
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila amekanusha vikali madai kwamba alishinda uchaguzi wa nchi hiyo kupitia wizi wa kura.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Kabila mwenye umri wa miaka 40 amepuuzia mbali madai kwamba matokeo hayo hayakuwa halali.
"Hakuna shaka yoyote matokeo haya ni halali,'' alisema Kabila wakati akiwambia waandishi.
Alitaja kwamba kura chache alizopata kwenye mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo ni dhihirisho kwamba mchakato wa uchaguzi ulikuwa wazi.
Amesema hajashangazwa na hatua ya Bwana Tshisekedi kujitangaza yeye ndiye Rais, lakini akasema ataendelea na kazi yake ya kuiongoza Congo, na kwamba ana imani kuwa uchumi wa nchi hiyo utakuwa kwa kiasi kikubwa katika miaka miwili au mitatu ijayo.
Vyama vya upinzani vimetangaza mipango ya kufanya maandamano baada ya kukataa ushindi wa Bwana Kabila.
Wagombea wengine wanne kwenye uchaguzi huo wamesema lazima urudiwe wakisema kulikuwa na wizi wa kura.

0 comments:
Post a Comment