WANAJESHI saba wa Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa wakati wakilinda amani Darfur
nchini Sudan, walipigana kwa saa mbili wakati wakijitetea kabla ya
kufikwa na mauti.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini,
Jenerali Davis Mwamunyange, alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati
akitoa salamu za rambirambi, wakati wa kuaga askari hao waliouawa Julai
13.
Katika shughuli hiyo iliyofanyika Makao
Makuu ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), Rais Jakaya Kikwete alion
goza
waombolezaji kuaga mashujaa hao ambapo pia Makamu wa Rais, Dk Mohammed
Gharib Bilal na mawaziri mbalimbali walihudhuria.
“Kikundi hicho (askari wa JWTZ) kilikuwa
kikitokea eneo la Abeche, kwenda Nation na kilipofika umbali wa
kilometa 25, doria hiyo ilipunguza mwendo kutokana na utelezi wa matope
yaliyosababishwa na mvua.
“Ghafla kikundi hicho kilishambuliwa na
watu ambao hawakufahamika, wakitumia silaha nzito za kivita,” alisema
Jenerali Mwamunyange.
Alisema ulikuwa ni mtego wa mashambulizi
na kwa mujibu wa taratibu za operesheni hizo, doria hiyo haikuwa na
silaha nzito, lakini ililazimika kujibu mapigano hayo hadi kikundi
kingine cha askari wa JWTZ, kilipoitwa kuongeza nguvu kunasua wenzao
katika mtego huo.
Jenerali Mwamunyange alisema wakati
kikundi hicho kikinasuliwa, askari hao walipoteza maisha kwa ujasiri
mkubwa na wengine 14 kujeruhiwa.
Alisema Tanzania imefikwa na msiba huo
wa mashujaa, ikiwa imeshiriki kulinda amani Sudan tangu mwaka 2007,
ambapo askari wake wamekuwa wakitekeleza majukumu yake kwa weledi wa
hali ya juu, kwa kushirikiana na vikundi vingine na wenyeji katika
maeneo ya operesheni.
Majina yao Awali Kaimu Msemaji wa JWTZ,
Meja Joseph Masanja, alitaja majina ya mashujaa hao na mahali
wanapokwenda kuzikwa, kuwa ni pamoja na Sajini Shaibu Othman (Zanzibar)
na Koplo Osward Chaulo (Kilolo, Iringa). Wengine ni Koplo Mohammed Ally
(Zanzibar), Koplo Mohammed Chukulizo (Kigoma), Praiveti Rodney Ndunguru
(Songea), Praiveti Fortunatus Msofe (Tanga) na Praiveti Peter Werema
(Tarime, Mara).
Rais Kikwete alisema mauaji ya wanajeshi
hao, yalimshitua, kumhuzunisha na kumkasirisha na kujikuta akijihoji
kwa nini watu wa Sudan waue Watanzania.
Alisema Watanzania hao walikwenda
kuwasaidia kupata amani, utulivu, kunusuru maisha yao na kuwaondolea
mazingira ya wasiwasi ili wafanye shughuli zao kwa tija.
Alisema tangu kuanza kwa shughuli za
ulinzi wa amani Darfur, walinzi wa amani 41 kutoka mataifa mbalimbali
wameuawa, na 55 kujeruhiwa na hakusita kuamini kuwa waliofanya tukio
hilo ni wasiotaka amani Darfur.
“Idadi hii ni kubwa, inahitaji
kutafakari vizuri na kutazama upya mfumo wa kiwango cha kujilinda kwa
wanajeshi… lazima uwezo huo uongezwe ili kupunguza vifo zaidi,” alisema
Rais Kikwete.
Aliahidi kufikisha maombi hayo kwa Umoja
wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN), ili walitazame vizuri. Mchango
wa Tanzania Rais Kikwete alisema Tanzania tangu Uhuru imekuwa
ikijitolea kusaidia wanyonge dhidi ubaguzi, uonevu na wengine ambao njia
za diplomasia zimekuwa zikitumika.
Aidha, alisema wakati wote walipoombwa,
walijua uwezekano wa askari wao kujeruhiwa au kupoteza maisha, ni mambo
yaliyofikiriwa kuwa yanaweza kutokea kwani walikwenda kwenye maeneo ya
hatari, yenye mapigano.
Alisema kutokea hayo si ajabu, lakini
hadhari kubwa ilichukuliwa kwa kupewa mafunzo, zana za kujihami,
kujilinda na kutekeleza majukumu.
Rais Kikwete alisema baada ya mauaji
hayo ya Darfur alizungumza na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon ambaye
alielezea masikitiko yake na kutoa pole nyingi, na kueleza kwamba
alizungumza na Rais wa Sudan, Omar Al-Bashir, ili achukue hatua ya
kusaka na kuwaadabisha wahalifu hao.
“Nami pia nilifanya mazungumzo na Rais
wa Sudan, na alielezea masikitiko yake na nilimsisitizia umuhimu wa
Serikali yake kufanya hivyo, kwa kuwa tukio hilo limetokea huko na hivyo
waliofanya hivyo ni Wasudani,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alimsisitiza, kwamba kwa kuwa
mauaji hayo yamefanyika katika mamlaka ya Sudan, waliohusika wawe Waasia
au Wasudani, lakini achukue hadhari zote kuwasaka.
Waziri Ulinzi Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema Watanzania wamesikitishwa
na mauaji hayo na inaweza kuwa mkakati wa kufifisha juhudi za UN kuleta
amani.
“Wizara itatoa kila msaada kuwezesha maziko na kusaidia familia za marehemu na waliojeruhiwa,” alisema Nahodha.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Meja Jenerali Salum Mustapha
Kijuu, Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu, alisema tukio hilo linasikitisha
na ni msiba wa Taifa kwa kuwa askari hao walikufa kazini na ni
mashujaa.
Katika eneo hilo, miili ya wanajeshi hao
iliingia kila mmoja kwa gari maalumu la Jeshi na kupokewa na maofisa wa
JWTZ na kupelekwa sehemu iliyoandaliwa kuagwa. UN itatoa medali kwa
kila askari, kwa kutambua mchango wao. HABARILEO
0 comments:
Post a Comment