MTANZANIA.
KWA mara nyingine hotuba ya kambi ya upinzani jana ilichafua hali ya
hewa bungeni, hatua iliyolazimu Naibu Spika, Jobu Ndugai, kuliahirisha
Bunge. Hotuba hiyo inadaiwa kukidhalilisha Chama cha Wananchi (CUF),
kwamba kinaunga mkono sera za usagaji na ndoa za jinsia moja, maneno
yanayodaiwa kuleta kichefuchefu.
Baada ya kutokea hali ya
kurushiana maneno, Ndugai alilazimika kuahirisha Bunge na hivyo kut
oa
fursa kwa Kamati ya Maadili ya Bunge kuijadili hotuba hiyo.
Tafrani hiyo
ilijitokeza wakati Msemaji wa kambi hiyo kuhusu Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Hezekiah Wenje akiwasilisha maoni ya kambi
yake.
Hata hivyo Wenje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana,
alinusurika kupigwa na wabunge wa CUF baada ya kudai kwamba, hotuba yake
imekidhalilisha chama chao.
Wenje alikuwa akisoma maoni ya kambi yake
kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Wakati Wenje akisoma hotuba yake, Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdalla Salim (CUF), alisimama na kuomba mwongozo wa spika.
Baada ya kupatiwa nafasi hiyo, Mbunge huyo alitumia kanuni ya 68 (1) sambamba na kanuni ya 64 (1) (abc), ambapo alisema:
“Katika
hotuba hii ya kambi ya upinzani, ukurasa wa 8, paragraph ya 3 inasema:
‘Kwa upande wa Chama cha CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa
kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na kupigania
haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga,” alisema.
Kabla
mbunge huyo kumaliza kuomba mwongozo wake, baadhi ya wabunge walisikika
wakiguna huku Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy akisikika akisema
wapigwe wapigwe.
Wakati zogo hilo likiendelea, Masoud aliendelea
kuomba mwongozo wake. “Mheshimiwa Naibu Spika, maneno haya hayakubaliki
kutolewa ndani ya Bunge hili maana hayana ukweli, huu ni uzushi, uongo,
uhuni uzandiki na huu ni ushenzi.
“Imekuwa ni tabia mbaya kama
hii, Watanzania walitupa ridhaa ya muda mrefu kuja humu ndani
kuzungumza, kwa bahati mbaya kunatolewa lugha kama hizi ndani ya vitabu.
“Mimi nadhani kwa hotuba hii, Chadema waombe radhi, pili wafute kauli yao, tatu kamati ya Maadili ya Bunge ichukue nafasi yake.
“Kama
Kamati ya maadili imeona jambo hili ni dogo, CUF itachukua hatua
zinazostahili dhidi ya Bunge na Chadema, hatukubali taarifa hii, uhuni
huu na matusi haya, huu ni udhalilishaji mkubwa kupita kiasi.
“Ninakuomba
Naibu Spika, Chadema wachukuliwe hatua za kinidhamu kwanza wakome,
wakome mara mia moja narudia tena kama Bunge hawatachukua hatua, CUF
itachukua hatua kwa Bunge na Chadema,” alisema.
Pamoja na kuzuka
kwa zogo ndani ya Bunge, Naibu Spika alimpa nafasi Wenje atoe ufafanuzi
ambapo hata hivyo wakati akitoa maelezo miguno iliendelea.
“Mheshimiwa
naibu spika, with due respect (kwa heshima kubwa) ninaomba wabunge
wanisikilize, tunachozungumzia, tunazungumzia mahusiano kati ya vyama
vya Tanzania na vyama vya nje ya nchi.
“Tumeeleza kwanza CCM ina
uhusiano na vyama gani, Chadema ina uhusiano na vyama gani na misingi ya
mahusiano kwa vyama vya Tanzania na vya nje ni ideology (itikadi) zao.
“CCM
wapo socialism (ujamaa), CUF wapo liberal na Chadema ni mrengo wa kati
na kwa misingi ya liberal……….” Kabla ya kumaliza kuzungumza vurugu
zikaanza, kelele za toka toka zilisikika huku baadhi ya wabunge wa CUF
wakisimama kumfuata Wenje wakitaka kumpiga.
Baadhi ya wabunge hao
ni pamoja na Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji, Mbunge wa Ole, Rajab
Mbarouk Mohamed, Mbunge wa Mji Mkongwe, Ibrahim Sanya, Mbunge wa Lindi
Mjini, Salum Khalfan Barwany na wengine.
Baada ya Ndugai
kushindwa kudhibiti vurugu hizo, aliahirisha Bunge hadi jioni na
kuitisha kikao cha Kamati ya Bunge ya Maadili kukutana muda huo.
Hata
hivyo wabunge hao wa CUF waliendelea kumfuata Wenje licha ya kuzuiwa na
baadhi ya wabunge wenzao, huku baadhi yao wakisikika wakitukana matusi
ya nguoni.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy Mohamed (CCM) alisikika akisema ‘mdundeni huyo, leo wapo wachache.
Sauti
nyingine zilizokuwa zikisikika ni pamoja ‘mambo ya kishenzi wafanyieni
haohao’ huku Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara (CUF), akisikika
akisema: “Hakisomwi kitu chezeni na wabunge wa CCM, sisi tunapiga.”
Wakati
huo Wenje alionekana akitolewa nje akisindikizwa na Mbunge wa Mtera,
Livingstone Lusinde (CCM), Mbunge wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere
(Chadema) na askari mmoja wa Bunge.
Wenje alisindikizwa hadi nje ya Ukumbi wa Bunge na kupelekwa katika Ofisi za Kambi ya Upinzani bungeni.
Hali ilivyokuwa nje.
Wabunge wa CUF walikusanyika katika viwanja vya Bunge, huku baadhi yao wakiporomosha matusi ya nguoni dhidi ya Chadema.
Baadhi
ya wabunge wa CCM walionekana kuwaunga mkono wabunge hao wa CUF, kwa
kupinga kile ambacho kilikuwa kimeandikwa katika hotuba ya kambi ya
upinzani.
Kwa upande wake Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji
akizungumza na waandishi wa habari nje ya viwanja hivyo alisema: “CUF
walikuwa tayari kumpiga mtu kuliko kuruhusu hotuba ile kusomwa bungeni,”
alisema.
Khatib alisema msimamo wa CUF siku zote unajulikana
kuhusu kupinga vitendo vya ushoga na ndoa za jinsia moja, hivyo
akashangaa maneno yaliyotolewa.
Hotuba ya Wenje.
“CCM wao
wanajiita kuwa wapo mrengo wa kijamaa/kikomunisti na wamekuwa wakipokea
misaada mingi sana ya fedha na nyenzo kutoka umoja wa vyama vya
kikomunisti ulimwenguni.
“CCM imekuwa ikipokea misada katika nchi
kama za Ujerumani kupitia SDP, Uingereza kupitia Chama cha Labour,
China kupitia Chama cha Kikomunist, Marekani kupitia Chama cha
Democrats.
“Kwa upande wa chama cha CUF, kutokana na itikadi
zake za mrengo wa kiliberali ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni
pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga.
“Hii
ni kwa mujibu wa tangazo lao kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali
ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza,
Lynn Featherstone kutoka chama cha Liberal Democrats.
“Kutokana
na umoja huo, CUF wamekuwa wakipata msaada wa kifedha na nyenzo nyingine
mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vya mrengo wa kiliberali na msaada wa
mwisho ni hivi majuzi Machi 2013, waliposaini makubaliano na chama cha
kiliberali kutoka Norway.
“Kambi ya Upinzani Bungeni, inavitaka
vyama vyote ambavyo vimekuwa na mahusiano na vyama vya nje viweke wazi
mikataba yao na malengo ya mahusiano hayo, ikiwa ni pamoja na misaada
ambavyo vimekuwa vikipokea kutoka kwenye nchi hizo,” ilieleza hotuba
hiyo.
BUNGE LILIVYOKUWA JIONI.
Bunge liliporudi jioni,
Naibu Spika, Job Ndugai alimtaka Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kinga,
Haki na Maadili ya Bunge, John Chiligati kuelezea uamuzi uliofikiwa na
kamati hiyo.
Chiligati alisema baada ya kamati kuzungumza na
Wenje na mlalamikaji ambaye ni Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdalla Salim
(CUF, Kamati iliamuru Wenje aombe radhi kwa CUF na maneno yale ya kuudhi
yafutwe.
Alisema kwa upande wa mlalamikaji, alikubali mambo hayo mawili yafanyike.
“Baadae
Wenje alileta mabadiko ya kitabu cha Kambi Rasmi ya Upinzani katika
kamati, hata hivyo hakukuwa na mabadiliko yoyote zaidi ya mabadiliko ya
lugha ikiwemo matumizi ya lugha ya kiingereza lakini maneno ni yaleyale.
“Hata
pale Kamati ilipomtaka aombe radhi, Mheshimwa Wenje alikataa kwa madai
kwamba katika maneno yale hakulenga CUF bali alilenga vyama vya kisiasa
duniani vyenye mrengo wa kiliberali.
“Kamati imeamua kiti chako,
Naibu Spika kimuamuru Wenje kuondoa maneno na awe muungwana aondoe
maneno yake hata kama aliyasema kwa nia njema,” alisema Chiligati.
WENJE APEWA NAFASI.
Baada
ya kupewa dakika tano, Wenje alisema ni kweli CUF ilijiunga na vyama
vya kiliberali mwaka 1997 na kuonyesha mkataba ambao vyama kiriberali
vilikubaliana katika kulinda haki za mtu mmoja mmoja ikiwemo kutambua
ushoga na usagaji.
“Ni kweli CUF ni chama cha kiriberali,
mheshimiwa Spika, nimedhalilishwa leo, nimetukanwa na wamefanya fujo
bungeni, kamati inahitaji nifute maneno ya ukweli, niombe msamaha kwa
kosa lipi?,” alihoji Wenje.
MASOUD AZUNGUMZA.
Baada ya
maelezo ya Wenje, Ndugai alimpa nafasi mlalamikaji ambaye alisema
msimamo wake upo palepale na kama Wenje hataomba msamaha na kufuta
maneno yake, wabunge wa CUF hawataruhusu hotuba yake isomwe.
Mbunge
mwingine aliyeomba mwongozo ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema)
na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde ambaye alitaka Wenje asisome
tena hotuba yake na majadiliano yaendelee.
NAIBU SPIKA AMRUDIA WENJE.
Ndugai alimtaka Wenje kwa mara nyingine kuomba msamaha na kusoma hotuba yake kwa kuruka vipengele vilivyolalamikiwa na CUF.
Wenje
alienda mbele na kukubali kuruka vipengele hivyo lakini badala ya
kuomba msamaha, aliendelea kusoma hotuba hiyo hali iliyosababisha
wabunge wa CUF kusimama.
Naibu Spika ilimlazimu kumkatisha Wenje na kumtaka arudi alipokaa.
“Kwa
mara nyingine tena, nalipeleka suala hili katika Kamati ya Haki,
Maadili na Madaraka ya Bunge na naliahirisha Bunge hadi kesho na
tutakapoendelea na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,” alisema
Ndugai.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment