ABIRIA zaidi ya 800 waliokuwa wakisafiri kutokea Dar es Salaam kuelekea Tabora kwa kutumia usafiri wa treni ya abiria, wamejikuta wakishindwa kuendelea na safari yao kwa muda wa saa 11, baada ya treni waliyokuwa wakiitumia kupata ajali katika eneo la Mazimbu, nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.
Imeelezwa kwamba, ajali hiyo ilitokea majira ya saa tano usiku wa kuamkia jana, kutokana na kuharibiwa kwa miundombinu ya reli katika Daraja la Tingetinge na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Wakizungumza jana na MTANZANIA Jumapili, baadhi ya mashuhuda waliokuwa katika eneo ilipotokea ajali hiyo wamesema uchakavu wa reli na madaraja katika kipande cha reli ya kati inayopita mkoani humo ndio chanzo kikubwa cha ajali nyingi zinazotokea mara kwa mara.
"Uchakavu wa miundombinu ndio chanzo cha ajali, tunaiomba Serikali kuacha kujali kukusanya pesa tu, ifanyie matengenezo reli hii, ni ya zamani sana," alisema Charles Onyango, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo.
Kwa upande wao, baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri katika treni hiyo wamedai kuwa, kusitishwa kwa safari hiyo kumewaathiri kwa kiasi kikubwa, kwani walikuwa hawana pesa za kujikimu.
"Ajali hii kimsingi inatutesa sisi kwa kuwa wengi tunasafiri kwa bajeti na ndiyo maana tumepanda huku kwenye unafuu,” alisema Juma Hassani.
Mkurugenzi wa Usafirishaji TRL, Rashid Ngwani, amesema wanafanya mawasiliano na makao makuu ya TRL kutafuta njia mbadala ya kuwasafirisha abiria waliokumbwa na ajali hiyo kutoka stesheni ya Morogoro.
Katika ajali hiyo, abiria wote waliweza kutoka salama, ingawa huduma ya usafirishaji wa abiria kutoka Morogoro kuelekea Kilosa kwa kutumia reli ya kati imesitishwa kwa muda mpaka ukarabati wa eneo ilikotokea ajali hiyo utakapofanyika.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ MAFURIKO YALIVYO WAHENYESHA ABIRIA ZAIDI YA 800 BAADA YA MABEHEWA YA TRENI KUACHA NJIA MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment