MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imepokea silaha mbalimbali
yakiwamo mapanga, visu, majembe, sufuria, makoleo na sufuria kama
kilelezo katika kesi inayomkabili Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake
49.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne likiwamo la wizi wa
mali yenye thamani ya Sh. milioni 59.6, uchochezi na kuingia kwa jinai
katika ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya
kujimilika isivyo halali.
Vielelezo
hivyo vilitolewa na shahidi ambaye ni mpelelezi kutoka Mkoa wa Kipolisi
Temeke, jijini Dar es Salaam, Thobias Walelo (34), mbele ya Hakimu
Mkazi Victoria Nongwa.
Mbali na
silaha hizo, pia shahidi huyo aliwasilisha mahakamani hapo jenereta,
mabegi mawili ya nguo, nyundo na ndoo za plastiki ambavyo vilipokelewa
kama vielelezo vya kesi hiyo.
Alidai kuwa Oktoba 12, mwaka jana, majira ya alasiri, alipokea jalada kutoka kwa bosi wake kwa ajili ya kulifanyia kazi.
“Nilipolisoma
lilikuwa na taarifa kwamba kiwanja cha kampuni ya Agritanza Ltd
kimevamiwa na Sheikh Ponda na wenzake,” alidai shahidi.
Shahidi
huyo ambaye ni wa 10 wa upande wa mashitaka, alidai kuwa yeye alikuwa
mhusika kupeleleza jalada hilo, akishirikiana na D/Ssgt Juma na D/Koplo
Furaha, kwa kupitia maelezo ya mlalamikaji na nyaraka za mabadilishano
ya ardhi hiyo kati ya kampuni ya Agritanza Ltd na Bakwata.
Alidai
kuwa yeye mwenyewe alikwenda Manispaa ya Temeke kwa Bwana Ardhi
kufuatilia ukweli wa nyaraka hizo za mabadilishano ya ardhi na kupewa
majibu kuwa eneo hilo linamilikiwa kihalali na kampuni ya Agritanza
Ltd.
Aliendelea
kudai kuwa Oktoba 14, 2012, baada ya kupata picha hiyo kamili, akiwa na
askari wenzake, walikwenda eneo la Chang’ombe Malkazi na kukuta umati
wa watu.
"Niliwaambia sikwenda kwa nia mbaya, nikawaomba waniteulie viongozi wao ili niongee nao,” alidai shahidi huyo.
Aliongeza
kudai kuwa waliwateua Sheikh Hussein Ismail, Sheikh Said Nyoni, Mukadam
Swalehe na Mbaraka Daruwesh, ili kupata uhalisia wa mawazo ya umati na
nyaraka walizokuwanazo kuhusiana na eneo hilo.
"Walipofika
ofisini kwangu, niliwaomba nyaraka wakadai hawakuja nazo, niliwaomba
niandike maelezo yao kuhusiana na kile wanachokilalamikia, wakataka
yachukuliwe mbele ya wakili wao na wakaomba kwenda kumchukua.
“Kwa
kuzingatia kauli mbiu ya jeshi la Polisi ya kutii sheria bila shuruti,
niliwaamini waende wakamlete wakili wao ili mchana wa Oktoba 15, 2012,
nichukue maelezo yao,” alidai shahidi huyo wa 10 wa upande wa Jamhuri.
Alidai kuwa kabla ya kuwaruhusu alichukua namba zao za simu za mkononi baada ya kuwaruhusu, hawakurudi tena.
"Nilipoona
muda unakwenda, niliwapigia simu wakaniambia: “Mheshimiwa, ukweli huko
hatutarudi tena, tumia maelezo hayo hayo ya mdomo tuliyokwambia sisi."
Baada ya
kupata taarifa hiyo, niliandika barua kwenda Manispaa ya Wilaya ya
Temeke na nikapata uthibitisho kuwa eneo hilo linamilikiwa na kampuni ya
Chang’ombe Malkazi.
“Niliwafahamisha
wakuu wangu wa kazi, ikapangwa timu na Oktoba 16, 2012 kuamkia Oktoba
17, 2012, tulikwenda eneo hilo na kuwakuta watuhumiwa wote tukawakamata
na kuwapelekea kituo cha polisi cha Kijitonyama kwa ajili ya mahojiano
kasoro washtakiwa Mukadam na Ponda,” alidai shahidi huyo.
BY HELLEN MWANGO
SOURCE: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment