BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NJAA YATIKISA NUSU YA TANZANIA

http://www.freemedia.co.tzWaziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza.
HALMASHAURI 70 kati ya 136 nchini, zinakabiliwa na janga la njaa kutokana na ukame unaosababisha uzalishaji kuwa mdogo.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Chiza alisema kuwa pamoja na halmashauri hizo kukabiliwa na njaa, 47 kati ya hizo ziko katika hali ya ukame zaidi na kuifanya serikali kuhakikisha inatenga tani 69,452 za chakula ili kuwanusuru wananchi.

Alisema tathmini iliyofanywa na serikali kwa kipindi cha Septemba 2012 na Januari 2013, ilibaini kuwa halmashauri 47 katika mikoa 19 zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula kutokana na hali ya ukame.


Chiza aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Kilimamnjaro, Manyara, Morogoro, Lindi, Tanga, Mtwara, Pwani , Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mwanza, Mara, Kagera, Iringa, Mbeya, Rukwa, Dodoma na Singida.

Alieleza kuwa njaa katika halmashauri hizo inatokana na ukosefu wa mvua za vuli katika robo ya nne ya mwaka 2011/12 pamoja na upungufu wa chakula katika nchi jarani na zile za Sudan Kusini na hivyo kusababisha mfumko wa bei za vyakula.

Waziri aliongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa hali ya njaa katika maeneo mbalimbali nchini, serikali imeidhinisha chakula cha msaada tani 69,452.

Pia alikiri kuwa kuwepo kwa miundombinu mibovu kumewasababishia wakulima kushindwa kuuza mazao yao katika masoko mazuri na badala yake wamekuwa wakiuza kwa wafanyabiashara wasio waaminifu.

Alisema kuwa pamoja na serikali kuweka utaratibu wa kuimarisha kilimo, bado vijana wengi wanakimbilia mijini badala ya kujihusisha na sekta hiyo.

Katika bajeti yake, wizara imeomba kiasi cha sh 328,134,608,000 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Mchanganuo wake ni kwamba sh bilioni 247 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh bilioni 81 ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Chiza alisema katika matumizi ya kawaida sh bilioni 210.1 ni kwa ajili ya matumizi mengine, sh bilioni 25.6 (mishahara ya wizara) na sh 11.3 (mishahara ya bodi na taasisi).

Alisema kuwa kati ya fedha za bajeti ya maendeleo sh bilioni 23.9 ni fedha za ndani na sh bilioni 57.1 ni za nje.

Nayo Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imeishauri serikali kuongeza bajeti ya wizara hiyo kwa madai kuwa iliyotengwa kwa mwaka ujao ni ndogo na haiwezi kuleta tija.

Katika maoni yao, kamati ilisema kuwa ukuaji wa kilimo nchini unashuka mwaka hadi mwaka kama inavyoonyeshwa katika takwimu mbalimbali tangu mwaka 2009 hadi ifikapo 2014.

Kutokana na mtiririko wa kushuka kwa ukuaji wa kilimo, kamati iliishauri serikali kuhakikisha inafanya uamuzi wa makusudi ili bajeti ya sekta ya kilimo ifikie kiwango kilichokubaliwa na nchi za SADC cha asilimia 10 ya bajeti ya serikali ili kilimo kiweze kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa.

Akisoma maoni hayo, Prof. Peter Msollwa, alisema kamati ilipendekeza serikali kuongeza ruzuku ya pembejeo kwa wakulima ya sh 66,326,180,000 kama utaratibu wa vocha utatumika kutoa ruzuku na sh 108.508,500,000 kama utaratibu wa mikopo utatumika kutoa ruzuku.

Pia waliitaka serikali kulipa madeni ya wizara yanayofikia sh 20,326,323,310 ambayo yanahusisha wazabuni mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2010/2011 na 2011/12.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: