Fadina Salum akiwa amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Ligula mkoani
Mtwara akiuguza majeraha ya risasi kufuatia fujo zilizozuka hivi
karibuni.(Picha na Khalfan Said).
WAKATI hali ya utulivu na amani ikielezwa kuwa imeanza kurejea katika mkoa wa Mtwara, imedaiwa kuwepo idadi kubwa ya majeruhi wa risasi waliolazwa katika hospitali ya mkoa wa Mtwara.
Mganga Mkuu wa mkoa, Dk. Sadun Kabuma,
amethibitisha kupokea majeruhi 30, ambapo 15 wana majeraha ya risasi
sehemu tofauti za miili yao.
Alisema, watu watatu walithitishwa
kufariki dunia akiwemo mjamzito Fatuma Mohamed, aliyefikis
hwa
hospitalini humo akiwa amekufa,ilibainika alipigwa risasi upande wa
kulia iliyochana mfuko wa uzazi.
Alisema risasi iliyotumika ilikiua kiumbe kilichokuwa na umri wa miezi sita na kutokea upande wa kushoto mwa tumbo.
Pia alisema , marehemu wa kwanza, Karim
Shaibu (22), alibainika kupigwa risasi risasi iliyochana ini na
kusababisha damu kujaa kwenye kifua.
Pia hospitali imepokea wanawake na watoto
zaidi ya 60, wakiomba hifadhi ya muda kwenye hospitali hiyo, na wengi
walilala na kupatiwa chakula kwa siku hiyo hadi hali ilivyotulia
wakarudi nyumbani kwao.
Akizungumzia hali katika Hospitali ya
Ndanda wilayani Masasi, alisema wanajeshi wanne waliojeruhiwa katika
ajali ya gari wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, walifanyiwa upasuaji
wa mifupa na wanaendelea na matibabu.
Alisema wawili kati yao hali ni mbaya wanatarajiwa kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kwa matibabu zaidi.
Alikizungumzia majeruhi wengine, Dk.
Kabuma alisema sita walipata mshtuko na tisa walikuwa na majeraha
yasiyohusiana na risasi na kwamba polisi watatu na mwanajeshi mmoja,
wamelazwa hospitalini humo.
Amina Abdalah na Athumani Ally, wakazi wa
mjini humo, walisema wanashukuru uwepo wa JWTZ kwa kuwa hawapigi,
kupora, kuua au kujeruhi raia kama walivyotendewa na polisi.
Baadhi ya majeruhi waliozungumza na gazeti
hili ni pamoja na, Fadina Salum, mkazi wa Mtaa wa Matupeni, aliyesema
kuwa Alhamisi wiki hii, alitoka mafichoni porini akiwa na mwanae, Amani
Tizo (14), baada ya kuona hali imerejea kwa utulivu.
Mwanafunzi Heri Fokasi, alisema siku ya
tukio alikuwa na kaka yake wakiwa nje ya nyumba yao, gari ya polisi
ilifika na kuwaweka chini ya ulinzi na kuwapiga na kisha kuwataka
wanyanyuke.
Katika hatua nyingine , askari wa Jeshi la
Wananchi (JWTZ) wameimarisha doria sehemu tofauti mkoani hapa, huku
serikali ya mkoa ikiwataka raia waendelee na shughuli zao.
Shughuli za uchumi na za kijamii zimerejea kama ilivyokuwa kabla ya machafuko ya hivi karibuni.
Katika eneo la kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani, usafiri ulikuwa kama kawaida.
Wananchi katika baadhi ya maeneo,
walikusanyika kwa vikundi, wakijadili mambo tofauti na wakati mwingine
kuzungumza na askari wa JWTZ.
Hata hivyo, usiku wa kuamkia jana,
ilisikika milio ya mabomu , hivyo kuzua taharuki kwa wananchi.
Haijajulikana yalikuwa yanarushwa na watu gani na hata Kamanda wa Polisi
wa mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, alipouliza alisema huenda walikuwa
wavuvi wa baharini.
Aidha, taarifa zilizopatikana baadhi ya wananchi wameanza kuondoka kwenda mikoa ya jirani kupumzika kutokana na vurugu hizo.
Hata hivyo, taarifa zilizothibitishwa na Mkuu wa mkoa, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, zilieleza kuwepo
vurugu katika kijiji cha Madimba, eneo la Msimbati ambako kutajengwa mtambo wa kuchakata gesi.
Wananchi hao wanataka viwanda vya
kuchakata gesi vijengwe mkoani humo ili pamoja na mambo mengine, vitoe
ajira na kukuza uchumi wa mkoa huo ulio kusini mwa nchi.
Wakati huo huo Jeshi la polisi limetuma
kikosi kazi kuchunguza uhalifu uliotokea, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba.
Moja ya majukumu ni kuchunguza tuhuma za kubaka, kuharibu mali na kutesa raia zinazodaiwa kufanywa na polisi.
SOURCE:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment