SERIKALI imesema kuwa mapambano
yaliyozuka katika mgodi wa Buhemba uliopo Butiama mkoani Mara kati ya
wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Usimamizi wa Madini (STAMICO) na
wachimbaji wadogo yalisababishwa na kutoelewana kati yao.
Aidha Serikali imetahadharisha uvamizi
kwenye maeneo ya leseni kubwa za utafiti unatishia nchi kukosa miradi
mikubwa katika migodi mpya siku za usoni.
Kauli hiyo ya Serikali inakuja baada ya
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR- Mageuzi) kutaka kauli ya
Serikali kutokana na tatizo lililopo kati ya Stam
ico na wachimbaji
wadogo, hali iliyopelekea wafanyakazi wa Stamico kupigwa na je, Serikali
inawaambia nini wana Buhemba ili kuwapa uwezo na si kuthamini watu
wawekezaji wa nje tu.
Akijibu swali hilo la nyongeza bungeni
mjini Dodoma mwishoni mwa wiki Naibu Waziri wa Madini, Steven Masele
alisema kulikuwa na mapambano kati ya watu wa Stamico na wachimbaji
wadogo siku ya Alhamisi lakini Wizara inaendelea kufanya utaratibu wa
kuhakikisha wachimbaji wadogo wanatengewa maeneo.
Katika swali la msingi, Mbunge wa
Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM), alitaka kujua Serikali ina mpango gani
wa kuwasaidia mitaji na nyenzo za kufanyia kazi wachimbaji wadogo katika
migodi ya kata za Songwa, Mwadui, Lohumbo, Uchunga, na Mondo ambao
wanamiliki kihalali maeneo hayo ili waweze kunufaika na rasilimali hizi.
Naibu Waziri alisema Serikali inatambua
na kuthamini mchango wa wachimbaji wadogo katika kuinua uchumi na pato
la taifa, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira.
Alisema inakadiriwa Watanzania wapatao
milioni moja wanajishughulisha na kazi hiyo nchini na kutokana na hali
hiyo kuanzia mwaka 2009/2010 Serikali ilianzisha mpango wa kutenga fedha
ili kuendeleza shughuli za wachimbaji wadogo ili waweze kununua vifaa
bora vya uchimbaji na uongezaji thamani madini.
Masele alisema kampuni mbalimbali
zilizokopeshwa fedha kwa ajili ya kuanzisha vituo vya ukopeshaji na
ukodishaji wa vifaa vya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo ni pamoja na
Stamico waliopata shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha
kukodisha vifaa vya uchimbaji madini eneo la Rwamgasa, wachimbaji
watakaoweza kununua vifaa hivyo kwa utaratibu wa kukopeshwa kisha kulipa
kidogokidogo watafikiriwa.
Pia Tan Discovery Mineral Consultancy
Co. Limited shilingi milioni 180 ambao tayari wameanzisha kituo cha
kukopesha vifaa eneo la Londoni Singida, kampuni ya Kilimo & General
Suppliers Limited shilingi milioni 60 ambapo ujenzi wa kituo kwa ajili
ya usagaji mawe ili kupata kokoto unaendelea.
Kampuni nyingine ni Gemsyle shilingi
milioni 35 kwa ajili ya uongezaji thamani ya madini na vito na C.E
Holding shilingi milioni 50 kwa ajili ya uongezaji thamani madini.
Masele alisema kuwa, wachimbaji wadogo
katika maeneo ya Songwa, Mwadui, Lohumbo, Uchunga na Mondo wana fursa ya
kupata mikopo kupitia kwenye utaratibu unaotakiwa na mikopo hiyo
itakuwa ikipitia benki kwenye dirisha la wachimbaji wadogo.
Aliwashauri wachimbaji katika maeneo
hayo kuungana ili iwe rahisi kukopesheka na kutoa wito kwa wachimbaji
wote waliovamia maeneo ya wawekezaji wengine kuacha vitendo hivyo na
badala yake waendeleze maeneo wanayomiliko kwa mujibu wa sheria.
0 comments:
Post a Comment