WAGOMBEA kiti cha Urais wa Marekani Rais Barack Obama na
mwenzake Mitt Romney wamefanya mdahalo wao wa kwanza kupitia televisheni
ambao umewaacha wengi na mshangao kutokana na kwenda kinyume na
matarajio yao.
"Miaka minne iliyopita niliposimama katika jukwaa hili nilisema kuwa
nitapunguza kodi kwa familia zenye kipato cha kati. Na hivyo ndivyo
nilivyofanya.
Tumepunguza kodi kwa familia za kipato cha kati kwa kiasi
cha dola 3600.
Na sababu ni kuwa naamini tutakuwa na mafanikio kama watu
wa kipato cha kati watakuwa na mafanikio".
Rais Barak Obama akizungumza katika mdahalo wa Denver Colorado, Marekani
HIVYO ndivyo alivyoanza mazungumzo Rais Obama katika mjadala huo
uliofanyika Chuo Kikuu cha Denver mjini Colorad na kutazamwa moja kwa
moja kupitia televisheni na watazamaji wanaokadiriwa kufikia milioni 50.
Obama alizungumza kwa muda mrefu lakini mpinzani wake Romney alimkosoa
zaidi kwa namna anavyoendesha utawala wake jambo ambalo lilionekana
kumgusa.
Mkurugenzi wa kituo cha siasa na masuala ya umma Terry Madonna
anasema kuwa Obama hakuwa katika hali yake ya kawaida hivyo hakufanya
vile ambavyo wafuasi wake na watu wengine duniani walivyotarajia.
Romney alimshambulia kwa Rais Obama juu ya histora yake ya
kushughulikia matatizo ya kiuchumi lakini safari hii hakuropoka wala
kutoa matamshi ya kutatanisha kama alivyozoeleka.
MASHAMBULIZI YA ROMNEY.
Romney alitumia mtindo wa kushambulia na kisha kurejea katika nukta
zake akionyesha namna atakavyoshughulikia kila kosa la Obama
alilolionyesha.
Wachambuzi wanasema kuwa Romney ameweza kumbwaga
mpinzani wake katika awamu hiyo ya kwanza ya mdahalo.
"Sina shaka akilini mwangu kuwa kama rais atachaguliwa tena mtaendelea
kuona watu wa kipato cha kati wakishuka zaidi huku kipato kikipungua na
bei zikipanda juu.
Nitainua kipato tena. Tuna ukosefu wa ajira wa
asilimia nane zaidi mwezi huu na kama nikiwa rais nitatoa nafasi mpya za
ajira milioni 12 kwa nchi hii", alisema Romney.
Mitt Romney mgombea wa Republican akizungumza katika mdahalo
KWA upande wa masuala ya afya Romney aliuponda mpango wa afya,
maarufu kama Obamacare, wenye thamani ya dola za Marekani trilioni 2.8
na kusema haufai lakini hakuweza kuja na mbadala sahihi kwa wapigakura.
Masuala ya afya ni moja kati ya ajenda kuu kuelekea uchaguzi wa Novemba
6 mwaka huu.
Mpango wa huduma za afya wa Marekani ndio wenye gharama
zaidi kuliko nchi zote na unalaumiwa kuwa kuchangia katika kushuka kwa
mishahara ya Wamarekani.
ROMNEY KINARA UCHAGUZI WA MAONI YA MDAHALO.
Mgombea mwenza wa Obama, Joe Biden.
UCHAGUZI wa maoni uliofanywa na kituo cha televisheni cha CNN kwa
watu wenye umri wa kupiga kura na walioangalia mdahalo huo unaonyesha
kuwa Romney amepata asilimia 67 huku Obama akiambulia asilimia 25.
Uchunguzi kama huo umefanywa pia na kituo cha televisheni cha CBS na
Romney amepata ushindi.
Huu ni mdahalo wa kwanza kati ya mitatu iliyopangwa kufanyika. Wagombea
wenza kutoka pande zote mbili watakutana pia kwa mdahalo wiki ijayo.
Watu wanasubiri kuona nini kitajiri kati ya mgombea mwenza wa Obama Joe
Biden kutoka chama cha Democrat na yule wa Romney Paul Ryan kwa tiketi
ya chama cha Republican
0 comments:
Post a Comment