TUNASIKILIZA MAZUNGUMZO YA MKUTANO WA WAFUGAJI.
SEHEMU YA AKINABABA WAFUGAJI KIJIJI CHA SIGINARI WAKIFUATILIA MATUKIO YA MKUTANO HUO
SEHEMU YA AKINAMAMA WAFUGAJI KIJIJI CHA SIGINARI WAKIFUATILIA MATUKIO YA MKUTANO HUO.
UMOJA wa wafugaji kanda ya mashariki (UWAKAMA) wameitaka serikali kusimamia kwa ukamilifu zoezi la kuhakiki idadi ya mifugo sanjari na utengaji wa ardhi ya kilimo na mifugo katika vijiji vyote vya wilaya wilaya ya Kilombero na Ulanga katika utekelezwaji wa operesheni ya kuwaondoa wafugaji na wakulima waliovamia mabonde na maeneo ya vyanzo vya maji ya Usangu na Kilombero.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili katika mikutano ya hadhara katika wilaya za Ulanga na Kilombero viongozi wa umoja huo na wafugaji walisema wanaomba watendaji wa serikali za wilaya hizo kusimamia kwa ukamilifu zoezi la kuhakiki idadi ya mifugo ikiwemo na utengaji wa ardhi yanya uwiano sawa kwa ajili ya kilimo na mifugo ndani ya vijiji vyote vya wilaya hizo ili wakati wa operesheni hiyo isilete malalamiko juu ya upotevu wa mifugo.
Mwenyekiti wa umoja huo wa UWAKAMA, Shema Jiji Ndama akizungumza na wafugaji hao katika mkutano uliofanyika kijiji cha Siginari tarafa ya Mangula wilaya ya Kilombero alisema kuwa mpango wa serikali wa kuwaondoa wakulima na wafugaji waliovamia mabonde na maeneo ya vyanzo vya maji ya Usangu, Kilombero ndani ya hifadhi ya mbuga za wanyama na maeneo ya ardhioevu ya Kilombero haina tatizo isipokuwa zoezi hilo likifanyika kwa umakini itaondoa kero mbalimbali zinazojitokeza wakati wa operesheni.
Mwenyekiti huyo anayeongoza wanachama wafugaji mikoa ya Pwani, Tanga na Morogoro alisema ni vema zoezi la kuhakiki mifugo lifanyike kwa umakini mkubwa ikiwemo kwa kuwashirikisha zaidi wafugaji na viongozi wa serikali ya vijiji ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza wakati wa operesheni zilizowahi kufanyika kwa madai ya kupotea kwa mifugo kwa njia za kupiga faini na minada katika oparesheni ya kuhamisha wafugaji iliyowahi kufanyika katika wilaya za kilosa na Kilombero.
Ndama alieleza kuwa katika operesheni hizo zilizowahi awali katika mikoa ya Morog
oro na Mbeya ikiwemo wilaya za Kilosa na Kilombero mwaka 2009 na mwaka 2006 hadi 2008 katika bonde la Ihefu wilaya ya Mbarali wafugaji wengi walidaiwa kupoteza mifugo kwa kiasi kikubwa hali iliyowafanya kurudi nyuma maendeleo yao katika sekta hiyo ya mifugo.
“Mpango wa kuhakiki mifugo sanjari na kutenga ekari za ardhi kwa ajili ya matumizi bora ya kilimo na mifugo ni mzuri sana, ila mashaka yangu ni namna zoezi la uhakiki idadi ya mifugo litakavyofanyika kwani endapo litafanyika kwa umakini hakutakuwa na upotevu wa mifugo kwa wale ambao watalazimika kuondoka katika wilaya hizo za Ulanga, Kilosa na Kilombero” alisema Ndama.
Katika mkutano mwingine uliofanyika kwenye kijiji cha Mtimbira wilaya ya Ulanga mfugaji, Michael Pawa akizungumzia juu ya operesheni zilizowahi kufanyika mwaka 2006 hadi 2008 katika bonde la Ihefu wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya na Kilosa Morogoro mwaka 2009 alisema kuwa zilikuwa na kasoro nyingi hali iliyopelekea wafugaji kupoteza mifugo mingi kutokana na madai ya usimamizi mbovu wakati wa operesheni hizo.
Pawa aliongeza kuwa serikali inabidi iwe makini katika zoezi la kuhakiki idadi ya mifugo katika wilaya hizo ili kuepuka malalamiko yaliyowahi kutokea kwa baadhi ya wasimamizi wa operesheni hasa watendaji wa halmashauri za wilaya wamekuwa na tabia ya kupindisha sheria na kutaifisha mifugo ya wafugaji.
“Nakubaliana na kauli ya serikali ya kuwa mifugo inaharibu mazingira ila kwa wakati mwingine imekuwa ikifumbia macho uharibifu unaofanywa na sekta nyingine ikiwemo ya kilimo cha mashamba makubwa ya mitiki ndani ya wilaya za Ulanga na Kilombero” alisema Pawa.
Mkuu wa wilaya ya Ulanga ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa wilaya Kilombero, Francis Miti alisema kuwa kwa sasa halmashauri zote za Ulanga na Kilombero zipo katika mchangato wa kuhakiki idadi ya mifugo na kutenga ardhi kwa aliji ya matumizi bora ya kilimo na mifugo katika vijiji vyote vya wilaya hizo mbili.
Miti alisema kuwa mpango huo wa sasa wa kuanza kuhakiki idadi ya mifugo na zoezi la kutenga ekari za ardhi ambayo imeaanishwa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi ndani ya kijiji kwa ajili kutenga maeneo ya mifugo na kilimo.
Mpango huo wa uhamishwaji wa mifugo unatarajiwa kuanza Agosti 30 mwaka huu mkoani Morogoro baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhakiki mifugo kukamilika.
0 comments:
Post a Comment