BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UGAIDI, UNYAMA ZANZIBA.

BAADHI YA VIGOGO SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZABAR WATAJWA KUFADHILI UGAIDI.

 https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhPbJBFbUx5CRsKZxWpVNfTSu32N4I0mAJeckUvZnP0W32oxD5VISmWvCa3gVgOLn4jbSVUWlENlPpCx-vB4hLmtaOO0ctMUIKVUQBjKu6E16NI_WWIGrAWP4R1C8_U3WE6VbFMTKKc0GxE/s1600/Dk-Shein1.jpg
RAIS WA ZANZIBA DK MOHAMED SHEIN.

VITENDO vya uchomaji makanisa moto vimeendelea kutikisa mji wa Zanzibar baada ya Kanisa la The Pool of Siloam, kuchomwa moto na watu wasiojulikana.

Tukio hilo ambalo limetokea siku chache baada ya Padri wa Kanisa Katoliki, Evarist Mushi, kuuawa kwa kupigwa risasi, limetokea jana katika eneo la Kianga, mkoa wa Mjini Magharibi, kisiwani Unguja, jana.

Hali hiyo imezidisha hofu kwa viongozi wa dini na waumini wao, huku Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ikiimarisha ulinzi katika makanisa yote mjini hapa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa siku kadhaa sasa, umebaini kuwapo kwa baadhi ya viongozi wa SMZ, wanaotajwa kufadhili vikundi vya kigaidi kwa lengo la kufanikisha nia zao.

Duru za uchunguzi kutoka visiwani humo, zililiambia gazeti hili kuwa baadhi ya wanaotajwa kuhusika wamo wanafanyakazi serikalini katika nafasi za juu na wengine wamestaafu.

“Kwa nini hamjiulizi tangu matukio hayo yatokee hivi karibuni kuanzia kwa sheikh aliyemwagiwa tindikali, kupigwa risasi kwa padri mwingine na hatimaye kuuawa kwa Padri Mushi? Kweli serikali haiwajui?” alihoji kiongozi mmoja wa SMZ ambaye anaeleza kukerwa na hali hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la kuchomwa moto kwa kanisa hilo la walokole jana, Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo, alisema kanisa hilo lilichomwa moto majira saa 9:00 usiku wa kuamkia jana na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za kanisa hilo.

Kamishina msadizi huyo wa polisi, alisema mlinzi wa kanisa, Mussa Jackison, alivamiwa na watu watatu na kuanza kushambuliwa kwa mawe lakini hakujeruhiwa kabla ya kutimua mbio.

Alisema baada ya mlinzi kufanikiwa kukimbia walikusanya mali za kanisa vikiwemo viti na mali zingine, kisha kuvichoma moto.

Hata hivyo alisema kwamba uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umeanza lakini hakuna watu waliokamatwa hadi sasa.
“Kanisa limechomwa moto majira ya saa 9:00 usiku baada ya watu watatu kumvamia mlinzi na kuanza kumrushia mawe,” alisema DCI Ilembo.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano Mchungaji wa Kanisa hilo, Penuel Wisdom, alisema alipokea taarifa za kanisa lake kuchomwa moto kwa mshtuki mkubwa kutokana na ukweli kwamba hilo ni tukio la pili kwa kanisa lake kuhujumiwa.

Alisema mwaka 2011, watu wasiopungua 80 walivamia kanisa lake na kulibomoa kwa kutumia vifaa vizito, zikiwemo sululu na nyundo za kuvunjia mawe.

Alisema katika tukio hilo, watu kadhaa walikamatwa na kukiri lakini hakuna hata mmoja aliyefikishwa katika vyombo vya sheria.

“Ombi letu kwa serikali ni kuimarisha ulinzi; tunaona usalama wa viongozi na waumini unatoweka kwa kasi Zanzibar,” alisema mchungaji huyo.

Alisema kwamba tangu kujengwa kwa kanisa hilo viongozi, waumini na wananchi wa Kianga wamekuwa na ushirikiano mkubwa na kusaidiana mambo ya msingi ya huduma za jamii kama kisima cha kanisa kutumiwa na majirani pamoja na uongozi wa kanisa kuazima huduma za umeme kutoka nyumba za jirani.

Hata hivyo alisema kwamba baada ya mradi wa ujenzi wa kanisa kuanza katika eneo hilo viongozi wa msikiti wa Kianga waliwahi kuhoji uhalali wa kujengwa kwa kanisa mahali hapo.

Alisema vyombo vya dola vinapaswa kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka kuwasaka watu wanaofanya vitendo hivyo kwa sababu wanatishia amani na umoja wa kitaifa kwa wananchi wa Tanzania.

Akizungumza kwa njia ya simu Sheha wa Kianga, Taufiki Ramadhan, alisema amepokea taarifa za kuchomwa moto kanisa hilo kwa masikitiko makubwa kwani kitendo hicho kinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu.

Alisema makanisa Zanzibar yamekuwepo kwa miongo mingi na waumini wa Kislamu na Wakiristo wamekuwa wakiishi pamoja bila ugomvi licha ya kutofautiana imani zao za dini na kushirikiana shughuli za kijamii kama kawaida.

Alisema hata utawala wa Kisultani ulikuwa ukiheshimu uhuru wa watu kuabudu ndiyo maana Wakiristo walipewa maeneo ya ardhi kujenga makanisa katikati ya mji mkongwe wa Zanzibar na utawala wa Sultan kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

“Baada tu ya kupokea taarifa za kanisa kuchomwa moto niliwasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi na Viongozi wa Jeshi la Polisi nashukuru walifika katika tukio na kuanza kufanya kazi ya uchunguzi,” alisema Sheha Ramadhan.

Naye mlinzi, Mussa Jackson, alisema baada ya kuwaona watu wakinyatia alijaribu kujitokeza ghafla aliona mvua ya mawe ikimwelemea na kuamua kukimbilia ndani ya kanisa kabla ya kutokea dirishani.

“Hali ilikuwa mbaya, walianza kukusanya kila kitu na baadaye kuwasha moto,” alisema Jackson.

Alisema kwamba tukio hilo linamkumbusha mwaka 2011 baada ya watu waliokuwa wakipinga kujengwa kwa kanisa hilo walipovamia na kulibomoa wakiwa na silaha za jadi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kusini Unguja Zanzibar, ACP Augustine Olomi, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 9.30 usiku.

Amesema moto huo ulizuka baada ya kikundi cha watu watatu kuonekana wakipita njia karibu na kanisa hilo na baada ya muda mlinzi wa kanisa hilo alisikia kanisa likishambuliwa kwa mawe juu ya paa.

Amesema baada ya mlinzi huyo kubaini kuwepo kwa hatari, alilazimika kukimbia kwenda kujificha lakini huku akiangalia kwa mbali kinachoendelea.

Kamanda Olomi amesema moto huo ungeweza kusababisha athari kubwa kama usingedhibitiwa mapema.

Hata hivyo amesema uimara wa dari lililotengenezwa kwa Gibsam umesaidia kuuzuia moto huo kuunguza paa na kuliteketeza kabisa kanisa hilo.

Kamanda huyo alisema wameimarisha ulinzi katika makanisa yote, huku wakiendelea na uchunguzi wa matukio hayo.

Mkasa wa kanisa kuchomwa moto umeongeza idadi na kufikia makanisa 26 na baa 12 kwa muda wa miaka 10 visiwani humo.

Hata hivyo hakuna mtu hata mmoja aliyewahi kukamatwa kuhusiana na matukio hayo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Matukio hayo yalifuatiwa na Katibu wa Mufti Zanzibar Shekh Fadhili Suleiman Soraga kumwagiwa tindikali Novemba 6 na Padri wa Kanisa Katoliki Ambrose Mkenda kupigwa risasi na kutibiwa Mhimbili Desemba 25 mwaka jana kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi Padri wa Evaristus Mushi Jumapili iliyopita Zanzibar.

Padri Mushi anazikwa leo katika makaburi ya mapadiri huko Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo misa ya kuanga mwili wa marehemu itafanyika katika Kanisa la St. Joseph Minara miwili katikati ya mji mkongwe wa Zanzibar.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: