MTANZANIA.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Harold
Sungusia
Heka heka za kupokea majeruhi Hospitali ya Ndanda hivi karibuniNyumba ya Mbun
ge wa Masasi Mariam Kasembe ikiungua moto hivi karibuni.
VURUGU zilizofanyika hivi karibuni mkoani Mtwara zimechukua sura mpya,
baada ya mambo mazito yenye sura ya kinyama ndani yake kuibuliwa.
Utafiti uliofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s), umebaini
watu zaidi ya 12 wamepoteza maisha katika vurugu hizo tofauti na takwimu
za watu watatu wanaotajwa na Serikali.
Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na Mtandao wa Haki za Binadamu
Kusini Mwa Afrika (SAHRINGON).
Akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Harold
Sungusia alisema utafiti huo wa muda mfupi umebaini kasoro katika
takwimu za Serikali kuhusiana na vifo vya watu.
Sungusia alisema
utafiti uliofanywa na shirika lake umebaini kuwapo kwa vitendo vya
ubakaji wa wanafunzi wa vyuo, huku wazee wa kimila wakidaiwa kuchinja
mbuzi za tambiko kupinga ujenzi wa bomba kwa ajili ya kusafirisha gesi.
Vifo
Sungusia alidai kuwa wamebaini vifo vilitokea katika
vurugu hizo ni zaidi ya 12 na kwamba shirika lake linaendelea kuhakiki
majina ya watu waliofariki dunia na taarifa zao nyingine.
Sungusia alitoa shutuma nzito kwa askari polisi kwamba ndio waliohusika na ongezeko la vifo hivyo.
“Hivi
vifo ni kutokana na askari polisi kuvamia nyumba za wananchi, kuvamia
maduka na kuingia ndani na kupiga mabomu ya machozi, huku wakiiba mali
za raia zikiwamo televisheni, redio na fedha,” alisema.
Alisema
timu ya watafiti hao inaendelea kuzungumza na wazazi na familia
zilizopoteza ndugu zao ili kuwa na uhakika wa majina yao, umri na maeneo
walipozikwa.
Sungusia alisema katika hali isiyo ya kawaida,
taasisi za Serikali zikiwamo hospitali na polisi zimeshindwa kutoa
ushirikiano wa karibu pale walipotakiwa kutoa taarifa halisi kuhusu
madhara ya vurugu hizo.
“Tumezungumza na baadhi ya wakazi wa
Mtwara juu ya mambo mbalimbali kuhusu gesi na athari zilizotokea katika
vurugu za hivi karibuni.
“Walieleza ndugu zao waliokufa na baadhi tumepata majina yao, tutayaweka baada ya kukamilisha taarifa zote,” alisema.
Matambiko ya kimila
Alisema
kuwa katika vurugu hizo zilizotokea, wamebaini kuwa tayari baadhi ya
wazee maarufu wa kimila wamekwishafanya matambiko yao na kuwapa vijana
imani ya kuapishwa juu ya kutetea na kulinda rasilimali za Mtwara
zisitoke bila wao kuridhia.
“Tumezungumza na wazee wa kimila na
wakakiri kwamba walikwishafanya matambiko yao na kutoa mbuzi wawili kama
kafara, mbuzi mmoja alichinjwa wakanywa damu na wa pili alipelekwa eneo
lenye gesi na kufanya matambiko yao.
“Katika matambiko yao
walikubaliana kama mbuzi huyo akipiga magoti, basi gesi hiyo haitatoka
Mtwara na kama angesimama ingeashiria inatoka. Wanasema mbuzi wao
alipiga magoti.
“Pia tumeelezwa kwamba, vurugu hizo zilichochewa
na taarifa zilizotolewa na wavuvi wanaovua kina kirefu cha bahari
kwamba, kuna meli imetia nanga baharini na inavuna gesi na inaipeleka
ng’ambo kupitia Nyambizi yaani Sub-marine.
“Kutokana na hali
hiyo, wananchi wa Mtwara walianza kuhamasishana mjini hadi vijijini na
kuwa na msimamo wao wa lugha ya kimakonde kama ‘AIYUKI’ yaani haitoki,”
alisema.
Ubakaji
Sungusia alisema wanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa
Umma, Chuo cha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Chuo cha
Mtakatifu Augostine ni miongoni mwa watu walioathiriwa.
Alisema
wanafunzi hao walivamiwa na polisi wakiwa njiani wakienda mjini
kujifunza kwa vitendo ‘field’ na kufanyiwa vitendo hivyo vibaya.
Alisema
licha ya wananchi wa Mtwara kushukuru askari wa Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) kurejesha amani, lakini wameendelea kuwa na hofu kubwa.
CUF kukutana na Wanamtwara
Wakati huo huo Chama cha Wananchi
(CUF), kimeandaa kongamano kubwa kwa ajili ya wananchi wanaotoka Mtwara
na Lindi waishio jijini Dar es Salaam, ili kujadili kwa uwazi tukio la
Mtwara.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam na waandishi wa
Habari Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kongamano hilo
litafanyika Juni 2, mwaka huu.
Alisema CUF imeamua kufanya
kongamano hilo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi
wakilalamikia hatua ya Serikali kutosikiliza kilio chao.
“Baada
ya majadiliano ya kina mawazo ya wananchi yatakusanywa kisha kupelekwa
kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na Spika wa Bunge, Anne Makinda ili
waweze kuyachambua nao kwa nafasi zao na kuyachukulia maamuzi,” alisema
Mtatiro.
Alisema kuwa chama chake kinafanya hivyo kutokana na
vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano katika mikoa ya kusini katika
kipindi hiki.
“Sisi vyama vya siasa hatuna mtutu wa bunduki, ila
tunatoa elimu kwa wananchi ni wapi tumeyumba kiuchumi na nini kifanyike
katika kuiondoa CCM madarakani,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Benjamin Masese, Christina Gaulahanga na Adelina Rutale.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment