BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SIRI ONGEZEKO LA BEI YA REJEREJA YA SUKARI YABAINIKA TANZANIA


CHAMA cha Wazalishaji Sukari Tanzania kimesema kupanda kwa bei ya rejareja ya bidhaa hiyo hadi kufikia Sh. 3,000 kwa kilo linatokana na mahitaji makubwa pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji.

Hata hivyo, imebainika kuwa kupanda huko kwa bei kwa sasa kumetokana na viwanda vingi kufunga viwanda kwa ajili ya maandalizi ya uzalishaji wa msimu ujao.

Katibu Mtendaji wa chama hicho, Deo Lyatto, akizungumza na Nipashe juu ya changamoto iliyoko sokoni ya kupanda kwa bei ya sukari, alisema ndani ya miaka minne kumekuwapo na ongezeko la uzalishaji lakini halitoshelezi mahitaji.

Alisema uzalishaji kwa miaka minne iliyopita umeongezeka kutoka wastani wa tani 300,000 hadi 326,909 kwa msimu wa 2016/17 kwa mwaka lakini mahitaji yamekuwa yakiongezeka.

“Kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa tani 33,763 kwa mwaka kulinganisha na msimu uliopita, lakini bado hautoshelezi mahitaji ya sukari nchini hasa Machi hadi Mei wakati viwanda vinaposimamisha uzalishaji kuruhusu matayarisho ya uzalishaji kwa msimu unaofuata kwa kufanya matengenezo,” alisema.

Pia alisema changamoto nyingine katika miezi hiyo ni mvua nyingi wakati wa uvunaji miwa na kupungua kwa kiwango cha sukari katika miwa, hivyo kusababisha changamoto kwenye soko.


Aidha, alisema kupanda kwa bei ya sukari katika soko hakuhusiani na wazalishaji bali hali ya soko kulingana na upatikanaji wa bidhaa na mahitaji kwa wakati husika.

Lyato alisema katika msimu wa mwaka 2016/17 (Mei, 2016 hadi Aprili, mwaka huu, viwanda vya sukari viliongeza uzalishaji hadi kufikia tani 326,909 ikilinganishwa na tani 293,146 kwa msimu wa mwaka 2015/16. 


Kwa sasa bei ya sukari kwa rejareja imekuwa ikiuzwa kati ya Sh. 2,600 na 3,000 kulingana na eneo wakati awali iliuzwa kati ya Sh. 1,900 na 2,200.Bei ya jumla kwa mfuko wa kilo 50 kwa sasa inauzwa kati ya Sh. 130,000 na Sh. 140,000.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: