HABARILEO.
SERIKALI imelaani vikali vurugu
zilizotokea Mtwara juzi na imeapa kuwasaka waasisi wa vurugu hizo ndani
na nje ya Mtwara na ndani na nje ya nchi ili waliohusika kupanga,
kushawishi, kuandaa na kutekeleza vurugu hizo wafikishwe kwenye mkono wa
sheria. Hadi jana, watu 91 walikuwa wamekamatwa wakituhumiwa kufanya
mikusanyiko isiyo halali na uharibifu wa mali na miundombinu.
Aidha Serikali imeapa kuwa damu ya
askari wanne wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
waliokufa katika ajali wakati wakitokea Nachingwea kwenda Mtwara
kudhibiti vurugu hizo haitamwagika bure.
Hayo yamo katika kauli ya
Serikali iliyotolewa bungeni mjini hapa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kuhusiana na vurugu hizo zilizotokea Mtwara juzi.
Akiwasilisha kauli hiyo ya awali ya
Serikali bungeni kwa mujibu wa kanuni ya 49 (1) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge, Toleo la Aprili 2013, Dk Nchimbi alisema watu waliohusika na
vurugu hizo hawataukwepa mkono wa sher
ia popote pale walipo. Alisema Mei
22, mwaka huu zilitokea vurugu kubwa katika Manispaa ya Mtwara na
viunga vyake kiini kikiwa ni madai ya baadhi ya wananchi wa Mtwara
kupinga usafirishaji wa rasilimali ya gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es
Salaam.
Alisema katika kutimiza hilo, Mei 15,
mwaka huu, kikundi cha watu ambao hawakufahamika walisambaza vipeperushi
vyenye lengo la kuhimiza wakazi wa Mtwara kuwa siku ya Ijumaa Mei 17,
saa 3 asubuhi wasikilize hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini
ikisomwa bungeni ili kujua mustakabali wa gesi kutosafirishwa kutoka
Mtwara.
“Vipeperushi hivyo vilihimiza huduma
zote za kijamii zisimamishwe siku hiyo. Pamoja na vipeperushi hivyo,
tarehe 17, Mei, 2013 huduma zote za kijamii kama vile usafiri wa magari
(daladala), pikipiki (bodaboda) na baadhi ya bajaj zilifanya kazi wakati
huduma za maduka na migahawa zilifungwa.
“Hata hivyo hotuba hiyo haikusomwa
bungeni siku hiyo. Kikundi hicho kiliendelea kuhamasisha kwa kutumia
mitandao ya simu na karatasi za vipeperushi na kuwahimiza wananchi
wasikilize hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini pindi
itakaposomwa,” alisema Waziri Nchimbi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, matukio hayo
yaliendelea tena Mei 22, mwaka huu ambapo majira ya saa 4 asubuhi
makundi ya vijana waliokuwa wanasikiliza hotuba hiyo waliokuwa maeneo ya
Sokoni, Magomeni na Mkanaredi walipanga mawe makubwa, magogo na kuchoma
moto matairi barabarani.
Alisema hali hiyo iliendelea kusambaa
maeneo mengine ya mji kama vile Chuno, Chikongola, Mikindani na kutoka
nje ya mji hadi Mpapura umbali wa kilomita 40 kutoka Mtwara Mjini na
kwamba Jeshi la Polisi lilikabiliana na hali hiyo ya vurugu kwa
kurudisha katika hali ya kawaida ya usalama na kuondosha magogo na mawe
yaliyokuwa barabarani.
Akizungumzia athari za vurugu hizo, Dk
Nchimbi alisema ofisi ya Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtwara
Mjini, Hasnain Mohamed Murji iliyopo Mikindani imeharibiwa na kuibiwa
vitu mbalimbali, ofisi ya Mahakama ya Mwanzo ya Mitengo imechomwa na
kuteketea na nyaraka za ofisi.
Madhara mengine ni kuchomwa moto kwa
ofisi ya CCM ya Kata ya Chikongola, kuchomwa moto kwa nyumba binafsi ya
Ofisa Mtendaji Kata ya Magomeni, kuchomwa moto kwa nyumba ya Mwandishi
wa Habari wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) wa Mtwara, Kassimu
Mikongoro, kuibiwa na kuvunjwa kwa nyumba za askari wanne na kuibiwa
vitu mbalimbali katika Ofisi ya Kata ya Chikongola.
Alisema mpaka sasa mtu mmoja Karim
Shaibu amefariki dunia katika vurugu hizo na kwamba askari wawili
walijeruhiwa kwa bomu la kishindo. Waziri Nchimbi alisema pamoja na
kukamatwa watuhumiwa hao 91, alisema vurugu hizo zimedhibitiwa na
operesheni ya kuhakikisha hali ya usalama inarejea inaendelea.
Vifo vya wanajeshi Akizungumzia sababu
za kufa kwa wanajeshi wa JWTZ, Dk Nchimbi alisema kutokana na kuzorota
kwa usalama, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa mujibu wa sheria aliomba kwa
Waziri wa Ulinzi kuongezewa nguvu kulinda raia wasio na hatia na mali
zao na Waziri alikubali na kuelekeza JWTZ waende mara moja.
“Katika kutekeleza agizo hilo askari 32
wa Jeshi la Wananchi walianza safari kutoka Nachingwea kwenda Mtwara.
Walipokuwa njiani katika eneo la Kilimani Hewa gari lao lilipata ajali
ambapo askari wanne walifariki dunia na 20 kujeruhiwa.
“Askari hawa wamefariki na kujeruhiwa
wakati wakiwa kazini kutekeleza wajibu wa kuwalinda Watanzania wenzao.
Damu yao haitamwagika bure. Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema peponi
marehemu na awape nafuu askari na vijana wetu waliojeruhiwa.”
Alitumia nafasi hiyo kwa niaba ya Taifa
kuwapongeza na kuwashukuru askari wa Jeshi la Polisi ambao alisema
pamoja na uchache wao, juzi walifanya kazi kubwa katika mazingira magumu
ya kurejesha amani bila kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu.
Aliwapongeza pia viongozi wa Mkoa na
Wilaya ya Mtwara Mjini kwa uongozi mzuri. Sakata la bomba la gesi Kuhusu
ujenzi huo wa bomba la gesi, Waziri Nchimbi alisema suala hilo
limezungumzwa sana.
Alisema Waziri Mkuu na baadhi ya mawaziri walikwenda
Mtwara na Rais Jakaya Kikwete pia alilizungumzia suala hilo kwa kina.
“Mheshimiwa Spika, manufaa makubwa
ambayo Mtwara itayapata yamezungumzwa sana, utaratibu wa kusafirisha
kiasi kikubwa cha gesi kwa bomba ndio unaotumika duniani kote kwa sababu
za unafuu wa gharama na kuhakiki ubora wake.
“Faida zake kitaifa pia zimeelezwa sana
ikiwamo Taifa kuondokana kabisa na upungufu wa nishati ya umeme na umeme
kupatikana kwa bei nafuu na hivyo kuharakisha mapinduzi ya viwanda na
maendeleo.
“Mheshimiwa Spika, wasaliti wa Taifa
letu wanajua maendeleo makubwa yatakayopatikana Mtwara na nchi yetu
kutokana na gesi, hivyo wanatumia vibaya ufahamu wetu mdogo kuhusu gesi
na kuchochea upinzani dhidi ya mradi huu unaotarajiwa kuwakomboa wana
Mtwara na Watanzania. Watanzania na wana Mtwara lazima kwa kauli
isiyoyumba tuzikatae njama hizi.
“Tunalo Taifa moja la Tanzania ambalo
maliasili zake ni za Watanzania wote. Tabia iliyoanza kujengeka ya kila
eneo kutaka inufaike peke yake na mali za eneo hilo italigawa taifa letu
vipande vipande.
“Baadhi ya taasisi za kiraia na vyama
vya siasa kwa maslahi binafsi yasiyo na upeo mpana vinaweza kudhani
kuunga mkono madai ya namna hii ni kuimarisha kukubalika kwao miongoni
mwa jamii, tunatimiza wajibu wetu wa kuwakumbusha msemo wa wahenga
usemao “ Tamaa mbele, mauti nyuma.”
Wataipasua nchi yetu, watasababisha
vifo vya maelfu ya watu, watalijaza taifa vilema na majeruhi na
hawatanufaika na matokeo haya mabaya.”
Aidha Waziri Nchimbi alisema vita
inayofahamika kama Vita Kuu ya Afrika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC) iliyopiganwa kati ya mwaka 1998- 2003 msingi wake mkubwa
ulikuwa ni kupigania rasilimali Mashariki ya nchi hiyo na ilisababisha
vifo, magonjwa na njaa na Waziri Nchimbi alihoji.
“Je, huko ndiko tunakotaka kulipeleka
taifa letu?” Spika aahirisha Bunge Kutokana na tukio hilo, Spika wa
Bunge, Anne Makinda jana alilazimika kukiahirisha kikao cha Bunge kwa
siku nzima ili kupisha Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana ili
kutathmini kwa kina kuhusu tukio hilo kabla ya kujua nini nafasi ya
Bunge katika kulishughulikia.
Alisema asingeweza kuruhusu mjadala juu
ya tukio hilo pamoja na kwamba lilikuwa mezani kwake kwa vile kauli za
wabunge zingeweza kuchochea zaidi hali hiyo na kusababisha kutokea kwa
madhara makubwa zaidi.
Alisema wakati Bunge litakapoendelea na
kikao chake leo, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ndiyo
itakayowasilisha hotuba yake ya bajeti kwa mwaka ujao wa fedha na kwamba
majadala kuhusu hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini
itapangiwa siku nyingine.
0 comments:
Post a Comment