BODI ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imeingia tena katika
kashfa baada ya kuficha matokeo ya wahitimu zaidi ya 2,5000 waliofanya
mtihani wa kuhitimu mafunzo Novemba, 2012.
Matokeo ya wahatimu hao
yalitarajiwa kutangazwa Desemba, mwaka jana kama ilivyo kila mwaka
lakini hadi sasa bado hayajatangazwa kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.
Kwa mara ya kwanza bodi hiyo ilipata kashfa ya kutoa ajira kinyemela
na kusababishwa Mkurugenzi wake, Dk. Clemence Tesha pamoja na maofisa
wengine kufikishwa mahakamani Juni, mwaka jana.
Dk. Tesha na
wenzake walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kutumia
madaraka yao vibaya kwa kumuajiri Amani Ngonyani kama Meneja Maendeleo
na Biashara wakati hakusajiliwa kama mtaalamu na kukiuka kifungu cha 46
(1) cha sheria ya NBMM namba 23 ya 2007.
Bodi hiyo ambayo
imetokana na iliyokuwa Bodi ya Taifa ya Usimamizi wa Vifaa (NBMM)
imekuwa ikilalamikiwa kwa kushindwa kutumiza majukumu yake ipasavyo.
Gazeti
hili juzi lilipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wahitimu wa elimu
ya fani ya ununuzi na ugavi kwamba matokeo yao yameshindwa kuwekwa wazi
jambo ambalo limewanya kupoteza mwelekeo.
Wahitimu hao walisema
wamekuwa wakifuatilia PSPTB kupata matokeo yao lakini hawaelezwi sababu
za msingi tofauti na kuahidiwa kutangazwa muda wowote.
MTANZANIA ilifika katika ofisi za PSPTB kupata ufafanuzi lakini baadhi ya maofisa wa mamlaka hiyo hawakuwa tayari kuzungumzia.
Maofisa
hao ambao hawakutaka kutaja majina yao walianza kusukumia mpira akiwamo
anayehusika na mitihani akidai kuwa majibu anayo lakini hana kibali
kutoka kwa Dk. Tesha ambaye hakuwapo ofisini.
Hata hivyo baada ya
mvutano huo, Ofisa mmoja kutoka idara ya fedha aliamua kuzungumza na
MTANZANIA kwa ufupi kwa sharti la kutotajwa jina lake.
“Ni kweli mtihani ulifanyika Novemba, mwaka jana na matokeo bado hayajatangazwa Desemba kama ilivyozoeleka kila mwaka.
“Si
kwamba tunapenda kushikilia matokeo haya la hasha, kuna sababu kadhaa
zimesababisha hali hii kutokea lakini hadi sasa PSPTB tunafanya jitihada
za kuokoa wahitimu hao taaluma yao isipotee hivi hivi.
“Kubwa
zaidi ni kwamba bodi iliyopo sasa umri wao ni mkubwa kulingana na sheria
zetu ndio maana inashindwa kukaa na kubariki matokeo hayo, suala la
umri huo lipo juu yetu na taarifa hiyo tayari limefikishwa wizarani ili
kufanyiwa kazi.
“Hadi sasa bodi haina mamlaka ya kutangaza
matokeo hayo hadi itakapopatikana nyingine kisheria lakini kutokana na
hali kutokea tumefanya marekebisho katika sheria za PSPTB kuepusha
kurudia tatizo kama hilo.
“Sasa marekebisho tuliyoyafanya
tumeyapeleka wizarani ili kupata baraka na kama yakikubaliwa yatakuwa
suluhisho hapo baadaye na si kwa tatizo ambalo tayari limejitokeza
sasa,” alisema ofisa huyo.http://www.mtanzania.co.tz
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment