SOMA SABABU YA KUYOTOA HAPA.
MCHEZA
sinema maarufu wa Kimarekani, Angelina Jolie, ametangaza kwamba
amefanyiwa operesheni ya kuondosha matiti yake yote mawili ili kupunguza
uwezekano wa kupata saratani ya maziwa na ya kizazi.
Kwa mujibu wa makala yake iliyochapishwa leo kwenye gazeti la The New York Times na
kupewa jina "Chaguo langu la kitabibu", Angelina Jolie amesema ameamua
kutangaza jambo hilo hadharani ili kuwapa moyo wanawake wengine wenye
historia ya familia zinazouguwa saratani.
Sasa muigizaji
huyo maarufu wa sinema duniani, anasema anawataka wanawake wenye hali
kama yake kutafuta ushauri wa kitabibu na kufanya uamuzi baada ya kuwa
na taarifa za kutosha ili waweze kuendelea kufanya kazi, kama
alivyofanya yeye.
"Licha ya kuweza kulifanikisha
hili na kubakia kimya kwa muda mrefu, sasa naandika kulitangaza kwa
sababu natarajia kuwa wanawake wengine wanaweza kufaidika na uzoefu
wangu."
Ameandika mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya masuala
ya wakimbizi.
Uamuzi mgumu lakini muhimu
Jolie aliamua kufikia uamuzi
huo wa kuyaondosha matiti yake yote mawili, kwa sababu alifahamishwa na
madaktari wake kwamba alikuwa na chembechembe inayoongeza hatari ya
kupata saratani kwenye maziwa yote mawili na kwenye fuko lake la uzazi.
Kutokana na chembechembe hiyo
iitwayo BRCA1, madaktari walikisia kwamba alikuwa kwenye kiwango cha
asilimia 87 ya hatari ya kupata saratani ya maziwa na asilmia 50 ya
kupata saratani ya kizazi.
Mama yake mwenyewe Angelina
alifariki akiwa na miaka 56 kutokana na maradhi hayo.
"Baada tu kujua kwamba huo
ndio ukweli kuhusu hali yangu, niliamua kuchukua hatua za kabla na
angalau kupunguza kiwango hicho cha hatari kadiri nilivyoweza. Nikafanya
uamuzi wa kuondosha matiti yangu yote mawili.
Nilianza na maziwa kwa
kuwa saratani ya maziwa ni kubwa zaidi kuliko hatari ya ile ya fuko la
uzazi, na operesheni ya fuko la uzazi ni kubwa zaidi," ameandika Jolie.
Jolie na mumewe, ambaye pia ni
muigizaji maarufu, Brad Pitt, wana watoto watatu wa kuwazaa na watatu
wa kuwalea, na ameandika kwamba sasa anaweza kuwaambia watoto wake
kwamba hawapaswi kuwa na hofu ya kumpoteza mama yao kwa sababu ya
saratani.