BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BUNGE KAJIANDALIA ULAJI.


SPIKA WA BUNGE ANNA MAKINDA.

BUNGE la Tanzania, limeanza kupitia upya ratiba ya mikutano yake ya kila mwaka kwa lengo la kuifanyia marekebisho ili iendane na mapendekezo yaliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). 

Taarifa za uhakika zilizolifikia MTANZANIA kutoka ndani ya Ofisi za Bunge, zimeeleza iwapo marekebisho hayo yatafikiwa, siku za kufanyika mikutano ya Bunge na vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge zitaongezeka.

Mabadiliko hayo, yanayoelezwa kuwa yatabadili kwa kiasi kikubwa mwenendo wa uendeshaji wa Bunge, yatakwenda sambamba na kuongezeka kwa posho na marupurupu wanayopata sasa wabunge, maofisa wa Bunge na mawaziri.

Kuongezeka kwa posho na marupurupu ya wabunge, maofisa wa Bunge na mawaziri kutazidi kupaisha juu kipato chao wanachojikusanyia kila mwezi ambacho hata hivyo kimekuwa kikilamikiwa na wananchi wengi kuwa hakiendana na mapato halisi ya watanzania.

Mshahara anaopata mbunge kwa sasa ni Sh milioni 11, ambao unajumuisha posho ya ubunge na usafiri. Pia mbunge anapohudhuria Bunge analipwa posho ya kijikimu Sh 150,000 kwa siku na posho ya kuketi kwenye kikao Sh 200,000 kila anaposaini kuingia kwenye kikao cha Bunge.

Kwa mwaka, Kamati za Kudumu za Bunge huketi kwa siku 40 na mikutano ya Bunge hufanyika kwa siku 90 za kazi nje ya siku za mapumziko ya mwisho wa wiki na siku za sikukuu. Idadi ya siku za kufanyika kwa vikao vya kamati na mikutano ya Bunge itaongezeka baada ya kupitishwa kwa mabadiliko yaliyopendekezwa na CAG.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mabadiliko hayo yamelenga kubadilisha muda wa kufanyika kwa mkutano wa kila mwaka wa Bunge la Bajeti ambalo kwa kawaida limekuwa likiketi kati ya Juni hadi Agosti na badala yake litakuwa likiketi kuanzia mwezi Aprili hadi Juni. 

Sambamba na kubadilika kwa muda wa kufanyika kwa mkutano wa Bunge la Bajeti, muda wa kufanyika kwa vikao vya Kamati za Bunge nao unakusudiwa kuongezwa ili kutoa nafasi zaidi kwa wabunge kutekeleza majukumu yao ya kibunge wakiwa katika kamati zao hizo ambazo zinatambulika rasmi kuwa sehemu ya shughuli za Bunge.

Baadhi ya wabunge walioko Dar es Salaam, wanakohudhuria vikao vya Kamati za Bunge vilivyoanza mapema wiki hii, wamelieleza MTANZANIA,kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge kwa nyakati tofauti, imekuwa ikikutana katika ofisi ndogo ya Bunge iliyoko Dar es Salaam na mjini Dodoma kuchambua mapendekezo yaliyotolewa na CAG ya kubadilisha mwenendo wa mikutano hiyo, hususani muda wa kuketi kwa mkutano wa Bunge la Bajeti ili uendane na kalenda ya bajeti ya serikali.

Wabunge hao ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini, walisema ingawa hadi sasa hakuna taarifa za kubadilika kwa siku za kufanyika kwa mikutano ya Bunge, wanatarajia kutangaziwa mabadiliko hayo wakati wowote katika mkutano ujao wa Bunge unaotarajiwa kuanza Januari 29, mjini Dodoma.

Mmoja wa wabunge aliyezungumza na MTANZANIA katika ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam jana, alisema mabadiliko hayo yanalenga kuelekeza kazi nyingi za kibunge kwenye Kamati za Bunge tofauti na inavyofanyika ya sasa ambapo shughuli hizo zinafanyika wakati wa mikutano ya Bunge, jambo linalopunguza ufanisi wake.

Alisema, kudorora kwa vikao vya Bunge kunakolalamikiwa na wananchi wengi kwa kiasi kikubwa kunachangiwa na wingi wa shughuli wanazokuwa nazo wabunge wakati wa mikutano rasmi ya Bunge.

Mbunge huyo, alisema miswada mbalimbali ya Serikali inayopangwa kuwasilishwa katika mikutano ya Bunge imekuwa haijadili vizuri na wabunge kwa sababu wakati vikao vikiendelea baadhi yao huwa wana kazi muhimu za kufanya katika kamati zao za kibunge.

“Mapendekezo ya CAG yamelenga kuboresha ufanisi wa kazi za wabunge. Ratiba ya sasa ya mikutano ya Bunge siyo nzuri kwa sababu ni finyu na mambo ni mengi sana. Ndiyo maana wakati mwingine unakuta idadi kubwa ya wabunge hawako bungeni kwa sababu ya kubanwa na kazi nyingine za kibunge wakati vikao vinaendelea. Hili likibadilishwa wabunge tutafanya kazi zetu vizuri na kwa ufanisi.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alipoulizwa kuwepo kuwepo kwa mabadiliko hayo alisema jambo bado linajadiliwa na iwapo litaafikiwa, uamuzi utatangazwa mapema mwezi ujao wakati wa mkutano ujao wa Bunge.

Alisema kufanyika kwa mabadiliko hayo, kunatokana na mapendekezo yaliyotolewa na CAG ya kubadilisha muda wa kufanyika kwa mikutano ya Bunge kuonakena yana umuhimu katika kuboresha shughuli za Bunge jambo ambalo lilichukuliwa na Bunge na sasa linajadiliwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge.

Hata hivyo, bado kuna sintofahamu ya kufikiwa kwa uamuzi huo kutokana na makubaliano ya uendeshaji Mkutano wa Bunge wa Bajeti ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yanayoelekeza kuwa bajeti za serikali za nchi wanachama zinapaswa kusomwa siku moja kwa nchi zote.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivi sasa zinafanyana mikutano yake ya Bunge la Bajeti kati ya Juni na Agosti, hivyo ili mabadiliko yanayolengwa kufanywa na Bunge la Tanzania yaweze kutekelezwa, inabidi nchi nyingine wanachama nazo zibadili ratiba zake za kusomwa kwa bajeti za Serikali zao. 
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: