Kundi la waasi la M23 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo,
linaloshutumiwa kuzusha vurugu mashariki mwa nchi hiyo, limesema
limebadili jina la tawi lake la kijeshi na linajiandaa kuzima
mashambulio mapya dhidi yake.
Kwa mujibu wa Kiongozi wa kundi hilo Jean-marie Runiga, sasa tawi la
kijeshi la kundi hilo litajulikana kama Jeshi la Kimapinduzi la Kongo
(ARC).
Katika mahojiano na mwandishi wetu wa Goma, Runiga pia amesema
kamanda wa jeshi hilo Kanali Makenga Sultani amepandishwa cheo kuwa
Jenerali.
Jumuiya za haki za binaadamu zinalishutumu kundi la M23 kwa kuwabaka
wanawake na wasichana pamoja na kufanya mauaji wakati likipigana na
jeshi la serikali.
M23 iliundwa mwezi Mei na wapiganaji wa zamani katika
kundi la waasi wa Kitutsi ambao walijumuishwa katika jeshi la taifa,
kutokana na mkataba wa amani wa 2008.
Waasi hao wanadai matakwa yao
hayakutekelezwa.
Machafuko mapya mashariki mwa Kongo yamewafanya raia wengi kuyahama makaazi yao.
Hatua hiyo ya waasi wa M23 hata hivyo imekuja siku moja baada ya
Kiongozi wake Runiga kusema kwamba huenda mapigano yakaanza tena
karibuni ikiwa serikali itakataa kuzungumza na kundi hilo.
Nchi jirani ya Rwanda imekuwa ikishutumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa
M23 , shutuma ambazo viongozi wa Rwanda wamezikanusha vikali.
Kwa upande mwingine baada ya ripoti ya tume ya wataalamu wa Umoja wa
mataifa kumhusisha moja kwa moja waziri wa ulinzi wa Rwanda Jenerali
James Kabarebe kuwa ndiye mwenye kuliamrisha kundi hilo , hivi karibuni
ripoti nyingine ya Umoja huo ikaitaja pia Uganda.
Ripoti yake ilisema maafisa wa ngazi ya juu wa Uganda wameipa M23
wanajeshi na silaha pamoja na msaada wa kiufundi. Ripoti hiyo pia
imeituhumu Uganda kutoa ushauri wa kisiasa kwa kundi hilo na
kulirahisishia mahusiano ya kigeni.
Uganda imekanusha kuhusika na harakati za M23. Karibu watu laki tano
wamelazimika kuyahama makaazi yao kwa sababu ya harakati za kijeshi za
waasi hao, mashariki mwa Kongo.

0 comments:
Post a Comment