BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CAG AWAUMBUA TFF YA RAIS JAMAL MALINZI KWA KUCHOTA FEDHA ZA UFISADI

MABILIONI ya shilingi yamebainika kuchotwa kwenye akaunti za Shirikisho la Soka (TFF) na kulipwa kwa wadau wa soka kinyume cha sheria.

Miongoni mwa watu waliopewa fedha hizo ni rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi na aliyekuwa msaidizi wake, Juma Matandika.

Wengine ni aliyekuwa katibu mkuu wa kilichokuwa Chama cha Soka (FAT sasa TFF), Michael Wambura na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Ayubu Nyenzi.

Nipashe imebaini malipo hayo mbali na kutofuata matakwa ya Kanuni za Fedha za TFF, pia yalifanyika bila wahusika kukatwa kodi ya serikali, kinyume cha Sheria ya Kodi ya Mwaka 2008.

Alipotafutwa na Nipashe jana asubuhi kuzungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, alisema taratibu zao za kiutendaji zinazuia kuweka hadharani majina ya watu na taasisi zinazowadai na wanazozidai.

"Leo (jana) si siku ya kazi, lakini hata ingekuwa siku ya kazi, nisingeyazungumzia masuala hayo kwa sababu taratibu zetu za kiutendaji haziruhusu 'ku-disclose' (kuweka wazi) majina ya tunaowadai na wanaotudai," alisema Mwesigwa.

Rais wa TFF (Malinzi) hivi karibuni aliulizwa kuhusu kadhia hiyo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo alikanusha na kuihusisha na fitna za mchakato wa uchaguzi ujao wa shirikisho hilo.

“Hilo jambo siyo kama sijalisikia, nimelisikia na hizo hesabu zinazosemwa nimezisikia na yanayoendelea nayajua hayanipiti," alisema

“Naomba tusisahau kwamba tunaingia kwenye uchaguzi wa TFF mwezi wa 10 (Oktoba) na naomba nitumie fursa hii kuwaomba wale wote (ambao) kwa namna moja au nyingine watapenda kushiriki uchaguzi huo kama wagombea, watulie.

"TFF ina uongozi uliopo madarakani na unatimiza majukumu yake kwa mujibu wa katiba. Muda utafika wa wao kuchukua fomu na kugombea, watachukua fomu na watatendewa haki."

Hata hivyo, Nipashe imebaini kuwa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za fedha za TFF iliyotolewa Januari 19, mwaka jana na Kampuni ya Ukaguzi ya TAC, inaanika ufisadi wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na watendaji wa TFF kwa kushirikiana na wadau wa soka nchini.

Nipashe imebaini kuwa, mkutano mkuu wa wanachama wa TFF uliofanyika Desemba 2011 uliidhinisha Kampuni ya Ukaguzi ya TAC kuwa mkaguzi wa hesabu za shirikisho kwa miaka mitano kuanzia mwaka ulioishia Desemba 31, 2011.

Ripoti ya ukaguzi wa kampuni hiyo inaonesha kuwa, katika kipindi cha kuanzia Agosti 15, 2014 hadi Septemba 30, 2015, TFF ililipa jumla ya Sh. milioni 274.072 kwa Wambura na kampuni za Punchlines (T) Ltd na Artriums Dar Hotel Ltd bila kuwa na nyaraka stahiki.

Pia, ripoti ya ukaguzi maalum wa fedha za udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa timu ya taifa (Taifa Stars) iliyotolewa Oktoba 2, 2014, inabainisha matumizi mabaya ya mabilioni ya shilingi miongoni mwa baadhi ya watendaji wa TFF.

Katika ripoti hiyo inaelezwa kuwa, kuanzia Novemba 13, 2013 hadi Februari 15, 2014, jumla ya dola za Marekani 315,577 (sawa na sh. milioni 688.368) zilichotwa kwenye akaunti ya fedha za udhamini wa TBL kwa Taifa Stars na kutumika kinyume cha makubaliano yaliyomo kwenye mkataba wa shirikisho na kampuni hiyo.

Inaelezwa pia kwenye ripoti hiyo kuwa kuanzia Novemba 11, 2013 hadi Machi 11, 2014, jumla ya dola za Marekani 381,248 (Sh. milioni 831.616) zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kutumika kwa shughuli ambazo hazijaanishwa katika mkataba wa TBL na TFF.

Miongoni mwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo kutumia kinyume fedha hizo ni Malinzi, Matandika, Ali Ruvu, Nyenzi, Ally Mayay, Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara, Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen.

Ripoti ya ukaguzi wa TAC inaonesha Wambura alilipwa jumla ya Sh. milioni 67.5, Punchline (T) Ltd ililipwa Sh. milioni 147.154 na Artriums Dar Hotel Ltd ililipwa Dola za Marekani 28,027 (Sh. milioni 59.417).

Aidha, ripoti hiyo inaonesha malipo ya maelfu hayo ya Dola kwa Artrium yalifanyika siku moja ya Machi 4, 2015 kwa TFF kuandika vocha nne zenye namba 001467, 001468, 001469 na 001470, tatu zikiidhinisha malipo ya Dola 9,000 kila moja wakati moja ikiidhinisha malipo ya Dola 1,027.

Katika ripoti hiyo, inaelezwa kuwa timu ya ukaguzi ilibaini malipo kwa wadau hao wa soka yalifanyika bila idhini ya Kamati ya Utendaji ya TFF.

Pia inaelezwa kuwa malipo kwa Kampuni za Artriums Dar Hotel Ltd na Punchlines (T) Ltd yalifanyika kinyume cha taratibu yakiidhinishwa na kamati iliyoundwa na Kamati ya Utendaji ya TFF kwa lengo la kubadili muundo wa ulipaji wa shirikisho kwa kipindi kilichoishia Septemba 30, 2013.

"Malipo yalifanyika kimakosa kwa Michael Richard Wambura ambaye hakuwa analidai shirikisho zaidi ya Sh. milioni 50. Kiasi alicholipwa Michael kilitokana na mkopo wa Dola za Marekani 30,000 ambao FAT ilipewa na Kampuni ya Jack System Limited Novemba 2002," ripoti ya ukaguzi inaeleza.

Inafafanuliwa zaidi katika ripoti hiyo kuwa kiasi cha fedha kilicholipwa na TFF hakikuwamo kwenye bajeti ya shirikisho kwa mwaka huo wa fedha.


"Hapakuwa na risiti au barua kutoka kwa waliolipwa kuthibitisha kupokea malipo hayo.

"Kwa kufanya malipo hayo ambayo hayakuwamo kwenye vitabu vya fedha vya mwaka uliopita na kwenye bajeti, baadhi ya shughuli muhimu za shirikisho hazikutekelezwa kutokana na fedha zake kuchotwa na kuelekezwa kwingine," inaeleza zaidi ripoti hiyo.

Inadaiwa kwamba, kabla ya kuchotwa kwa pesa hizo, Malinzi alimwagiza Mwesigwa kumwandikia barua ya kwenda likizo kwa lazima aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha wa TFF, Edgar Masoud (alifariki dunia Machi 27, mwaka huu) kisha kuajiri mkurugenzi mpya na kumkabidhi jukumu la kusaini hundi za malipo na ndani ya kipindi kifupi kulibainika kuchotwa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti za shirikisho.

Baada ya likizo yake kumalizika na kurejea ofisini, katikati ya Agosti 2016, Masoud alipewa barua ya kuachishwa kazi, ripoti inasema.

Malinzi pia anadaiwa ndiye aliyetoa maelekezo ya kulipwa kwa Michael Wambura Sh. milioni 67 ambaye deni lake dhidi ya TFF lilikuwa limeshafutwa tangu uongozi wa awamu ya kwanza chini ya Leodegar Tenga, baada ya Kamati ya Utendaji ya wakati huo kukataa madai hayo na kufikiwa kwa mwafaka wa kutolipwa.

WADAIWA SUGU TFF
Wakati Wambura akilipwa Sh. milioni 67.5 kwa madai ya kwamba anaidai TFF, Nipashe imebaini kiongozi huyo wa zamani wa FAT ni miongoni mwa wadaiwa 18 wa muda mrefu wa shirikisho hilo ambao kwa pamoja wanatakiwa kulilipa Sh. milioni 301.394.

Ripoti ya ukaguzi inaonesha Wambura anadaiwa Sh. milioni 50.828 na shirikisho hilo.

Wadaiwa wengine wa TFF waliotajwa katika ripoti hiyo ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh. milioni 157.408, Klabu ya Yanga Sh. milioni 62.9, Creastus Ruta Sh. milioni 10.781 na Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Sh. milioni 8.213.

Wengine ni Jumbe Magati Sh. milioni 1.954, Florian Kaijage Sh. milioni 1.88, Simba Technology Sh. milioni 1.5, Asheri Gasabile Sh. milioni 1.408, Adam Brown Sh. milioni 1.093, Ramadhani Kilemile Sh. 900,000, Chama cha Soka Wilaya ya Ilala (IDFA) Sh. 880,000 na Silas Mwakibinga Sh. 875,770.

Pia wamo katibu mkuu wa zamani wa TFF, Fredrick Mwakalebela Sh. 468,000, Ahmed Naheka Sh. 414,652, Edith Ruben Sh. 295,000, Glory Mwenda Sh. 150,000 na Raymond Wawa Sh. 132,252.

Ripoti hiyo ya ukaguzi inaonesha kuwa, wadau hao wa soka wanadaiwa kiasi hicho cha fedha na TFF kwa kipindi cha kuanzia miaka mitatu hadi nane.

MAMILIONI COCA-COLA
Imebainika pia baadhi ya watendaji wa TFF na wadau wa soka nchini walilipwa jumla ya Sh. milioni 287.843 na shirikisho hilo pasi na uthibitisho wa masurufu (imprest).

Fedha hizo zilitolewa na wadhamini wa michuano ya soka la vijana ya Copa Coca-Cola, Uhai na Airtel.

Nipashe imebaini malipo hayo yalifanyika kinyume cha Ibara ya 112 ya Kanuni za Fedha za TFF na Ibara ya 54(2) cha kanuni hizo, kinachozuia masurufu kutumika bila uthibitisho wa kiuhasibu.

Miongoni mwa waliotajwa katika ripoti ya ukaguzi wa TAC kutumia masurufu hayo bila kuwa na nyaraka za uthibitisho wa kiuhasibu wakidai kufanikisha michuano ya Copa Coca-Cola ni Nyenzi aliyepewa na TFF Sh. milioni 2.02, Matandika Sh. milioni tano na mwingine aliyetajwa kwa jina moja la Mgoi Sh. milioni 1.7.

Ripoti hiyo pia inabainisha kuwa masurufu ya jumla ya Sh. milioni 63.307 yalitumika kinyume cha taratibu kwa madai ya kuwezesha mikutano ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) iliyofanyika mwaka 2014.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mikutano hiyo ilifanyika Machi 10, Aprili 29, Mei 2, Agosti 14, 15, 20, 21 na Desemba 22, mwaka huo.

Ripoti hiyo inasema menejimenti ya TFF bado haijathibitisha matumizi ya jumla ya Sh. milioni 351.149, zilizotokana na masurufu ya michuano ya vijana na mikutano ya FIFA, ambayo watendaji wakuu wa shirikisho hilo wanadaiwa kuyatumia kugharamia usafiri, malazi na posho.

Ukaguzi huo pia umebaini kuwapo na tofauti kati ya taarifa za fedha zilizopo kwenye vitabu vya TFF na stakabadhi za benki.

Taarifa za akaunti ya TFF tawi la NBC Samora na Stanbic zinaonesha kuwapo kwa tofauti ya Sh. milioni 33.805 kati ya stakabadhi za benki na vitabu vya fedha vya shirikisho huku watendaji wa TFF wakishindwa kuieleza timu ya ukaguzi sababu za tofauti hiyo.

KUHAMIA MJINI
Ripoti ya ukaguzi pia inaonesha TFF ililipa dola 14,580 (Sh. milioni 42.458) mwaka 2014, sawa na Dola 1,215 kwa mwezi, ikiwa ni gharama ya Dola 16 kwa kila mita mraba ya malipo ya pango, umeme, maegesho ya magari ya maofisa na watendaji wake kwenye jengo la Mfuko wa Pensheni wa PSPF.

Ukaguzi huo pia umebaini PSPF walipewa zabuni hiyo bila ushindani na uamuzi huo haukuwamo kwenye Mpango wa Manunuzi wa TFF Mwaka 2014 na hivyo haukutengewa fungu kwa mujibu wa Kanuni za Fedha za shirikisho.

"TFF haikuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2011 wakati inatoa zabuni kwa mpangishaji (PSPF). Hatua hii huenda imesababisha kutolewa kwa zabuni kwa mtoa huduma ambaye tozo zake ni kubwa kulinganisha na malipo ya kila mita mraba yaliyoidhinishwa," inaeleza ripoti hiyo.

Rais wa TFF, Malinzi alitangaza kuzihamishia Posta jijini Dar es Salaam ofisi za makao makuu ya TFF muda mfupi baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na mtangulizi wake Tenga Novemba 2, 2013.

Hata hivyo, ujumbe wa FIFA uliotua nchini Agosti 2014 ukiongozwa na Meneja Miradi Anayeshughulikia Programu za Afrika, Zelkifli Ngoufonja, ulieleza kutofuraishwa na uamuzi huo na kuuagiza uongozi wa TFF kurejea kwenye majengo ya makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo Karume jijini.

MALIPO YENYE SHAKA
Ripoti ya ukaguzi inaeleza kuwa timu ya ukaguzi ilitilia shaka malipo kwa Evarist Majuto Maganga aliyepewa na TFF hundi namba 000185 Julai 17, 2014 kwa madai ya kutoa huduma ya Sh. milioni 48.525 kwa shirikisho hilo.

Aidha, Innocent Melleck Shirima alilipwa Sh. milioni 3.143 kupitia hundi namba 000036 Februari 6, 2014 kwa kuandaa mkutano wa waandishi wa habari (press conference), kuadhimisha siku 100 za uongozi mpya (wa Malinzi) madarakani.

Pia kuna malipo ya Dola za Marekani 51,043 (sawa Sh. milioni 112.55) yaliyofanywa na TFF kupitia hundi namba 239160 (Dola 35,280) na 239206 (Dola 15,763) kugharamia tiketi za ndege ambazo waliozitumia hawajatajwa kwenye ripoti, hata hivyo.

"Tunapendekeza kwamba, katika siku zijazo, malipo yafanyike kwa kuzingatia uwapo wa nyaraka za uthibitisho wa malipo na ankara za madai ya kodi (Tax invoices)," inaeleza zaidi ripoti hiyo.

UKWEPAJI KODI MIL.99/-
Ukaguzi umeibaini TFF haikukata Kodi ya Lipa Kadri Unavyopata (PAYE) ilipomlipa Dola za Marekani 90,000 (Sh. milioni 189) aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen iliyeamua kumtimua mwaka 2014.

"Ibara ya 59 ya Sheria ya Kodi ya Mwaka 2008 inawataka waajiri kuwakata PAYE wafanyakazi wao," inaelezwa katika ripoti hiyo.

"Malipo ya Sh. milioni 78.814 yalifanyika kupitia vocha namba 1086 na hundi namba 0607 Machi 3, 2014 na mengine ya Sh. milioni 63.68 yaliyofanyika kupitia vocha namba 1458 na hundi namba 0059 Aprili 16, 2014 hivyo kufanya malipo ya jumla ya Sh. milioni 189 ambayo hata hivyo, hayamo kwenye vitabu vya fedha za TFF.

"Pia tulibaini kodi ya PAYE ya Sh. milioni 42.636 ya mwaka 2014 pamoja na ya mwaka 2015 ambayo ni Sh. milioni 56.588 hazijalipwa kwa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) na kiasi hicho cha kodi (Sh. milioni 99.224) hakijawekwa kwenye vitabu vya taarifa za fedha za TFF.

"Pia Sh. milioni 5.937 ambazo zilipaswa kulipwa na TFF kwa TRA kutokana na makato ya asilimia tano ya huduma mbalimbali zilizotolewa na washirika wa TFF, hazijalipwa kwa TRA na hazijawekwa kwenye taarifa za fedha za shirikisho."

TRA, TAKUKURU
Alipotafutwa na Nipashe mwishoni mwa wiki kuzungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema maofisa wa mamlaka hiyo watalifuatilia kulingana na taarifa iliyotolewa.

Kadhalika, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Makao Makuu, Mussa Misalaba alisema wanazifanyia kazi ripoti za ukaguzi zilizotolewa kuhusu hesabu za fedha za TFF. "Tunalijua hilo suala na liko mikononi mwetu," alisema Misalaba.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: