MAHAKIMU NA MAJAJI KUKIONA CHA MOTO KWA KUVUGA KESI ZA MADAWA YA KULEVYA KATIKA MAHAKAMA
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rodgers Sianga ameanza kazi rasmi baada ya kutangaza kuwashughulikia mahakimu na majaji wanaotuhumiwa kudhoofisha vita dhidi ya dawa za kulevya pamoja na maofisa wa serikali walioshiriki kuingiza viuatilifu vya dawa za kulevya.
Sianga alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusu kutangazwa kwa awamu ya tatu ya kutangaza orodha ya majina ya watu wanaosadikiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Kamishna Mkuu huyo aliyeteuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na kuapishwa juzi na Rais John Magufuli, alisema mambo anayoanza nayo katika vita dhidi ya dawa za kulevya, amemuagiza Kamishna wa Operesheni, Mihayo Msikhela kuwatafuta maofisa wa serikali walioisaidia nchi kupitisha tani 21,000 za viuatilifu vya dawa za kulevya mwaka jana.
“Mwaka jana, maofisa wa serikali waliisaidia nchi kupitisha tani hizo.
Nataka Kamishna wa Operesheni watu hawa watafutwe, wakamatwe na wahojiwe, wakipatikana na hatia wafunguliwe mashitaka kama watu wengine wanaoingiza dawa la kulevya,” alisema Sianga ambaye kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa Mkoa wa Kilimanjaro.
Pia Sianga alisema wanaandaa orodha ya mahakimu na majaji ambao kwa makusudi wamekuwa wanavuruga kesi za dawa za kulevya kwa makusudi na watakaobainika wanahusika watawekwa ndani kwa kuwa hakuna aliye juu ya sheria.
“Tutaanzia hapa kwa sababu kesi zetu nyingi zimekuwa zikichukua muda bila sababu mtu anakaa anajua kwa sababu yeye ni jaji anasema katika kesi yake ataamua anachotaka.
Kuna kesi moja Tanga mtu kakutwa na kilo 50, jaji anasema anamuachia kwa kuwa hakuna uthibitisho,” alisema Sianga na kuongeza: “Mtu mwingine alikutwa na dawa, alibeba kete 180 tumboni, lakini jaji anasema huyu mtu nikimuangalia naona ana vidonda vya tumbo, lakini si daktari.
Hakuna aliye juu ya sheria.
Hawa lazima tuwa-impreach.
” Alisema ari ya mapambano ya dawa za kulevya aliyoanzisha Rais Magufuli na Makonda watakwenda nayo ili kuhakikisha mapambano yanafanikiwa na kuwaondoa wafanyabiashara wa dawa hizo ambao wamekuwa wakitamba na wengine kuwadhalilisha watu kwa sababu ya fedha zao wanazopata kupitia dawa hizo.
“Kuna mtu mmoja yeye ilikuwa ikifika jioni anawaita wanaume anawaambia wakimbie atakayeshinda anampa dola mia moja, wanaume wanavaa bukta zao wanakimbia, hii ni udhalilishaji.
Hatutamuacha mtu atakayebainika kuhusika,” alibainisha Kamishna Mkuu Sianga.
“Wauzaji wa dawa za kulevya wametesa familia kwa sababu mtumiaji anaondoa akiba na samani iliyokuwa ndani ya nyumba, wengi ambao hamjapata madhara hamjui mateso ya dawa.
Wafanyabiashara hawa wameleta huzuni ndani ya nyumba, hatuna msamaha na mtu tutawashughulikia.
” Aidha, alifafanua kuwa biashara ya dawa za kulevya imekuwa ikichangia mfumuko wa bei kwa kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wana fedha, wamekuwa wakinunua vitu kwa bei ya juu na kwa kuwa mfanyabiashara anataka fedha, anaamua kupandisha bei na kusababisha watu wa hali ya chini kushindwa kununua vitu.
“Unakuta mfanyabiashara anauza samaki pale Feri na anauza kwa bei ndogo tu, lakini akitokea mfanyabiashara wa dawa za kulevya kwa kuwa ana fedha zake za dawa basi samaki wa elfu moja atanunua kwa elfu tano,” alieleza akionesha madhara ya dawa za kulevya.
Aidha, Sianga alizitaja athari mbalimbali zinazotokana na matumizi ya dawa za kulevya, kwa kubainisha kuwa mtu anapotumia mirungi anaharibu mfumo wa chakula na kusababisha kansa kwenye tumbo, koo na mdomo na kumfanya akose hamu ya kula na kumfanya mwanamume asiwe mwanamume.
Aliongeza kuwa athari za matumizi ya bangi yanatafuna kichwa cha mtu, mtu anakuwa na mawenge na hawezi kufikiria tena, pia alisema heroine nayo ina athari kubwa kwa kuwa inaharibu akili na mwili.
“Tulikutana na mtu mmoja ambaye ni muathirika tukazungumza naye, lakini yeye anasema msinisemeshe naongea na Rais Mkapa na Clinton wakati hapo alipokaa hakuna mtu, kwa hiyo utaona ni kiasi gani dawa hizi zina madhara hatuwezi vumilia,” alieleza zaidi.
Alisema nchi imekuwa ikipitisha kiasi kikubwa cha dawa, mwaka jana eneo la kusini pekee lilipitisha tani 20 za dawa, hivyo kwa kuwa wanapambana na uingizwaji wa dawa za kulevya wanazitambua njia zote zinazotumika kupitisha.
Pia alisema suala la dawa sio la Mkoa wa Dar es Salaam, pekee bali ni kwa mikoa yote, hivyo watafanya kikao na mikoa yote waandae orodha ya wahusika wa biashara hizo katika mikoa yao na watafanya hivyo kwa Zanzibar ili kuondoa mwanya wa watu hao kuhamishia biashara zao huko baada ya kuondolewa nchini.
Baada ya kumaliza mkutano huo, Kamishna Sianga alitangaza kusakwa na kufikishwa mbele ya Mamlaka hiyo mshukiwa aliyemtaja kwa majina ya Ayub Kiboko.
Aidha alisema kwamba wapo watu ambao wako nchi za nje, nao watawafuata huko waliko.
Alitaja nchi hizo ni pamoja na ambao wanajulikana wakiwa nchini China na Afrika Kusini.
0 comments:
Post a Comment