BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM YAPASUKA VIPANDE MKOANI KAGERA, MAKAMU MWENYEKITI PHILIP MANGULA AENDA KUVIUNGANISHA.



MAKAMU MWENYEKITI CCM TAIFA PHILIP MANGULA.Meya  wa Manispaa ya Bukoba Mh, Anathory Aman akikata utepe wakati wa ufunguzi wa nane nane.

MGOGORO mkubwa unaoendelea kufukuta ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukoba Mjini mkoni Kagera kati ya madiwani na Meya wa Manispaa hiyo, Anatory Amani, umemlazimu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula, kwenda kutuliza upepo.

Kiongozi huyo anatarajiwa kuwasili mjini Bukoba leo kujaribu kutafuta muafaka wa kutuliza fukuto la madiwani hao kutaka kumng’oa Amani, wakimtuhumu kuwa ameingiza halmashauri kwenye miradi ya kifisadi.

Baadhi ya madiwani hao tayari wameapa kuwa wako radhi kupoteza nyadhifa zao au kwa kufukuzwa au kujivua uanachama lakini lazima wahakikishe Amani anang’oka ili kuinusuru CCM katika tuhuma za ufisadi.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka mjini Bukoba, zinasema kuwa CCM imelazimika kumtuma Mangula baada ya Amani kukimbia kikao cha madiwani wa chama hicho kilichokuwa kimjadili ili kutafuta ufumbuzi wiki iliyopita.

Meya alitumia sababu ya ugonjwa na kuondoka kikaoni muda mfupi baada ya katibu wa kikao, Ashura Hassan na msaidizi wake, Hilde Blandus, nao kuondoka kwa visingizio kama hivyo.

Pamoja na kudai kuugua, Amani aligoma kuwapatia wajumbe muhtasari wa kikao cha kamati ya siasa ya wilaya kilichopita akidai katibu wake aliondoka nazo.

Meya huyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Kagondo, anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu na hivyo kikao hicho cha madiwani wa CCM kilikuwa kijadili na kupata muafaka wa ama ang’oke mwenywe au asubiri kura za kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kiitishwe leo.

“Kikao hicho kilikuwa kijadili na kisha kupeleka ripoti kwenye kamati ya saisa ya wilaya, lakini kutokana na kuahirishwa bila muafaka ina maana madiwani tunaendelea na hoja yetu kwenye ‘full council’,” alisema mmoja wa madiwani hao.

Tayari madiwani nane wa CCM akiwemo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, na wengine wawili wa upinzani wametia saini hati ya kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo, aitishe kikao cha dharura ili kumng’oa meya huyo.

Hata hivyo, kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kiitishwe leo hakitakuwepo kwa kile kilichodaiwa kuwa Amani kupitia mwanasheria wake alimwagiza mkurugenzi asikiitishe akidai madiwani hao walikiuka kanuni.

Kaimu mkurugenzi wa manispaa hiyo, Salapion Rujugulo, alikanusha madai hayo jana, akisema kuwa mkurugenzi alikuwa nje ya kituo akifanya mitihani yake chuoni Mzumbe, kwamba akirejea atawaandikia barua madiwani kuwaalika kikaoni.

Licha ya tarehe ya kikao kutotajwa, Tanzania Daima ilidokezwa kuwa mkurugenzi huyo, Hamis Kaputa, jana alikuwa njiani kurudi kazini kumuwahi Mangula ambaye anaingia mjini humo akitokea Mwanza.

Hoja ya kumng’oa meya iliibuliwa hivi karibuni na Balozi Kagasheki, ambaye pia ni Waziri wa Malialisili na Utalii, akiunga mkono msimamo wa CHADEMA, kupinga miradi ya uuzwaji wa viwanja zaidi ya 5000 na ujenzi wa soko la kisasa.

Kagasheki aliapa mbele ya wapigakura wake kuwa hayuko tayari kusutwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kutokana na mikataba ya siri yenye harufu ya kifisadi aliyoisaini Amani kwa kificho bila kuwashirikisha madiwani wenzake.

Taarifa za ndani zinadai kuwa rushwa imeanza kutembezwa kwa baadhi ya madiwani wa vyama vyote ili kuwarubuni wasipige kura ya kumng’oa meya.

Baadhi ya vigogo wa serikali akiwemo mkuu wa wilaya na mkoa, mwenyekiti na katibu na chama tawala mkoa wa Kagera, wamekuwa wakifanya kila juhudi kumnusuru Amani asing’olewe.

Mkuu wa Mkoa, Kanali mstaafu Fabiani Massawe, ametajwa kumkingia kifua meya kwa kuwaziba midomo madiwani wasichukue uamuzi wao, jambo ambalo limeibua mgawanyiko kwa baadhi ya wana-CCM mkoani humo wakihoji ni kwa nini anamlinda mtuhumiwa.

Mgogoro huo ulikwishamfikia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na Kanali Massawe anadaiwa kujaribu kutaka kumshawishi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, aingilie kati.

“Massawe anahaha kumnusuru meya lakini sisi tunaangalia salama ya chama chetu mbele ya upinzani kwenye uchaguzi ujao. 

Huyu alijaribu kumpigia simu Ghasia lakini waziri huyo alimtaka ampelekee malalamiko kwa maandishi akisema hafanyi kazi kupitia simu,” alisema.

Halmashauri hiyo ina madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM.

Ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.

Miongoni mwa vigogo waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha kumng’oa meya huyo ni Naibu wake, Alexander Ngalinda (Diwani wa Kata ya Buhende), na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Bukoba.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: