseka, polisi wamekaa kule ndani wamejikunyata hawana mtetezi, eti Makonda ameunda tume, hivi kesi ya ngedere unampelekea nyani?" Alihoji.

DK. WILLIBROD SLAA
Askofu Gwajima pia alidai kutumiwa ujumbe na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, akieleza kushtushwa na kuhusishwa na kukamatwa kwake kwa tuhuma za dawa za kulevya.

Alisoma ujumbe huo kanisani akidai umetumwa kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp ambao Dk. Slaa anampa pole kwa kutuhumiwa katika sakata hilo. Nipashe haikuweza kuthibitisha ujumbe huo kama kweli umetoka kwa Dk. Slaa.

Katika ujumbe huo, Askofu Gwajima alidai Dk. Slaa alimwambia ameonewa na haungi mkono utaratibu uliotumika katika kumtuhumu na yuko tayari kutoa ushahidi juu ya askofu huyo endapo atahitajika kufanya hivyo.

Askofu Gwajima alisema leo anarejea tena kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa masharti aliyopewa na jeshi hilo.NIPASHE
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: