BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWANAFUNZI AKAMATWA NA POLISI AKIUZA BASTOLA NA RISASI 13 DAR ES SALAAM


Bastola

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia mwanafunzi wa Chuo cha St Joseph, Lewis Mbise (23) akituhumiwa kukutwa na bastola moja aina ya Luger cz 100 yenye namba C 4122 ikiwa na risasi 13 ndani ya magazine, mali ya baba yake kwa lengo la kuiuza.

Pia linawashikilia walimu wawili na mwanafunzi kwa tuhuma za kuvujisha mtihani wa Kidato cha Sita unaoendelea. Akizungumzia tukio la mwanafunzi kukamatwa na bastola, Kamanda wa kanda hiyo, Kamishna Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba mwanafunzi huyo alisema alikamatwa Mei 5 maeneo ya Mbezi Magari Saba katika Manispaa ya Ubungo baada ya kupata taarifa kuwa kuna kijana anauza silaha.

Kamanda Sirro alisema baada ya taarifa hizo, jeshi hilo lilifuatilia na kumpata kijana huyo na katika mahojiano, alikiri kuwa bastola hiyo aliiba nyumbani kwa baba yake mzazi pamoja na fedha kiasi cha Sh 800,000. “Ni watu wengi wanatumia silaha, lakini hawatunzi silaha ni kitu ambacho kinatakiwa kutunzwa.

Tayari nimeagiza baba wa kijana huyu akamatwe kwa hatua zaidi, niwasihi na wengine wanaotumia silaha kuhakikisha silaha hizo zinahifadhiwa vizuri,” alieleza Kamanda Sirro. Alisema upelelezi unaendelea kufanyika ili kubaini lengo la mtuhumiwa kuiba silaha hiyo ikiwamo kujua kama kuna taarifa ya kupotea kwa silaha hiyo kabla haijapatikana.

Sirro alisema watuhumiwa waliokamatwa kwa tuhuma za kuvujisha mitihani ni walimu Musa Elius (35) na Innocent Mrutu (33) mkazi wa Kibamba na mwanafunzi Ritha Mosha.

Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao walinaswa Mei 6, maeneo ya Chang’ombe baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Ofisa wa Baraza la Mitihani la Taifa, Aron Mweteni kuwa Mei 5, katika Shule ya Sekondari Chang’ombe alimkuta Elius akiingia darasani na mwanafunzi Mosha ambaye ni mtahiniwa wa mtihani wa Kidato cha Sita unaoendelea, wakiwa na karatasi yenye maswali na majibu ya somo la Kemia kwa Vitendo.

Alisema baada ya kuwakamata na kuwatilia shaka, ufuatiliaji wa awali ulifanyika kupitia Baraza la Mitihani la Taifa na kubainika kuwa swali hilo ni miongoni mwa maswali ya mitihani ya Kidato cha Sita unaofanyika mwaka huu.

Mitihani hiyo ilianza Mei 2, mwaka huu na itakamilika Mei 19, mwaka huu. Kamanda Sirro alisema watuhumiwa wote wanaendelea na mahojiano na upelelezi utakapokamilika watachukulia hatua za kisheria.habarileo
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: