BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

USILOLIJUA JUU YA VALENTINE DAY (SIKU YA WAPENDANAO) NDIO HII


Mt, Valentino, Padri February 14
Mtakatifu Valentino alikuwa ni padre wa Roma (Italia) ambaye aliishi kwa kuishuhudia imani ya kikristo kati ya mwaka 197 na 273. Kanisa linamtambua kuwa ni shahidi wa imani kwa kuwa alitoa uhai wake kwa kuilinda, kuitetea na kuitangaza imani ya kikristo. 


Lakini pia Mtakatifu Valentino anajulikana duniani kote kuwa ni mtakatifu wa wapendanao. Kwa hiyo utakatifu wake katika historia ya Kanisa na umaarufu wake duniani kote ni mambo mawili yanayojikitika katika jambo moja la msingi kwa maisha ya mtu wa dini yeyote na mahali popote; jambo hilo ni imani. 

Valentino aliongoka katika ujana wake na kubatizwa mnamo mwaka 197 na baadae akawa Padri kwa kuiishi imani ya kikristo mpaka mwaka 273 alipouawa kwa ajili ya kuitetea imani. Imani hiyo ya kikristo aliishi si tu kwa maneno bali pia kwa vitendo kwani wakati ule kuwa mkristo ilikuwa ni jambo gumu sana. 

Ugumu huo ulitokana na ukweli kwamba watawala wa Kirumi wa nyakati hizo walikuwa bado hawajaipokea imani ya kikristo. Valentino aliishi imani ya kikristo nyakati za mfalme Claudio ambaye mara kadhaa alimtesa na kumfunga gerezani na baadae aliuawa kwa amri ya mfalme Aureliano. 

Utakatifu wake Mtakatifu Valentino anatambulika na wengi duniani pote kwa sababu ya upendo wake kwa watu. Tabia yake ya kupenda watu ilijikita katika imani yake kwa Neno la Yesu, “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. 


Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yoh. 15:12-13). Mtakatifu Valentino alitumia muda wake mwingi kuwasaidia watu wa ndoa na vijana wachumba kwa kuwafundisha juu ya upendo. Aliwafundisha kuwa upendo ni fadhila kuu ya kikristo na kiutu, kwa hiyo alisisitiza kuwa upendo ni kielelezo cha imani na utu. 

Watu wa ndoa aliwafundisha kuwa upendo wao hujionesha katika mambo makuu mawili: uaminifu na umoja. Uaminifu wa viapo vya ndoa katika kupendana na kuheshimiana siku zote na kwa hali zote. Umoja katika kutambua kuwa ndoa ni kati ya mume mmoja na mke mmoja. 

Mtakatifu Valentino aliisha nyakati ambazo ndoa za mume mmoja na wake wengi zilikuwa ni kama jambo la kawaida. Wanawake walinyimwa upendo ndani ya ndoa zao na wakawa wanyonge mbele za waume zao. 

Yeye alikemea jambo hilo bila kujali mtu yeyote; watawala kwa mfano, walikuwa pia na tabia hiyo ya kukosa uaminifu kwa ndoa zao. Polepole watu wengi walianza kujirekebisha na upendo ukaanza kurudi ndani ya ndoa. 

Hata hivyo mfalme Claudio alimchukia Valentino na kumfunga gerezani. 


Wachumba aliwafundisha kuwa upendo wa kweli wa wapendanao hujidhihirisha katika kufunga ndoa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hivyo basi aliwakemea bila woga vijana wengi waliokuwa wanaishi maisha ya unyumba. Vijana wengi waliongoka na kufunga ndoa takatifu kanisani. Jambo hili pia lilimkera sana mfalme kuona kwamba watu wengi wanaingia katika dini ya kikristo. 

Pia aliwatetea vijana waliokuwa jeshini ambao walikatazwa kwa sheria ya mfalme wasifunge ndoa. Sheria hiyo iliwanyima wanajeshi maisha ya ndoa kwa imani kuwa askari hodari hawatakiwi kuishi maisha ya ndoa. Mtakatifu Valentino alipigania haki ya hao askari na kuwataka watawala waibatirishe sheria hiyo potovu.

Katika kuwasaidia watu wautambue utakatifu wa ndoa, Mtakatifu Valentino alifanikiwa kuwafungisha ndoa wachumba wawili (mmoja mkristo na mwingine alikuwa mpagani) ambao wazazi wao walikuwa wamewawekea vikwazo. Mchumba wa kike ambaye ni mkristo alikuwa mgonjwa na yule wa kiume ambaye ni mpagani alikuwa ni askari. 


Askari aliwaambie eti si vizuri aoe kwani maisha yake yamo daima hatarini na hasa wakati wa vita na hivyo atamwacha mkewe kuwa mjane. Na yule binti pia aliambiwa asiolewe eti kwa kuwa yeye ni mdhaifu na hivyo anaugua mara nyingi itakuwa ni vigumu kwake kutimiza wajibu wake wa nyumbani. 

Mtakatifu Valentino aliingilia kati na kuwafundisha wazazi wa vijana hao kuwa upendo hauna mipaka wala ubaguzi. Na pia wale wachumba akawafundisha kuwa katika ndoa ni lazima kupendana katika taabu na raha, afya na magonjwa, na kuheshimiana daima. 

Mtakatifu Valentino alifaulu kumbatiza askari na kumfungisha ndoa kwa yule binti ambaye alikuwa taabani mgonjwa kitandani. Ushahidi wake Mnamo mwaka 269 mfalme Aureliano alimkataza rasmi Valentino kuhubiri, kuwaongoa na kuwafungisha ndoa takatifu. 


Mtakatifu Valentino aliendelea kumshuhudia Kristo bila woga na akawa tayari kwa lolote ila tu upendo wa Kristo uhubiriwe. Mwaka 270 mfalme alimhukumu Valentino adhabu ya kufungwa gerezani kwa miaka mitatu. 

Na mnamo 14 Februari 273 kwaamri ya mfalme Valentino aliuawa kwa kukatwa kichwa. Hukumu hiyo ni kwa sababu mtakatifu Valentino alikuwa amewabatiza watu wengi na kuwafungisha ndoa takatifu ya mume mmoja na mke mmoja wanaotakiwa kudumu katika uaminifu, upendo na umoja. 


Katika miaka mitatu aliyofungwa gerezani kabla ya kukatwa kichwa, mtakatifu Valentino alifaulu kumhubiria mkuu wa gereza na kumwongoa. Na pia binti mmoja wa mkuu wa gereza ambaye alikuwa kipofu alifanyiwa muujiza na mtakatifu Valentino akapata kuona. Mkuu wa gereza alibatizwa yeye na familia yake na akafunga ndoa takatifu.

Na tarehe 14 mwezi Februari, mwaka 273 ambayo ndiyo siku ya kuuwawa kwake mtakatifu Valentino aliwaandikia barua watu wengi aliowafungisha ndoa akawasihi wadumu katika upendo, uaminifu na umoja. Kila barua aliyoiandika mwishoni iliandikwa “ndimi Valentino wako.” 

Maneno hayo yakawa ni kielelezo cha upendo wa mtakatifu Valentino kwa watu wote kuwa yeye aliishi na kufa kwa ajili ya kuwapenda watu wote kama kristo alivyosema: “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yoh. 15:12-13).

Urithi wake Mtakatifu Valentino ametuachia urithi mkubwa wa imani. Mtakatifu Valentino anatufundisha kuwa fadhira ya upendo ni kielelezo cha imani. Mtu yeyote mwenye imani humpenda Mungu na huwapenda wenzake. Kipimo cha imani na kipimo cha utu ni upendo. 


Dunia inahitaji sana upendo ili mambo mengine mazuri yawezekane. Mtakatifu Valentino alitambua kuwa watu wa familia wanapopendana jamii yote itapendana na kuishi kwa amani.Anatufundisha kuwa upendo huanzia nyumbani, yaani kati ya wanafamilia. 

Ndiyo maana aliwataka watu wa ndoa wapendane katika misingi ya imani na wafunge ndoa takatifu. Leo hii watu wengi duniani pote wanaikumbuka tarehe ya 14 februari kuwa ni siku ya wapendanao. Je, wanatambua kwa nini Valentino alitoa uhai wake siku hiyo? Tunatakiwa tupendane kwaupendo wenye msingi katika imani kama alivyofundisha mtakatifu Valentino.

Siku ya Mtakatifu Valentino ni siku ya wapendanao katika misingi ya imani na utu. Kwa bahati mbaya watu wengi katika maisha ya leo tunapendana katika misingi ya tamaa za kimwili na kimapato. Leo hii kuna watu wengi wa ndoa ambao wana nyumba ndogo lakini nao wanasema eti leo ni siku yao ya wapendanao. 


Ni upendo gani huo wenye nyumba kubwa na ndogo? Je, Valentino hakufa kwa kupinga jambo hilo? Vijana wengi leo wanaishi uchumba sugu bila kufunga ndoa. Lakini wao pia wanasema eti leo ni siku yao ya wapendanao. Ni upendo gani huo pasipo msingi wa imani. 

Je, valentino hakutoa uhai wake ili kuwafundisha na kuwapigania vijana wafunge ndoa takatifu? Ni ajabu kuwa siku ya Mtakatifu Valentino uovu mwingi dhidi ya upendo ndiyo hufanyika
Ni vema siku hii iwe kwa ajili ya kujikumbusha maana halisi ya upendo. 


Wakati ule Mtakatifu Valentino alikwazika sana kuona watu wanaishi pamoja bila kufunga ndoa, alikwazika kuona vijana watu wa ndoa wanakosa uaminifu katika ndoa zao. 

Na alisikitika kuona hata vijana wanakosa haki za kuuishi upendo wa ndoa. Lakini akija leo hii, mtakatifu Valentino atashindwa hata kushangaa kuona jinsi upendo ulivyogeuzwa kuwa ni starehe ya kimwili badala ya kuwa ni fadhila ya kimungu. 

Na mbaya zaidi atakutana na watu wa jinsia moja (ushoga na usagaji) wanaodai eti wanapendana na wana haki ya kufunga ndoa. Katika siku hii Mtakatifu Valentino anatukumbusha tena kuwa upendo ni fadhila ya kimungu na sio starehe ya kimwili.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: