Mwandishi wa habari katika jimbo lililojitenga na
Somalia, Somaliland, ameuawa na watu waliokuwa wamejihami alipokuwa
anarejea nyumbani kutoka kazini.
Ahmed Farah Ilyas alikuwa mwandishi katika eneo
Las Anod, mji ambao umekumbwa na msukosuko akifanyia kazi kampuni ya
Somalia ya Universal TV.
Kabla ya kuuwawa kwake, Farah alikuwa anafuatilia taarifa ya mlipuko
wa mabomu ya ardhini ambayo serikali imelaumu Al Shabaab kulifanya.
Ilyas ni mwandishi habari wa kumi na sita kuuawa nchini Somalia mwaka huu.
Tangu kuong'olewa mamlakani kwa Rais Siad Barre
mwaka 1991, Somalia daima imeshuhudia wanamgambo wa Somalia wakipigania
udhibiti wa Somalia.
Somaliland ilijitangazia uhuru wake baada ya kung'olewa kwa Barre na imekuwa salama ikilinganishwa na Somalia.
Eneo la Sool liko katika sehemu ambayo inadaiwa na jimbo la Puntland na imeshuhudia msukosuko siku za hivi karibuni.
Mwandishi wa BBC Hagar Jibril ambaye yuko katika
eneo jirani la Burao, anasema kuwa watu walishuhudia tukio hilo
wanasema Ilyas alipigwa risasi na watu wawili waliokuwa wamejihami
nyakati za jioni.
Mapema siku ya Jumanne, watu wanne walijeruhiwa
baada ya kulipukiwa na mabomu ya kutega ardhini ambayo gavana wa eneo la
Sool Mahamed Mahamud Ali alisema yalitegwa na Al Shabaab.
Duru zinaarifu kuwa kesi dhidi ya wanamgambo hao ilianza kusikilizwa mjini Las Anod siku ya Jumanne.

0 comments:
Post a Comment