SAFARI YA MATUMAINI KIBAO KWA WANAFUNZI WATATU MAJERUHI, AJALI ILIYOUA WENZAO 33 KUELEKEA KATIKA MATIBABU MAREKANI
Majeruhi wa ajali ya gari la Shule ya Msingi ya Lucky Vincent ya Arusha wakiwa na wazazi wao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA), kabla ya kusafirishwa kwenda Marekani kwa matibabu.
NI safari ya matumaini kwa wazazi, wataalamu wa afya, ndugu, jamaa na Watanzania wote, ya wanafunzi watatu majeruhi wa ajali iliyosababisha vifo vya watu 35 wakiwemo wanafunzi, walimu na dereva wa shule ya Lucky Vicent ya Mei 6 mwaka huu.
Watoto hao watatu; Doren Mshana, Wilson Tarimo na Sadya Awadh wanakwenda nchini Marekani kwa safari ya saa zaidi ya 20 angani wakiwa na ndege ya Shirika la Mfuko wa Msamaria la Marekani linaloendeshwa na Frankline Graham, mtoto wa Muhibiri maarufu duniani, Bill Graham.
Ndege hiyo aina ya DC 8 ambayo imewachukua watoto hao jana saa 05:45 asubuhi, inatarajia kufika Uwanja wa ndege wa Charllotte, Jimbo la North Calorina kisha watoto hao kupanda ndege nyingine ndogo hadi jimbo la IOWA kwa ajili ya matibabu yao katika hospitali ya Mercy jijini Sioux ambayo ni miongoni mwa hospitali 30 bora nchini Marekani.
Safari hiyo inahusisha wazazi (mama) wa watoto hao, muuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, Siniphorosa Silalye na Daktari Bingwa wa Mifupa, Dk Elias Mashalah.
Mzazi wa mmoja wa wanafunzi hao watatu majeruhi, Elibariki Mshana ambaye mtoto wake ni Doren aliishukuru Serikali na wasamaria waliowezesha kufanikisha safari hiyo na kutaka watu wasihukumu bali wajue ni lazima kushukuru kwa kila jambo maana Mungu ndiye anayejua siku za mwanadamu za kuishi.
Elibariki alitoa kauli hiyo jana wakati akimsindikiza mwanaye pamoja na watoto wengine wawili; Wilson na Sadya, kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) tayari kwa safari kuelekea Marekani kwa matibabu zaidi.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari waliofika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jana kisha kwenda pamoja KIA, Elibariki alisema watu wanahukumu juu ya tukio hilo lakini jambo la msingi ni kumshukuru Mungu kwa kila jambo.
Alisema anamshukuru Mungu pia kwa kutendamuujiza kwa watoto hao (watatu) kunusurika na ana imani kubwa watapona. “Sitasita kumshukuru Mungu kwani mwanangu ametoka kwenye tanuri la mauti na sasa yu hai sifa na utukufu ni kwake eeh Bwana maana mawazo ya binadamu si kama ya Mungu,” alisema Elibariki.
Alisisitiza kuwa ingawa mtoto wake, Doren amevunjika mkono wa kulia na mguu kisha kuvunjika taya lakini Mungu ni mwema na anaishukuru serikali kwa jitihada zake katika kuokoa maisha ya watoto hao sanjari na timu nzima ya madaktari ambao wamepelekea watoto wao kuwa salama kutoka Marekani na Tanzania.
Naye baba mzazi wa Wilson, Godfrey Tarimo, alisema mtoto wake anaendelea vizuri na anaamini atapona ingawa ameumia sehemu mbalimbali za mwili wake ila moyoni anaamini kuwa mtoto wake amekwenda akiwa kwenye kitanda ila siku moja atarudi na kumpokea akiwa anatembea mwenyewe na kumwonyesha tabasamu kama aliyokuwa nayo awali kabla ya kupata ajali.
“Najua mtoto wangu anaondoka leo na mama yake kwenda kwenye matibabu lakini naamini moyoni kuwa siku atakayorudi nitakuja kumpokea akiwa na afya njema pamoja na tabasamu kama alilonionyesha kabla ya kupata kwake ajali”.
Naishukuru serikali yangu, watu mbalimbali pamoja na shirika hili lililojitolea kuwasaidia watoto hawa maana Mungu ni mwema sina cha kusema zaidi namshukuru kwa kila jambo hadi leo hii mwanangu yu hai hakika Mungu atabaki kuwa Mungu tu.
Kwa upande wake, mzazi wa Sadya, Awadh Abdallah alisema anawaombea watoto hao wafike salama na wapate matibabu mazuri kisha siku watakaporudi waweze kuwapokea wakiwa na afya njema.
Alisema siku ya kwanza walipopata ajali, Mei 6, katika kilima cha Rhotia, Karatu, mwaka huu hali zao zilikuwa mbaya lakini akaishukuru timu nzima ya madaktari kwa moyo wa pekee kwa watoto wetu kwani hali zao ni nzuri hivi sasa.
Awali ndugu, jamaa na marafiki walikusanyika Hospitali ya Mount Meru saa 1:00 asubuhi kwa ajili ya kuagana huku wengine wakilia na wengine wakiwaombea watoto hao warudi salama huku wazazi wa watoto hao ambao ni akinamama watatu wakilia pale wanapowaacha watoto na familia zao huku wakiwa na wazo moja tu la kuwauguza watoto wao waliojeruhiwa na hatimaye warudi katika hali zao za kawaida.
Mama mzazi wa Doren, Grace Elibariki, alisema anashukuru Mungu kwa niaba ya wazazi wenzake wanaokwenda nchini Marekani na wanaamini kwa pamoja watoto wao watarudi wakiwa wazima na kutembea wenyewe.
“Mungu ni mwema kwetu kwani sisi ni kinanani hadi tuwe hapa basi hatuna jinsi tumeyapokea haya yaliyotokea na hatuna budi kushukuru kwa kila jambo ni lazima tumshukuru mungu maana yeye ndiye anayejua maisha yetu, mtuombee tufike salama watoto wetu wapate nafuu kabisa na turudi tukiwa na furaha.”
Naye Mratibu wa safari hiyo ambaye ni Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu alishukuru shirika hilo kwa kusaidia watoto hao pamoja na serikali ya Tanzania kwa kuhakikisha hati za kusafiria za watoto hao, daktari, muuguzi pamoja na wazazi wao zinapatikana kwa haraka.
Alisema ndege hiyo itakapofika nchini Marekani, Shirika hilo la Msamaria limeandaa ndege nyingine maalumu (Air Ambulance) itakayoondoka uwanjani hapo kuelekea katika Hospitali ya Mercy.
Awali mmoja kati ya wauguzi anayeambatana na watoto hao ambaye ni Muuguzi na mtaalamu wa wagonjwa mahututi na waliopata ajali kutoka Hospitali ya Mount Meru, Siniphorosa alisema anakwenda na watoto hao na ana imani siku watakayorudi watoto hao watakuwa wakitembea wenyewe huku wakiwana nyuso za furaha.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema tukio hilo lisihusishwe na masuala ya siasa huku akikemea baadhi ya watu kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii kueleza mambo waliyoyajua pia alitoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki waliokumbwa na tukio hilo.
Alisema kazi hii ni nusu ya safari, ya kwanza ilikuwa ni ya kuwahifadhi watoto waliokufa pamoja na walimu wao pamoja na dereva ambao walitangulia mbele za haki pia alishukuru shirika la Samaritan kwa msaada huo wa ndege iliyowezesha watoto hao kuondoka jana kwenda nchini Marekani.
Alitoa salamu kutoka kwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuwa anawatakia safari njema na kuishukuru serikali ya Marekani kwa kujitolea kuwapata matibabu watoto hao.
Katika hatua nyingine, Shule za Kimataifa zilizopo Arusha Shule ya Kimataifa ya Moshi (ISM), Braeban na St Costantine zimeamua kuendesha mfuko wa kusaidia uchangiaji fedha zitakazosaidia wazazi na madaktari watakuwa Marekani sanjari na kujenga kituo maalum cha wagonjwa mahututi hospitali ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) kitakachokuwa na vifaa vya kisasa zaidi kwa ajili ya kusaidia majeruhi watakaopata ajali.
Kusafirishwa kwa watoto hao kwenda Hospital ya Mecry iliyopo nchini Marekani kunatokana na jopo la madaktari waliokuwa wamemtembelea Nyalandu kuwa watu wa kwanza kutoa huduma ya kwanza siku ya ajali Mei 6 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment