IGP, Said Mwema.
IMAMU wa Msikiti wa Mwakaje, Sheikh Ali Khamis Ali (65) ameuawa kwa kupigwa kisu cha shingo na watu wasiojulikana huko Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis, amethibitisha kiongozi huyo wa dini ya Kiislamu kuuawa shambani kwake majira ya saa 8:00 mchana juzi.
Hata hivyo, alisema kwamba uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umeonesha sheikh huyo atakuwa ameuawa na watu wanaosadikiwa kuwa wezi wa mazao baada ya kuwakamata wakiiba katika shamba lake.
Alisema kwamba Sheikh Ali alikwenda shambani kwake huko Kitope kukagua mazao, na baada ya kufika aliwakuta watu wakiiba nazi, na kusababisha purukushani kabla ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali na kufa.
Alisema kwamba marehemu alikuwa Imamu wa Msikiti wa Mwakaje sehemu anayoishi, huku akifanya shughuli zake katika shamba ambalo lipo Kitope katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Hata hivyo, alisema kwamba tukio la kuuawa kwa kiongozi huyo halina uhusiano wowote na vurugu za kidini, na matukio ya kuhujumiwa viongozi wa dini Visiwani Zanzibar.
Kamanda Ahmada, alisema kwamba polisi baada ya kupokea taarifa za tukio hilo, walifika katika eneo la tukio na kumkuta imamu huyo akiwa na jeraha upande wa kulia wa shingo yake.
“Tumeanza kufanya uchunguzi wa kuwasaka watu waliohusika na mauaji hayo, na kwamba watu hao kabla ya kumuua imamu huyo walikuwa wamefanikiwa kuvuna nazi na kuzifua.
“Wamemuua kwa kumpiga na kitu chenye ncha baada ya kuwakamata wakiiba nazi katika shamba lake,” alisema.
Akizungumzia mkasa huo, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pembe Khamis, alisema kwamba marehemu alikuwa akiishi katika Kijiji cha Mwakaje na shughuli zake za kilimo alikuwa akifanya huko Kitope Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kwamba baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitibabu wanafamilia walikabidhiwa maiti kwa ajili ya maziko juzi.
Viongozi waliohujumiwa hadi sasa visiwani hapa ni pamoja na Katibu wa Mufti, Sheikh Fadhili Suleiman Soraga, ambaye alimwagiwa tindikali Novemba 6 mwaka jana wakati akifanya mazoezi ya viungo huko Magogoni Msumbiji na kutibiwa nchini India.
Wakati wananchi wakitafakari tukio hilo, Desemba 25 mwaka jana, Padiri wa Kanisa la Katoliki Jimbo la Zanzibar, Ambrose Mkenda, alinusurika kufa baada ya kupigwa risasi mbili na kukimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Febuari 17, mwaka huu, Padiri Evaristus Mushi, aliuliwa kwa kupigwa risasi tatu kichwani wakati akienda kuongoza misa ya Jumapili katika Kanisa la Theresia huko Kibweni.
Matukio hayo yalitanguliwa na kuchomwa moto makanisa 25 na baa 12 katika maeneo tofauti Zanzibar.
Lakini hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa na
kufikishwa mahakamani kuhusika na matukio hayo.
0 comments:
Post a Comment