BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

POLISI WANASWA NA PEMBE ZA NDOVU KAGERA.

PEMBE ZA NDOVU PICHA YA MAKTABA.
TEMBO.

ASKARI polisi wawili na raia mmoja wa Wilaya ya Biharamlo mkoani Kagera, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani hapa, baada ya kukamatwa na vipande 17 vya meno ya Tembo. Tukio hilo lililotokea jana katika Kijiji cha Rwamchanga mjini Mugumu, limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alipozungumza na MTANZANIA.

Kamanda huyo aliwataja askari waliokamatwa kuwa ni Koplo David Delina mwenye namba E9172

kutoka ofisi ya upelelezi Biharamulo na Gerard Tuti mwenye namba F5553, ambaye ni mpelelezi kutoka Ofisi ya Kamanda wa Makosa ya

Jinai Bukoba na raia ni Boniphace Kurwa (31) mkazi wa Geita.

Askari hao walikamatwa katika nyumba ya kulala wageni ya Galaxy iliyoko mjini Mugumu, saa 8 usiku baada ya kutajwa na Kurwa aliyekutwa na meno hayo.

Kamanda Mwakyoma alisema askari hao baada ya kuhojiwa walikiri kuwa walifika hapo kwa maelekezo ya mfanyabiashara mmoja Boniphace Emmanuel (maarufu kama Mnyarwanda mkazi wa Biharamulo).

Kukamatwa kwao kunatokana na taarifa zilizotolewa polisi kutokana na intelejensia kali ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), kwa ajili ya kukabiliana na mtandao huo hatari unaoundwa na wafanyabiashara wakubwa.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, inadaiwa kuwa askari polisi wakishirikiana na askari wa hifadhi ya taifa ya Serengeti wakiwa kwenye doria walifanikiwa kumkamata Boniphace Kurwa akiwa katika pikipiki.

Mtuhumiwa huyo akiwa na mwenzake aliyetambuliwa kwa jina moja la Nyarata, ambaye alikuwa na pikipiki yenye namba za usajili T 834 BPH Toyo, ambazo wamiliki wake wanafuatiliwa walikuwa wamebeba nyara hizo.

Hata hivyo Nyarata alifanikiwa kukimbia na kutelekeza pikipiki na mzigo huo na anasakwa ili aunganishwe na wenzake kwenye kosa hilo.

Mwakyoma alisema baada ya kubanwa mtuhumiwa huyo aliwataja askari hao na kuwapeleka askari hadi nyumba ya kulala wageni ya Galaxy, iliyoko mjini Mugumu na kuwakamata.

“Hao askari walikuja na gari aina ya Toyota Carina yenye namba za usajili T403 BPK, inasemekana ni mali ya Koplo David,” alisema Kamanda.

Kwa mujibu wa kamanda huyo askari hao tayari wameshasomewa mashitaka ili taratibu za kiraia ziweze kuchukua nafasi yake.

“Suala la maamuzi ya kijeshi yaliyofikiwa bado…lakini watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Januari 8 mwaka huu, taratibu za uchunguzi zinaendelea,” alisema.

Alidai watumishi wa Serikali wanatakiwa kutambua kuwa hawako juu ya sheria na wale wote wanaotuhumiwa na kuthibitika watakamatwa na kufikishwa mahakamani kama raia wengine.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vya habari zinadai kuwa, watuhumiwa hao waliingia mjini Mugumu Januari 4 mwaka huu wakiwa na gari Toyota Ballon lenye namba za usajili T403 BJK kutokea Biharamulo.

Watuhumiwa hao wakiwa na mwanamke mmoja walifikia hoteli ya Galaxy, ambapo Delina alilala chumba namba 29 na Tuti ambaye alikuwa na mwanamke walilala chumba namba 28.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TANAPA, Allan Kijazi alipoulizwa juu ya sakata hilo alitaka sheria ichukue mkondo wake kwa kuwa ujangili unatishia uhai wa wanyama.

“Kazi yetu ni ulinzi wa maliasili hizi hivyo hatutasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayekamatwa kwa kosa la ujangili na tunapambana kuhakikisha huo mtandao wa ujangili unatokomezwa,” alisema.

 CHANZO http://www.mtanzania.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: