BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SUGU APIGWA PINI KUSOMA HUTUBA YA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI DODOMA

Tokeo la picha la photos of Joseph Mbilinyi 'Sugu'
KIKAO cha Bunge jana nusura kivurugike baada ya Kiti cha Spika kuzuia kusomwa kwa baadhi ya maneno yaliyokuwamo kwenye hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mvutano ulianza baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, kumzuia Waziri Kivuli wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi 'Sugu', kusoma maneno yote yaliyomo kwenye hotuba yake kuanzia ukurasa wa sita hadi wa 10 akidai yalikiuka Kanuni za Kudumu za Bunge.

Mbali na sakata la kupotea kwa Ben Saanane, ambaye Msaidizi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Sugu alitaka kusoma maneno yanayohusu kuvamiwa kwa waandishi wa habari na wafuasi wa Prof. Ibrahim Lipumba na kukamatwa kwa waandishi wa habari kwa amri za wakuu wa wilaya, mambo ambayo Zungu alisema yanashughulikiwa na vyombo vya dola.

Dalili za hotuba hiyo kukumbana na rungu la Kiti cha Spika zilianza kuonekana mapema asubuhi wakati Zungu alipokuwa akisoma matangazo ya Bunge baada ya kipindi cha 'Maswali na Majibu' na kueleza kuwa msomaji wa hotuba hiyo atatakiwa kutosoma kuanzia ukurasa wa sita hadi wa 10 na ukurasa wa 37 hadi wa 47 wa hotuba yake kwa kuwa kurasa hizo zilikuwa na maneno yaliyodaiwa kukiuka kanuni za Bunge.

Alisema mbunge yeyote atakayeona uamuzi wa mwenyekiti huyo haukutenda haki, atatakiwa kuwasilisha
malalamiko yake kwa Katibu wa Bunge kwa kutumia Kanuni ya 5(4) cha Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016.

“Hapa tunafuata kanuni na mimi hapa ndiyo nina kadi, nina filimbi na nina jezi kabisa kwa sababu nyie huko mmevaa nguo za kawaida," alisema.

“Kwa hiyo, msemaji wa kambi ya upinzani wa wizara hii, naomba atakapokuja hapa, asisome ukurasa wa sita hadi wa 10 na asisome ukurasa wa 37 hadi wa 47,” aliagiza Zungu.

Hata hivyo, wakati Sugu akiwasilisha hotuba hiyo, alikwenda kinyume cha maelekezo ya Zungu kwa kutaka kusoma kurasa zilizopigwa marufuku kusomwa bungeni ukiwamo ukurasa uliohusu kutoweka kwa Saanane.

Kutokana na hali hiyo, Zungu alizima kipaza sauti kilichokuwa kinatumiwa na mbunge huyo na kumtaka afuate maelekezo, maagizo ambayo Mbunge huyo wa Mbeya Mjini (Chadema) hakuwa tayari kuyafuata.

“Mheshimiwa Sugu, nakuomba usisome hayo unayotaka kusoma, soma ukurasa wa 12 ambao sisi tunao hapa. Nakuomba tafadhari maana 'rulling' (uamuzi) yangu ikishatolewa, huwezi kuihoji hapa,” alisema Zungu.

Pamoja na maelekezo hayo na mengine, Sugu alikataa kuyafuata na badala yake akatilia mkazo umuhimu wa kusoma kilichokuwa kimeandikwa na kambi yake kwa kuwa ndicho wanachoamini.

Baada ya mvutano huo kushika kasi, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
(Chadema), aliomba mwongozo wa Kiti na kueleza asivyoridhishwa na utaratibu wa kuwazuia wapinzani kuwasilisha baadhi ya maoni yao.

“Kwa hiki kilichofanyika sasa hivi, kinaonyesha serikali inataka kutupangia mambo ya kuzungumza sisi wapinzani.

Lakini, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kuhusu majadiliano, mbunge ataruhusiwa kuzungumza na kama ataambiwa amekosea, aliyesema amekosea atatakiwa kuwasilisha ushahidi.

“Huu utaratibu wa serikali kuchukua hotuba za upinzani na kuamuru ni kipi kisemwe na kipi kisisemwe, hatuukubali.

“Kama ni hivyo, msemaji wa upande wa serikali ahame kwenye kiti chake na kuja kukaa hapo ili ieleweke Bunge hili linaongozwa na serikali,” alisema.

Maneno hayo ya Lissu yalimwinua kitini Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, ambaye aliitaka Kambi ya Upinzani ifuate maelekezo ya Mwenyekiti wa Bunge kwa kutosoma maneno aliyoyazuia.

“Nameelewa sana Mheshimiwa Tundu Lissu, lakini tunapofanya kazi hapa bungeni, lazima tufuate kanuni zinazotuongoza," Mhagama alisema.

“Kwa kuwa yeye ni ‘Chief Whip’ wa Upinzani, na mimi pia ni ‘Chief Whip’ wa Serikali, aelewe kwamba, aliyezuia hotuba kusomwa ni wewe Mwenyekiti wala si mimi.

“Lakini, kama kuna maeneo tunashindwa kuelewana, tunatakiwa tukae pamoja ili tuangalie namna ya kutatua tatizo lililopo kwa sababu hata Kanuni ya 64 inaeleza wazi ni nini kinatakiwa kujadiliwa hapa.”

Baada ya maelezo hayo ya Waziri Mhagama, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (Chadema), alisimama na kuomba mwongozo wa Kiti, akilalamikia utaratibu wa kambi ya upinzani kupangiwa maneno ya kusoma katika hotuba zao.

“Hata kama kuna muda watu wananyamaza, msidhani hawana maumivu. Iweje serikali ituamulie mambo ya kuzungumza?" alihoji.

“Tukitoka bungeni humu, mnaanza kutusema, tukibaki mnatunyanyasa kwa wingi wenu. Hebu tuambieni mnataka tufanye nini? Kumbukeni leo mpo na kesho hampo, acheni kutunyanyasa."

Baada ya mvutano huo, Sugu aliitwa na Zungu kwenda mbele kuendelea na uwasilishaji wa hotuba yake lakini akasusa kwa maelezo kuwa haridhishwi na maelekezo ya Mwenyekiti huyo wa Bunge.

Sugu ameungana na mawaziri kivuli wengine kadhaa kususa kuwasilisha hotuba zao katika Bunge hili la Bajeti lililoanza Aprili 4, mwaka huu. 


Miongoni mwao ni Lissu ambaye aliamua kususa na kusema 'wenye hatia waoga' alipoona anaombewa mwongozo kila anaposoma sentensi chache kwenye kitabu chache na Ally Saleh ambaye alisusa wakati wa mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: