BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MKUU WA WILAYA YA ILEMELA MASENZA ATUHUMIWA KULIVURUGA KANISA LA FMCT MKOANI MWANZA.


MKUU wa Wilaya ya Ilemela, mkoani Mwanza, Amina Masenza, anatuhumiwa kuingilia kati maamuzi ya mahakama katika mgogoro unaofukuta katika Kanisa la The Free Methodist church in Tanzania (FMCT). 


Akizungumza na Mtanzania jijini Mwanza jana, Mchungaji wa Kanisa la FMCT, Remmy Stanslaus, alisema yeye bado ni kiongozi halali anayetambulika kisheria.



Alisema licha ya mahakama kutoa uamuzi wa kuendelea kumtambua kama mchungaji na msimamizi wa mali za kanisa hilo, lakini Masensa ameshindwa kutii amri za mahakama.

Mchungaji Remmy alisema kuwa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa kanisa hilo Raphael Mlumba, alifungua kesi namba 22 ya mwaka 2011 katika mahakama ya mwanzo Ilemela.

“Kisha kesi namba 17 ya mwaka 2011 na kisha kesi namba 3 ya mwaka 2012, katika mahakama ya mkoa akitaka kanisa hilo lisinitambue mimi na kukabidhi mali zote chini ya uangalizi wake,” alisema.

Kwa mujibu wa Mchungaji Remmy, mahakama katika maamuzi yake tofauti iliamua kumtambua kama msimamizi wa mali zote za kanisa hilo.

Alisema katibu mkuu wa zamani wa kanisa hilo amekuwa akilipinga na kuamua kukimbilia katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela.

Mchungaji Remmy alisema kuwa, alipata taarifa ya kuhitajika kwa Masenza na kwamba alipofika alielezwa kuwa, anatakiwa kuketi meza moja na Katibu Mkuu wa kanisa hilo aliyeondolewa Raphael Mlumba, ili kujadili namna ya kusimamia mali za kanisa hilo.

Mchungaji huyo alisema kuwa, alishangazwa na kauli za mkuu huyo wa wilaya kwa kuwa suala hilo tayari lilikuwa limeshamalizwa na mahakama na kutoa maamuzi ya kumtambua yeye na kutaka mali zote ziwe chini ya uangalizi wake.

“Katibu mkuu alimueleza DC kuwa, nimefunga kanisa, pale Nyasaka hakuna kanisa bali kuna shule ya awali ya watoto, hii inashangaza sana kwa mkuu wa wilaya kushindwa kuheshimu utawala wa sheria,” alisema.

Alisema kuwa, hayuko tayari kushirikiana na katibu mkuu huyo ambaye hatambuliki kutokana na kusimamishwa na kanisa la FMCT na kumtaka DC huyo kuheshimu amri ya mahakama.

“Kuna uongozi utakuja toka makao makuu ya Kanisa yaliyopo DRC pamoja na Burundi, nao wana nakala ya hukumu ya mahakama, sipendi suala hili lichukuliwe kisiasa, kwani wakati wa kesi mlalamikaji aliwasilisha nyaraka ambazo mahakama iliziona zina mapungufu ndio maana nikaamuliwa niendelee kusimamia mali zote za kanisa letu,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Amina Masenza, hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, kutokana na simu zake za mkononi kutokuwa hewani muda wote alipopigiwa, ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo.

CHANZO http://www.mtanzania.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: